Na Mwandishi Maalum,Nyasa
NAIBU Waziri wa maji Maryprisca Mahundi, amepokelewa na ndoo tupu za
maji na wanawake wa kijiji cha Likwilo kata ya Kilosa wilayani Nyasa
kutokana na kijiji hicho kutokuwa na huduma ya maji safi na salama kwa
muda mrefu.
Naibu Waziri Mahundi, alikutana na hali hiyo jana wakati akiwa katika
ziara yake ya siku mbili wilayani humo kukagua miradi ya maji
inayotekelezwa na wizara ya maji kupitia wakala wa maji vijijini
Ruwasa.
Kijiji cha Likwilo ni miongoni mwa vijiji katika 84 wilaya ya Nyasa,
ambavyo tangu Uhuru mwaka 1961 havijawahi kupata maji ya bomba, badala
yake wananchi wanalazimika kutumia maji ya visima vya asili na wengine
kutumia maji ya ziwa Nyasa kwa matumizi ya kila siku.
Akiongea na wananchi hao,Naibu Waziri amewaomba kuwa wavumilivu wakati
huu ambapo Serikali kupitia wizara ya maji imejipanga kuhakikisha
inamaliza changamoto ya maji katika kijiji hicho na maeneo mengine ya
wilaya ya Nyasa.
Alisema,wizara ya maji itatoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya
kuboresha huduma ya maji katika mji mdogo wa Mbambabay makao makuu ya
wilaya ya Nyasa ili kupunguza kero kubwa ya maji.
Amewaondoa wasiwasi wananchi hao juu ya fedha hizo na kusisitiza
kuwa,zitaletwa ndani ya wiki moja kuanzia sasa ili kuanza utekelezaji wa
miradi ya maji.
Aidha alisema,serikali itachimba visima viwili vya maji ili kukabiliana
na changamoto ya huduma ya maji safi na salama,wakati ikusubiri mpango
wake wa kutekeleza mradi mkubwa utakaotumia maji ya ziwa nyasa
kusambaza maji katika maeneo mbalimbali katika wilaya ya Nyasa.
Katika hatua nyingine,Naibu Waziri amewashukuru wananchi wa kijiji hicho
na kata ya Kilosa kwa kuonesha imani kubwa na Chama cha Mapinduzi kwa
kuwachagua wagombea wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na
kuwaomba kuendelea kuwa na imani na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Kwa mujibu wake,wananchi wa jimbo la Nyasa hawakufanya makosa kumchagua
Stella Manyanya kuwa Mbunge wa jimbo hilo, kwani ni mtu makini anayejua
majukumu yake na kiongozi anayefanya kazi nzuri ya kuwatumikia
wananchi.
Akizungumza kwa niba ya wananchi Mbunge wa jimbo la Nyasa Stella
Manyanya alisema, jimbo la Nyasa ni kati ya maeneo yenye vyanzo vingi
vya maji hapa nchini,lakini jambo la kusikitisha kuna kero kubwa ya maji
safi na salama.
Hivyo,ameiomba wizara ya maji kuhakikisha ina maliza changamoto ya maji
ili wananchi wapate nafasi ya kufanya shughuli zao za maendeleo badala
ya kuendelea kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji jambo
lililochangia sana kurudisha maendeleo yao.
Alisema, katika vijiji 84 alivyotembelea wakati wa kampeni za uchaguzi
Mkuu mwaka jana, wananchi walimueleza kero kubwa ya maji maji safi na
salama.
Ameiomba wizara ya maji kuwa na huruma na wananchi wa jimbo hilo ambao
kwa muda mrefu wako katika mateso makubwa ya kukosa maji safi na salama
kwani licha ya Serikali kwa nyakati tofauti kuanza kujenga miradi ya
maji,bado changamoto ya maji kwa wananchi wa Nyasa ni kubwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Nyasa Fidelis Duwe
alisema,kuna malalamiko makubwa ya wananchi kuhusina na ukosefu wa maji
safi na salama kwani kati ya vijiji 84 vilivyofikiwa na maji ya
bomba,vilivyofikiwa na huduma hiyo havizidi 10 na kila wanapokwenda
kilio kikubwa cha wananchi ni kero ya maji.
Katika hatua nyingine,SERIKALI imetumia jumla ya shilingi milioni
390,870.000 kutekeleza mradi wa maji katika kijiji cha Chimate wilaya ya
Nyasa ambao umeanza kuwanufaisha zaidi ya wakazi 2,798 wa kijiji hicho.
Meneja wa wakala wa usambazaji maji vijijini Ruwasa wilaya ya Nyasa
Evaristo Ngole alisema hayo jana kwa naibu Waziri wa maji MaryPrisca
Mahundi aliyetembelea mradi huo uliotekelezwa kwa fedha za malipo kwa
matokeo(P4R) kwa kutumia mafundi wadogo.
Ngole alisema, maandalizi ya mradi wa maji Chimate ulianza mwezi Juni
2020 kwa kutayarisha vifaa vya ujenzi na kazi rasmi ya ujenzi ilianza
Julai.
Ngole alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi
wa chanzo cha maji,ujenzi wa tenki la mita za ujazo 75,kujenga vituo 15
vya kuchotea maji na ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji
urefu wa km15.50.
Alisema, hadi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 85 na fedha
zilizotumika ni shilingi milioni 356,112,310 kwa kujenga chanzo,kujenga
tenki,vituo 18 vya kuchotea maji, na kujenga mtandao wa mabomba ya
kusambaza maji na wanategemea kukamilisha ujenzi wa mradi huo ifikapo
mwezi Mei.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa maji MaryPrisca Mahundi ameipongeza
Ruwasa kwa kazi nzuri ya kutekeleza mradi huo na kuwataka wanufaika wa
mradi kuwa walinzi wa miundombinu ili uweze kudumu kwa muda mrefu.
Alisema, wizara ya maji itaendelea kutekeleza miradi ya maji katika
vijiji na maeneo mbalimbali kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani na
kumaliza kero ya maji ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya
wananchi kushindwa kufanya kazi za maendeleo.
Hata hivyo,akiongea kwa niaba ya wenzake mkazi wa kijiji hicho Andrew
Mwarabu ameiomba Ruwasa kuongeza idadi ya vituo Vya kuchotea maji kutoka
18 vya sasa hadi kufikiwa 23 kutokana na idadi kubwa ya watu katika
kijiji hicho.
Ameishukuru wizara ya maji kutekeeza mradi huo, kwani umemaliza kero ya
maji iliyokuwepo na kuhaidi kutunza mradi kwa manufaa yao.
Picha,Baadhi ya wanawake wa kijiji cha Likwilo kata ya Kilosa wilayani
Nyasa wakimuonesha ndoo tupu za maji Naibu waziri wa maji Mhandisi
MaryPrisca Mahundi aliyevaa koti jeupe kama ishara ya uhaba wa huduma ya
maji safi na salama katika kijiji hicho,wakati wa ziara yake ya siku
mbili wilayani humo kukagua utekelezaji wa miradi ya maji,kushoto kwa Nnaibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Nyasa Esabela Chilumba.
Picha na Muhidin Amri
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...