WAZIRI wa Kilimo Prof. Adolf
Mkenda amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ina mpango wa kuongeza nguvu
uzalishaji wa zao la alizeti kwa lengo la kuhakikisha kuwa kuna mafuta ya
kutosha ya kula yanayozalishwa nchini na hivyo kupunguza utegemezi wa mafuta
hayo kutoka nje.
Kwa mujibu wa takwimu
zilizopo sasa uzalishaji wa ndani unakidhi asilimia 43. Aidha nchi
inazalisha tani 270,000 za mafuta ya kula kila mwaka na huagiza nyingine
tani 600,000 kufidia pengo lililopo ndani.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf
Mkenda ameyasema hayo leo mchana tarehe 22 Januari, 2021 wakati alipofanya
ziara ya kukitembelea kiwanda cha kusindika mafuta ya kula ya alizeti; Kiwanda
cha Pyxus Agriculture Tanzania cha Jijini Dodoma.
Prof. Mkenda amesema kwamba
pamoja na kuongeza nguvu kuhakikisha kwamba mafuta ya kula yanapatikana nchini
kwa kiasi kinachotakiwa pia serikali itaendelea kuboresha mazingira ya
uwekezaji na kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwawezesha wawekezaji na pia wakulima
wadogo kuwa nafasi ya kusafirisha bidhaa zao nje.
Prof. Mkenda amesema kwamba
anafahamu kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanasababishwa kukwama kwa
uzalishaji mkubwa wa mafuta nchini hivyo Serikali itapitia upya Sheria na
kanuni ili kuondoa mkwamo na kuwezesha uzalishaji wa ndani kukua zaidi.
Waziri Mkenda alisisitiza
kuwa hakuna mageuzi ya kiuchumi yanayoweza kutokea bila kuwa na mapinduzi
kwenye kilimo.
"Tukiongeza tija kwenye
kilimo, bei za bidhaa kama chakula itapungua, mageuzi kwenye kilimo yatasaidia
sana kukuza viwanda hapa nchini.” Amesisitiza Prof. Mkenda.
Waziri wa Kilimo amesema
suala la mbegu za alizeti ni changamoto lakini Serikaĺi itahakikisha mbegu za
kutosha zinapatikana. Pia alitaka kuangaliwa kwa mfumo wa kilimo cha mkataba
kwa kuboresha mfumo wake.
"Tabia ya Watu kuingia
mkataba lakini wakati wa kuvuna wanampa mtu mwingine haipendezi, lazima Wakulima
waheshimu mikataba.” Amekaririwa Prof. Mkenda.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa
ataitisha mkutano wa Wataalamu ili kuangalia upya sera na taratibu zinazotumika
katika uzalishaji wa alizeti nchini.
Hata hivyo alikiri kwamba
mahitaji ya mafuta ya kula nchini yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa
corona ambao umesababisha mwenendo usiokuwa wa afya wa biashara ya kimataifa
ikiwamo ya mafuta ya kula.
Waziri pia aliwaambia
Wamiliki wa Kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania kwamba Serikali haijazuia
upelekaji wa mafuta ya kula nje na kwamba kuchelewa kwa maofisa wa Serikali
kutoa vibali kunaathiri Wakulima wadogo hapa nchini ambao wanategemea kiwanda
kama hicho kupata soko la uhakika.
“Kiwanda hicho kimepata soko katika
Jumuiya ya Ulaya ya kupeleka mafuta yaliyosafishwa mara mbili (Double
Refined).”
“Tuna uwezo wa kuilisha
nchi yetu na mafuta tunayozalisha wenyewe na kuuza mengine nje” alisema Profesa
Mkenda na kuongeza kuwa kwa bahati mbaya Wakulima wadogo bado wanahangaika
katika uzalishaji.
“Wataalam wanasema kama Wakulima
wakibadilika na kufanya kilimo biashara chenye matumizi ya zana za kisasa na
mbegu bora za kisasa wataweza kuzalisha tani 10 za alizeti kwa hekta.”
“Wakulima nchini wanazalisha
chini ya tani moja kwa hekta.” Amekaririwa Waziri Mkenda.
Mkurugenzi Mtendaji kiwanda
cha Pyxus Agriculture Tanzania Bwana Malcolm McGrath alisema kiwanda chake kwa
sasa kinazalisha tani elfu ishirini (20,000) kwa mwaka lakini kina uwezo
wa kuzalisha mara sita zaidi ya hapo.
Mkurugenzi huyo amesema tayari
wamekuwa na mawasiliano na Wakulima wadogo, wa kati na Wakubwa wa alizeti
kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro, Manyara, Singida, Tabora na Kigoma
lakini kuna changamoto kubwa ya ughali wa mali ghafi hivyo kufanya bidhaa
yao kuwa ghali ukilinganisha na nchi nyingine zinazopeleka mafuta katika
soko la Ulaya.
Bwana McGrath ameiomba Serikali
kuwezesha kilimo cha mkataba ili wawe na uhakika wa mali ghafi na pia kusiwepo
na uchelewefu wa usafirishaji wa bidhaa hiyo bandarini.
“Tunakabiliwa na changamoto
za kuchelewa kwa makontena yetu bandarini. Pia bila sababu yoyote ile mamlaka
za Manyara zimesitisha mpango wetu wa kufanyakazi na wakulima na hivyo hali
hiyo itatuathiri kwa asilimia 25 ya malengo yetu,” alisema Mkurugenzi huyo.
Mwenyekiiti wa Shirikisho la
Wachakataji Alizeti mkoa wa Dodoma Bwana Ringo Iringo amesema pia kuna
changamoto katika masuala ya tozo mbalimbali na kodi ya ongezeko la thamani kwa
teknolojia inayoingizwa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo
ya Mazao; Wizara ya Kilimo Bwana Enorck Nyasebwa amesema timu ya Wataalamu
itakutana kutafuta suluhisho la kuongeza uzalishaji nchini. Alisema kuna
ongezeko kubwa la mahitaji ya mafuta ya alizeti yanayozalishwa nchini katika
soko la India na Afrika Kusini.
Mwenyekiti wa Baraza la
Kilimo la Taifa; Bwana Timoth Mmbaga amesema uhaba wa mafuta ya kula uwe ni
onyo kwa nchi.
"Uhaba wa mafuta ya kula
ni fursa pia ni onyo; Hivi Malaysia angekataa kutupa mafuta tungefanyaje? Ili
ni onyo lazima tujitegemee na sasa tunajitosheleza kwa asilimia 43 tu. Jitihada
zifanyike ili hii asilimia hiyo isirudi nyuma tena.” Amesisitiza Bwana Mbaga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...