Na Amiri Kilagalila,Njombe
Serikali
kupitia wizara ya kilimo kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau
wengine wapo katika mchakato wa kuanzisha mnada wa chai hapa nchini
unaotarajia kuwepo jijini Dar es salaam.
Kauli
hiyo imetolewa na ofisa kutoka wizara ya kilimo idara ya maendeleo ya
mazao na masoko ya kilimo Fikiri Katiko kwenye kikao kilichokutanisha
wadau mbalimbali wa zao la chai hapa nchini kilichoandaliwa na
kuratibiwa na mradi wa Markup kilichofanyika hapa mkoani Njombe.
Alisema
lengo la kuanzisha mnada huo ni kupunguza gharama za kusafirisha chai
kutoka hapa nchini na kupeleka Kenya ambapo kwasasa mnada wa zao
hilo.hufanyika.
Alisema
endapo mnada utakuwepo hapa nchini utasaidia kupunguza gharama na pia
kusaidia wakulima wa chai kupata bei nzuri ya kuuza zao hilo.
Alisema
kwa kuwa serikali inatarajia pia kutumia maabara ya hapa nchini hivyo
wataweza kuhakiki ubora wa zao hilo la chai itakayouzwa katika mnada huo
tofauti na sasa ambapo maabara inayotumika ni ya huko nje ya nchi.
"Tumekuwa
tukipeleka asilimia 80 ya chai yetu nje ya nchi lakini sehemu kubwa ya
majani ya chai makavu huwa yanauzwa kupitia mnada wa Mombasa sasa
serikali kwa kuona hilo lipo katika mchakato wa kuanzisha mnada wa chai
nchini" Alisema Fikiri.
Mratibu
wa mradi wa Markup Tanzania Safari Fungo lengo la kikao hicho cha wadau
wa chai kusaidia wakulima na wafanyabiashara kuongeza thamani ya zao
hilo na baadae waweze kupata masoko.
Alisema
chai ni kinywaji cha pili ulimwenguni kinachonyweka zaidi baada ya maji
hivyo ni lazima wazalishaji wa zao hilo wapatiwe mbinu na kujengewa
uwezo kuanzia katika kuvuna, kuongeza thamani hadi namna ya kupata
masoko.
"Shughuli hii
imegawanyika katika maeneo makuu mawili, kwanza sehemu ya nadharia
ambapo wakulima na wafanyabiashara watapata nafasi ya kujengewa uwezo
darasani na baada ya hapo tutaenda shambani wakaone namna yale mafunzo
waliyoyapata wanaweza kubadilisha kwa vitendo" alisema Safari.
Meneja
mkuu wa kiwanda cha chai Ikanga Gerald Ngenzi alisema sekta chai nchini
inapitia wakati mgumu tofauti na miaka mitano iliyopita changamoto
kubwa ikiwa kwenye suala la bei.
Alisema
zao la chai kama ilivyo kwa mazao mengine ni lazima liweze kushindana
kimataifa lakini ili lifanikiwe katika ushindani huo lazima zao hilo
liwe na ubora.
"Kupitia
Markup wataalam mbalimbali wanafundishwa, kuwezeshwa ili kuhakikisha
wanarudi shambani kutekeleza mafunzo waliyoyapata ili mkulima azalishe
chai iliyo bora" alisema Gerald.
Baadhi
ya wakulima walioshiriki kikao hicho cha wadau wa chai akiwemo Kennedy
Peter kutoka wilaya ya Tarime mkoani Mara alisema kuanzishwa kwa soko la
mnada wa chai hapa nchi utawawezesha wakulima kupata bei nzuri
itakayosaidia kuboresha maisha yao.
Alisema
vile vile kupitia mnada huo utakaokuwa hapa nchini taifa litanufaika
kwa kupata fedha za kigeni ambazo zitasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.
"Vijana
wengi hawajikiti katika zao hili kwasababu ya ugumu wake kwenye bei
pamoja na masoko hivyo serikali inapaswa kuweka viwanda ili kuinua
thamani ya zao.la chai" alisema Kenedy.
Mmoja wa wataalamu akiandika jambo wakati wa kikao cha wadau wa zao la
chai kilichoandaliwa na mradi wa Markup Tanzania ili kukuza zao la chai
nchini.
Ofisa kutoka wizara ya kilimo idara ya maendeleo ya
mazao na masoko ya kilimo Fikiri Katiko akizungumza mara baada ya kikao
kilichokutanisha wadau mbalimbali wa zao la chai hapa nchini
kilichoandaliwa na kuratibiwa na mradi wa Markup kilichofanyika hapa
mkoani Njombe.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...