*Kasi yake yakisiwa kuwa namba moja Afrika.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imempongeza Waziri wa Nishati
Mhe. Dkt. Medard Kalemani kwa kasi yake ya kusambaza umeme vijijini
ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 80 ya vijiji vyote nchini
vimepelekewa huduma ya umeme.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Seif
Khamis Gulamali baada ya kuwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu
Muundo na Majukumu ya Wizara ya Nishati kwenye kikao cha Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika leo tarehe 20 Mwezi
Januari, 2021 Bungeni jijini Dodoma.
Mhe. Seif Khamis Gulamali
amesema, kasi ya usambazaji umeme vijijini ni kubwa na yawezekana
Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika inayoongoza katika usambazaji wa umeme
vijijini.
Akizungumza kufuatia pongezi hizo, Waziri Kalemani
amesema, Wizara ya Nishati itahakikisha vijiji vyote 2200 vilivyobakia
ambavyo bado havijaunganishwa na umeme, vinapatiwa huduma hiyo ndani ya
miezi 18 kuanzia sasa.
Akijibu swali kuhusu maeneo yenye
changamoto ya ukatikaji wa umeme hapa nchini, Waziri Kalemani ameeleza
kuwa, kwa upande wa Dodoma , Dar-es-salaam na Mwanza, Wizara ya Nishati
kupitia ofisi ya TANESCO imefunga mitambo yenye uwezo wa kutoa umeme wa
kutosha hivyo endapo kutatokea kukatika kwa umeme kutakuwa kumetokana
na hitilafu ya kiufundi.
Dkt. Kalemani ameeleza bayana kuwa, kwa
upande wa jiji la Dodoma, Wizara ya Nishati kupitia Shirika lake la
TANESCO imekamilisha Mradi wa MW 400 na mahitaji ya Dodoma kwa sasa ni
MW 45 tu hivyo umeme upo wa kutosha. "Iwapo kutatokea kukatika kwa umeme
kwa jiji la Dodoma hiyo itakuwa kuna tatizo la kiufundi lakini si kwa
mitambo ya umeme kuelemewa ." Amesema Waziri Kalemani.
Waziri
Kalemani amekiri kuwa, kulikuwa na tatizo la umeme kwa mkoa wa Ruvuma
isipokuwa eneo la Masasi na Tunduru na kueleza kuwa kuna vifaa vya
kuboresha nguvu ya umeme ( Automatic Voltage Regulators - AVR )
vinaendelea kufungwa ili kuongeza umeme uwe mkubwa kwa ajili ya
watumiaji.
Dkt. Kalemani amemhakikishia Mhe. Mha. Stella Manyanya
mbunge wa Nyasa aliyehoji kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme katika
jimbo la Nyasa kuwa, ufungaji wa vifaa vya AVR utakuwa umekamilika ndani
ya miezi mitatu kuanzia sasa na hivyo upatikanaji wa umeme katika
maeneo husika utaimarika.
Akijibu swali kuhusu ratiba ya
utekelezaji wa kazi za Wakandarasi katika maeneo yanayopitiwa na miradi
ya umeme, Waziri Kalemani amesema, "tumewasihi sana Wakandarasi
wanapofika kwenye maeneo husika, wakutane nanyi Waheshimiwa Wabunge na
Wakuu wa Wilaya. kwanza, kutoa taarifa kuwa wameingia kwenye maeneo yenu
lakini pia wajue wanaanzia maeneo gani yenye kero ili kushauriana nao
mahali pa kuanzia. Tutakapokuwa tunazindua tutawakabidhi kwenu
Wakandarasi hao ili mkae nao wajue waanzie wapi." Amesema Dkt. Kalemani.
Akielezea
kuhusu tatizo la upatikanaji wa mafuta kwa maeneo ya vijijini na miji
midogo, Dkt. Kalemani ameieleza Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini kuwa, Wizara ya Nishati ina mpango wa kuendelea kusambaza Vituo
vya Mafuta katika maeneo ya vijijini na miji midogo kwa ajili ya
kuongeza upatikanaji wa Nishati ya Mafuta na usalama kwa watumiaji wa
maeneo tajwa yanayokabiliwa na upungufu wa mafuta.
Waziri
Kalemani amefafanua kuwa, katika utekelezaji wa suala hilo, kanuni
zinapitiwa ili kupunguza gharama za uwekezaji wa vituo vya mafuta katika
maeneo ya vijijini na miji midogo ikizingatiwa kuwa kujenga kituo cha
kawaida cha mafuta inagharimu shilingi 500,000,000/= ambazo ni nyingi
kwa wawekezaji wa vijijini.
Dkt. Kalemani amesema. Wizara ya Nishati, inafikiria kujenga vituo rahisi vya pampu moja, ambavyo uwekezaji wake utakuwa nafuu.
Kikao
hicho cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichoanza
leo jijini Dodoma kimekutana na Uongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi
zake na kitarajiwa kukamilika tarehe 22 Januari, 2021.
Makamu M/Kiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini Mhe. Seif Khamis Gulamali na Katibu wa kamati hiyo Bi. Felister
Mgonja pamoja na wajumbe wa Kamati tajwa hapo juu, wakifuatilia kwa
makini maelezo ya Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani alipokuwa
akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati Kuhusu Muundo na Majukumu ya
Wizara kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo tarehe
20 Januari, 2021 Bungeni jijini Dodoma. Kulia kwa Waziri Kalemani, ni
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Leonard Masanja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...