Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mwanza , Mhe. Mary Masanja (katikati) akizungumza na Viongozi  wa Bodi ya Barabara ya Mkoa leo jijini Mwanza. Pamoja na mambo mengine  amewataka viongozi hao watembelee  Vivutio vya Utalii vilivyopo katika maeneo yao na kushiriki pia kuhamasisha  Utalii wa ndani  ili kuongeza Pato la Taifa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mwanza, Mhe. Mary Masanja (kushoto) akiteta jambo na Kaimu Mwenyekiti wa Kikao cha Pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Bw. Emmanuel Kipole wakati wa Kikao cha Bodi hiyo kilichofanyika Jijini Mwanza.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mary Masanja (Wapili Kulia)  akipitia baadhi ya Nyaraka za Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza akiwa pamoja na viongozi Mbalimbali wa mkoa wa Mwanza wakati wa Kikao cha Pili cha Bodi ya barabara ya Mkoa huo kwa mwaka 2020/2021 Jijini Mwanza.
*****************************************

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja amesisitiza kuwa fursa zilizoko kwenye Sekta ya Maliasili na Utalii  zikitumika ipasavyo zitasaidia kukuza  Pato la Taifa na uchumi wa  mtu mmoja mmoja.

Mhe. Mary Masanja ametoa Kauli hiyo  leo jijini Mwanza  wakati wa  kikao cha pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa Mwaka 2020/2021. Amesema takwimu za watalii wanaoingia hapa nchini kuanzia mwaka 1993 walikuwa  230,000. Aidha,  mwaka 2019 idadi  hiyo ya watalii iliongezeka na kufikia milioni 1.5.

‘’Idadi ya Watanzania kwa sasa ni milioni 60, lakini ukingalia takwimu hizo watalii wanaoingia kwenye hifadhi zetu kuangalia vivutio ni milioni 1.5,  hii inaonesha sisi Watanzania tuna kazi kubwa ya kufanya, kuwa wazalendo na kupenda vile tulivyo navyo ‘’ amesema Mhe. Masanja.

Katika hatua nyingine Mhe. Mary Masanja  amewaeleza viongozi wa mkoa huo  kuwa uwepo wa vivutio vingi vya Utalii katika Kanda ya ziwa ni fursa pekee ya wananchi kuendelea kunufaika akitoa wito kwa viongozi waliohudhuria mkutano huo  wahamasishe Utalii wa ndani kwa nguvu zote.  “Ni lazima tuongeze nguvu katika  kuhamasisha utalii  wa ndani bila kusahau kuhamasisha wageni kutoka nje ya nchi yetu , Utalii wa ndani unatuhusu sisi wenyewe ,nikiuliza hapa wangapi wamefika kwenye hifadhi zetu na kwenye vivutio  mbalimbali tulivyonavyo tutabaini  idadi kidogo sana, nawaomba sana tuhamasishane ’ Amesisitiza Mhe. Mary Masanja.

Ameongeza kuwa Janga la Corona limesababisha  kuyumba kwa sekta Utalii duniani kote pia hapa nchini  kwa kuwa watalii  waliokua wakitegemewa nchi zao zimeathiriwa na Corona  hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa Balozi wa kutangaza Utalii na kutembelea vivutio vilivyopo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...