Kamishna Msaidizi Mwandamizi-Ukaguzi wa ndani Christopher Mtibili akifafanua jambo mbele ya wahariri wa Vyombo vya habari nchini (hawapo pichani), waliofika katika makao makuu ya shirika hilo yaliyopo jijini Arusha,Pichani kulia ni Naibu Kamishna Msaidizi Huduma za Shirika-TANAPA, Juma Kuji na kushoto ni Afisa Mwandamizi Uhifadhi (TEHAMA) Bw.Boniface Mariki


===== ======= ========
Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) limesema kuwa Mfumo mpya wa Ukusanyaji Mapato kwa njia ya Kieletroniki maarufu kama (GePG) Umeongeza uwajibikaji na uwazi katika ukusanyaji mapato pamoja na kuongeza mapato kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza na wahariri wa Vyombo vya habari nchini waliofika Makao Makuu ya Shirika hilo yaliyopo jijini Arusha,Naibu Kamishna Msaidizi Huduma za Shirika Juma Kuji alisema kuwa Mfumo wa GePG umeleta manufaa makubwa pamoja na kuboresha muda wa kuhudumia wateja.
Naibu Kamishna Kuji alisema kuwa kabla ya kuanza kutumia mfumo huo mapato ya shirika yalikuwa wastani wa kati ya sh. bilioni 100 na 200 hadi kufikia wastani wa sh. bilioni 364 kwa mwaka kabla ya ugonjwa wa korona kuzuka.
“Ndugu zangu wahariri mfumo huu wa GePG tulikuwa na akaunti kama 100 za kukusanya makusanyo kupitia hifadhi zetu zote 22 na hii ilikuwa inatupa kazi kubwa ya kufanya usuluhishi wa hesabu pamoja na kutumia gharama kubwa ya tozo za benki na tulikuwa tunatumia muda mrefu kukusanya taarifa na kuandaa ripoti hata kuzipata fedha zenyewe mara nyingi zilikuwa zikichelewa kuingia kwenye akaunti zetu kukosekana " alisema Afande Kuji
Pia alisema kuwa wingi wa akaunti za kuhifadhia fedha umepungua kutoka akaunti 100 hadi kubakia akaunti nane ambapo nne ni za kukusanya fedha za ndani na nne ni za makusanyo ya fedha za kigeni yaani dola.
“Tumepunguza utitiri wa Akaunti zetu kwasababu tuna mageti 22 nchi nzima, na tulikuwa tunaendesha akaunti 100, ilikuwa kazi kubwa kutengeneza taarifa zote hizi ni lazima uwatumie wahasibu kusimamia kila akaunti kila akaunti, kuna gharama kubwa zimepungua, hivyo basi tunaweza kuyaona makusanyo yote kwa muda mchache sana na kwa uwazi na hakuna gharama tunazotoa na ripoti zinapatikana mara moja”alisema Naibu Kamishna Kuji
Nae Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ukaguzi wa ndani Christopher Mtibili alisema kuwa kupitia mfumo wa GePG umewezesha kuongeza mapato kupitia makusanyo na kuchangia pato la Taifa pia.
Alisema kipindi cha nyuma kabla ya Mfumo huo walikuwa wakipata changamoto mbali mbali ambapo chaneli za malipo zilikuwa nyingi, tofauti na sasa ni ‘CONTROL NUMBER’ tu.
Hata hivyo Afisa Mwandamizi Uhifadhi (TEHAMA) Bw.Boniface Mariki alisema kuwa Mfumo huo umewawezesha waongoza watalii kuweza kuokoa muda na kuwawezesha kulipa kabla ya kupata huduma na hata kama kuna makosa ya kiufundi basi kupitia mfumo huo yanaweza kurekebishika.
“Wafanyabiashara wengine walikuwa wanataka huduma kwanza kisha kulipa baadae, lakini kutokana na Mfumo huu huwezi kupata huduma yeyote bila kulipia utalipa kwanza ndio upate huduma maana hakuna mazungumzo hivyo hasara hakuna kabisa, hata mtu akilipa zaidi ya mara moja kupitia mfumo huu unaweza kuona kila kitu na ukaweza kumsaidia”Alisema Afisa Mariki
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lilianza kutumia mfumo huu wa GePG tangu tarehe mosi September,2018.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...