*Nchi 16 kushiriki, Watanzania washauriwa kutumia fursa
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
KATIKA kuhakikisha falsafa ya KAIZEN inatekelezwa katika sekta mbalimbali nchini hasa viwanda katika kuleta tija na maendeleo ya Taifa, Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya siku ya KAIZEN Afrika yatakayofanyika mwezi Juni mwaka huu na kuhudhuria na nchi 16 za Afrika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya pili ya KAIZEN Tanzania yaliyoambatana na utoaji tuzo kwa viwanda vikubwa na vidogo vinavyofanya kazi kwa kuzingatia falsafa ya KAIZEN, Katibu mkuu wa Wizara ya viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe amesema, Serikali imekuwa ikitenga fedha za kuendeleza miradi inayotekelezwa kupitia falsafa ya KAIZEN kwa kushirikiana na Serikali ya Japan ambao ni wafadhili wa KAIZEN katika kuendeleza viwanda.
"Wizara ya viwanda na biashara imekuwa ikisimamia maendeleo ya biashara, viwanda vikubwa na vidogo pamoja na sera rafiki zinazoendana na wakati na tupo katika mchakato wa kuweka sera mpya na za kitaifa katika masuala ya kumlinda mlaji, haki miliki na ubora wa bidhaa ambao utaleta ushindani katika soko la kidunia." Amesema Shemdoe.
Pia amewataka washiriki wa mkutano huo kuwa mabalozi bora wa falsafa ya KAIZEN katika utendaji kazi pamoja na kutumia fursa za ujio wa mataifa kumi na sita nchini.
"Hii ni fursa kwetu watanzania katika kuhakikisha tunakuza viwanda na biashara zetu, wakifika wageni tuwatembeze katika vivutio vyetu vya utalii, tuwaoneshe bidhaa za viwanda vyetu pamoja na kubadilishana uzoefu wa masoko." Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi idara ya maendeleo ya viwanda kutoka wizara ya viwanda na biashara Ramson Mwilangali amesema, maadhimisho ya pili ya KAIZEN nchini yamelenga kubadilishana uzoefu, fursa na kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuelekea maadhimisho ya KAIZEN Afrika yatakayofanyika nchini.
Mwilangali amesema Licha ya falsafa ya KAIZEN kuwa ngeni miongoni mwa umma wa watanzania elimu bado inaendealea kutolewa zaidi kwa sekta mbalimbali.
Vilevile kaimu Balozi wa Japan nchini Nirinuma Takashi amesema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha miradi mingi zaidi ya kujenga Taifa inatekelezwa Tanzania.
Ameeleza kuwa uendelezaji wa viwanda vidogo ni muhimu katika kujenga uchumi wa nchi na kuwataka washiriki na washindi wa Tuzo za KAIZEN kuwa mabalozi katika kutangaza falsafa hiyo katika maeneo yao ya kazi.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na utolewaji wa vyeti kwa viwanda 18 vilivyoshiriki pamoja na zawadi kwa viwanda vilivyofanya vizuri zaidi kwa kuzingatia falsafa ya KAIZEN ambavyo ni pamoja na Quality Form (Dar es Salaam,) New Kingdom (Mbeya,) Kioo Limited, Super Doll na Maswa Nutrition kutoka Simiyu.
KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana ya 'badilika' kwa ubora/uzuri na hutumika katika biashara, KAIZEN huusu shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi, mfumo, michakato na nyanja zote za kuendesha biashara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...