Na Moshy Kiyungi, Tabora, Februari, 2021.

M’pongo Love alikuwa mwanamke mahiri kwa utunzi na uimbaji wa nyimbo za muziki wa dansi mwenye haiba ya pekee na alipata umaarufu mkubwa nchini kwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alizaliwa Agosti 27, 1956 katika kitongoji cha Boma nje kidogo ya jiji  la Kinshasa, nchini Kongo Belgium wakati huo. Baba yake alikuwa kiongozi wa Jeshi wakati mama alikuwa Mkuu wa Chuo cha Elimu cha Wasichana, ambao walimpa majina ya Alfride Mpongo Landu maarufu kama  Mpongo Love.

, mwaka 1960 M’pongo akiwa bado mdogo wa miaka minne, alidungwa kimakosa sindano ya Penicillin kwa ajili ya chanjo ya polio, iliyomsababishia ulemavu wa mguu wake mmoja.

Mwaka 1962 baada ya kupatiwa tiba ya uhakika Mpongo Love akaanza kutembea, japokuwa ulemavu wake ulionekana wakati akitembea ambaye kabla hajawa mwanamuziki, alikuwa Katibu Mtendaji kwenye kampuni ya Districas, iliokuwa ikijishughulisha na maswala ya uuzaji wa magari.

Alianza kujihusisha na masuala ya muziki akiwa mwimbaji wa kwaya ya shuleni kwao ambako kipaji chake katika uimbaji kilijitokeza kabla ya kuhamia katika jiji la Kinshasa wakati akiwa na umri wa miaka 18, ambako akawa anashughulika na uimbaji .

 

Akiwa na umri wa miaka 19 kwa msaada wa Empompo Loway akaunda kundi lake mwenyewe akalipa jina la Tcheke Tcheke Love, ambapo alifanya vyema katika tasnia hiyo ya muziki kwa msaada kutoka bendi ya OK. Jazz ikiongozwa na Franco Makiadi, akasaidiwa pia na mpuliza saksafoni wa bendi hiyo, Empopo Loway ambaye ndiye aliyempangia muziki wake pamoja na kumtafutia mdhamini mwenye uwezo wa kugharamia shughuli zake za muziki.

Mpongo mwaka 1976 alitokeza kwenye luninga akifanya tamasha na kuachia rekodi zake za mwanzo baada ya kuwezeshwa na Empopo Loway pamoja na bendi kadhaa za jijini Kinshasa.

Nyimbo zake zimejikita katika mtindo wa rumba la Kikongo zilishamiri haraka sana kama wimbo wa Ndaya, uliompatia sifa kibao unaohadithia kisa cha mwanamke aliyeolewa ambaye anamuenzi mumewe vizuri.

Mwaka huohuo aliachia kibao kingine chenye jina la Paspossible Maty, kikisimulia hatari ya kujiegemeza kwenye mapenzi wakati unahitajika uwe unafanya kazi, kilichopokewa vizuri sana, ndipo watu wakagundua, uimbaji wa binti huyo mzuri, mrembo mwenye sauti nyororo, ingawa ni mlemavu.

Wakati uchumi wa nchi ya Kongo ukitetereka, Mpongo Love alijaribu bahati yake akaenda Paris nchini Ufaransa ambako alitiliana mkataba na Safari Ambiance akarekodi album yake ya kwanza La Voix du Zaire ya mwaka 1979, iliyopata mafanikio ya wastani.

Baada ya kutengana Empopo  Loway, Mpongo Love alirudi Paris Studio mwaka 1981 akarekodi album ya Famme Commercante..Mfanyabiashara mwanamke.., ikiwa ni kazi yake iliyokuwa bora sana yenye nyimbo sita, ambayo ilipangiliwa na Mkongo toka Brazzaville, Sammy Massamba.

Iliyofuatia ni album ya Basongeur ..watendaji.. ya mwaka 1983, nayo ilipokewa vizuri sana.

Baada ya kurekodi album ya Basongeur Mpongo alijaribu kuvunja mkataba na Safari Ambiance, Nembo hiyo ikamfungulia mashataka ambayo yalisababisha kuzuiwa kurekodi Paris kwa miaka kadhaa.

Aidha alikwenda nchini Gabon ambako alirekodi album na mwanamuziki ambaye pia ni mwanasiasa, Mgabon Alexandre Sambat ambayo haikuwa na mafanikio mazuri.

Mkongwe huyo alianya mlolongo wa ziara na matamasha kadhaa hususan katika nchi za Afrika Magharibi ambako aliweza kupandisha shughuli zake za muziki kuwa hai.

Mpongo Love alirekodi albuma yake ya mwisho ya Parteger huko Paris mwaka 1989 baada ya maamuzi ya kesi yake na Safari Ambiance kumalizika.

Akiwa ni mtunzi na mwimbaji bora wa kiwango cha juu, hakuweza kutimiza ahadi wakati wa mwanzoni mwa shughuli zake Kazi zake na Empopo Loway na baadaye Safari Ambiance, ziliweza kuweka misingi ya mafanikio yake ya muda mrefu, lakini kuvunja na kukatisha mkataba na nembo hiyo, kulisabaisha kuanguka kwake ambako hakuweza kurudi tena katika chati.

Alifanikiwa kutengeneza takriban albums za L’Afrique danse avec ya mwaka 1977,  Safari Sound SAS 036 ya mwaka 1982, Safari Sound – SAS 047 ya 1983, Mokili Compliqué ya mwaka 1985,  Une Seule Femme ya mwaka 1986, Gina ya1986, Exclusivité Ya L’Amour ya mwaka1987 na Partager mwaka 1987.

Mpongo Love alifariki dunia Januari 15, 1990 jijini Kinshasa baada kuugua ugonjwa ambao haukujulikana, akawaacha ukiwani watoto wake watatu Sandra M'pongo Ndo, Ritchy Pongo Landu na Grâce Pongo Otina.

Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, Amina.

 

Mwisho.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandishi wa makala haya napatikana kwa namba: 0784331200, 0736331200, 0713331200 na 0767331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...