WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda ahakikishe anawakamata viongozi wa AMCOS kwa tuhuma za kutoa fedha za wanachama na kuwapa madiwani ili wakawashawishi madiwani wenzao wakubali kubadilisha eneo la ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Madiwani waliohusika katika mvutano huo ni wa kata za Mkumbi (Bruno
Kapinga,) kata ya Lukalasi (Bosco Ndimbo) na wa kata ya Linda (Haule,)
ambao wanadaiwa kuchukua fedha kutoka kwa watendaji wa AMCOS kwa ajili
ya kwenda kushawishi madiwani wenzao wakubali kuhamishwa kwa eneo la
ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Januari 4, 2021) baada ya kuzindua
jengo la utawala la Halmashauri ya Mji wa Mbinga akiwa wilayani Mbinga
mkoa wa Ruvuma. Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,
Christine Mndeme asimamie ujenzi wa halmashauri hiyo unaoendelea
katika eneo la Kigonsera.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa mvutano wa Madiwani wa
Halmashauri ya Mbinga Vijijini ambao baadhi yao hawataki makao makuu
ya halmashauri hiyo yajengwe Kigonsera na kuamua kuendesha mchakato wa
kushawishi wengine wagomee mradi huo jambo ambalo linakwamisha
maendeleo kwa sababu tayari mradi huo umeshaanza kujengwa.

Mvutano huo unaongozwa na Madiwani hao wa Kata tatu za Mkumbi,
Lukalasi na Linda ambao wanataka makao makuu yajengwe kwenye kata ya
Mkumbi katika eneo ambalo litailazimu Serikali ilipe fidia ya zaidi ya
shilingi milioni 400 huku kukiwa na eneo la bure la ekari 150 ambalo
ndiko yanakojengwa makao makuu.

“Hatuwezi kukubali huko mnakotaka nyie ni lazima tulipe fidia ya zaidi
ya shilingi milioni 400 na kuna eneo la bure ekari zaidi ya 150, hii
haikubaliki hatuwezi kufanya mambo kama haya kwenye fedha za wananchi
haiwezekani. Mmeamua kila AMCOS ichange shilingi 600,000 mpate milioni
tatu mfanye kampeni ya kutaka halmashauri ijengwe kwenye eneo lao hiyo
ni rushwa.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Kwa kuwa zile ni fedha za wakulima,
Kamanda wa TAKUKURU kawakamate watendaji wa AMCOS hizo wahojiwe kwa nini walitumia fedha za kuwapa Madiwani wakahonge ni lazima wahojiwe waeleze ni nani aliyetoa maagizo ya kutoa shilingi milioni tatu.
Hatuwezi kutumia fedha za wananchi kwa ajili ya kuhonga watu lazima
fedha hizo za wakulima zirudishwe ni mali ya wakulima.”

Mapema, Waziri Mkuu alizindua jengo la utawala la Halmashauri ya Mji
wa Mbinga na kukagua ujenzi wa nyumba nane za watumishi wa halmashauri
hiyo na amesema kwamba ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo
iliyogharimu shilingi bilioni 3.7.

Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Grace Quintine kwa usimamizi mzuri wa
miradi hiyo ambayo imejengwa kwa viwango bora na majengo hayo
yanalingana na kiwango cha fedha kilichotolewa.

“Tulimletea shilingi milioni 350 hapa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba
saba za watumishi na ametumia milioni 321 na tulimletea shilingi
milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi lakini
ametumia shilingi milioni 251 na hakuna ubabaishaji majengo yote
yamejengwa kwa viwango bora. Nampongeza sana Mkurugenzi huyu amefanya vizuri sana endelea kujenga miradi mingine ikiwemo na ya vyumba vya madarasa.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Grace
Quintine amesema halmashauri yao katika mwaka wa fedha 2019/2020
ilipekea shilingi milioni 650 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
watumishi zikiwemo saba za Wakuu wa Idara na moja ya Mkurugenzi.

Amesema gharama za ujenzi wa nyumba saba za Wakuu wa Idara ni shilingi
milioni 321.771 ambapo kila nyumba iligharimu shilingi milioni 45.967
kati ya shilingi milioni 50 zilizoidhinishwa za kupokelewa ambapo kila
nyumba ilikadiriwa kutumia shilingi milioni 350 kwa nyumba zote.

“Ujenzi wa nyumba ya ghorofa moja ya Mkurugenzi wa Mji umegharimu
shilingi milioni 251.780 kuhu makadirio yakiwa ni shilingi milioni
300. Lengo la miradi hii ni kuboresha mazingira ya makazi ya watumishi
wa halmashauri ikiwa ni pamoja na kupunguza kilipa posho za nyumba kwa
kila mwezi.”

Amesema shilingi milioni 28.228 zilizobaki katika ujenzi wa nyumba za
Wakuu wa Idara zitatumika kujenga mnara wa tenki la maji na uwekaji wa
tenki moja la maji kwa kila nyumba na kuanza ujenzi wa uzio kuzunguka
nyumba zote saba.

Mkurugenzi huyo amesema mbali na utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo
ya nyumba za makazi, pia Serikali ilitoa shilingi bilioni 3.1 kwa
ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo ambalo
lilijengwa na kampuni ya SUMA-JKT Kanda ya Mtwara.

Amesema ujenzi wa jengo hilo la utawala lenye jumla ya vyumba 52
vikiwemo vyumba vya ofisi za watumishi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Mji, ukumbi mkubwa wa mikutano na ukumbi mdogo kwa ajili ya vikao vya
Wakuu wa Idara na Vitengo. “Ujenzi umekalika na lilianza kutumika
Januari 2020. Naishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi hii.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...