“Uwajibikaji
ni miongoni mwa alama kubwa ambayo inanifanya nimkumbuke Hayati
Magufuli,” amesema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa
Othman Masoud Othman, leo hii Jumamosi (Machi 20), wakati wa mazungumzo
yake na kituo cha televisheni cha ITV nyumbani kwake, Osterbay jijini
Dar es Salaam.
Mheshimiwa
Othman amesema Hayati Magufuli tangu akiwa naibu waziri, kisha waziri
na hatimae kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alibeba sifa
moja ya uwajibikaji.
”Uwajibikaji
ndio sifa ya uongozi na ndicho kipimo cha utumishi wa mtu, hasa
unapokuwa katika utumishi wa umma na hata taasisi binafsi, Na jambo hilo
Dk. Magufuli alikuwa nalo.” alisema Mheshimiwa Othman
Makamu
huyo wa kwanza wa rais wa Zanzibar ameongeza kwamba Hayati Magufuli
alipenda sana kuona mambo yanafanywa na kuenda kwa haraka na ufanisi
mkubwa. Akitoa mfano wa hayo, Mheshimiwa Othman amesema wapo watumishi
wa umma waliokuwa wanachelewesha sana utekelezaji wa majukumu, “lakini
kipindi cha awamu yake aliweza kwa kiasi kikubwa kuleta heshima hasa ya
utumishi wa umma.”
Aidha,
Mheshimiwa Othman amesema Hayati Magufuli alikuwa na maono ya ukombozi
wa rasilimali za taifa. “Katika hili, wote ni mashahidi namna ubadhirifu
uliokuwa unafanyika katika sekta ya madini na watu wachache walivyokuwa
wakitumia rasilimali hizo kwa maslahi yao binafsi badala ya manufaa ya
taifa.”
“Mimi sikuwa
mwanasiasa hasa, bali nilikuwa mwangalizi wa siasa. Katika eneo hili,
Dk. Magufuli aliweza pia kutumia nafasi yake ya kisiasa hata
kuibadilisha taswira ya chama chake kwa kufichuwa ufisadi mkubwa
uliokuwa ndani yake,’’ alisema Mheshimiwa Othman.
Kuhusiana
na Tanzania ya baada ya Hayati Magufuli, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar amempongeza Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuchukuwa rasmi
nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akisema kuwa
ana imani sana na utendaji wake, kwani ni kiongozi ambaye tayari ana
uzoefu wa uongozi kupitia ngazi mbalimbali mpaka kufikia sasa.
Mheshimiwa
Othman amesema, itapendeza sana kuona mashirikiano na mahusiano mema ya
vyama vya siasa kwa sasa na kwamba hii ni fursa kwa waliopo kuhakikisha
wanatengeneza namna za kuondoa tofauti na kuleta umoja wa Watanzania.
“Napenda
kuliona taifa linaungana na kuleta mafanikio,” alisema Makamu huyo wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye tangu jana amekuwa akiungana na
viongozi wengine wa serikali waliopo jijini Dar es Salaam kwenye
shughuli zinazohusika na msiba wa Hayati John Magufuli.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...