Na Amiri Kilagalila, Njombe


Halmashauri ya Mji Njombe imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni mia mbili thelathini na tisa  laki tisa na themanini elfu kwa vikundi 24, vikundi 08 vikiwa ni kwa   vijana na vikundi 16 vya wanawake hii ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali  ambapo Halmashauri imeweza kutenga asilimia kumi za mapato yake ya ndani kwa ajili ya zoezi hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya hundi ya mfano Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Romanus Mayemba ameipongeza Halmashauri kwa jinsi ambavyo imeweza kufanya usimamizi na kuhakikisha kwamba maagizo ya Serikali ya utoaji mikopo bila riba yanatekelezwa katika kila robo na kuwafikia walengwa kwa wakati.

“Niwapongeze wale wote mliobahatika kupata mikopo.Fedha za mikopo zinazotolewa zinajumuisha asilimia kumi ya mapato ya ndani pamoja na marejesho. Unaporejesha mikopo unatoa fursa kwa vikundi vingine vyenye sifa kuweza kukopa lakini pia unajijengea sifa ya kukopeshwa kwa mara nyingine. Tuzingatie urejeshaji wa mikopo kwa wakati. Tunapokwenda kutumia mikopo tuwe na uhakika wa kuirejesha na hii itatusaidia kusukuma maendeleo kwenye Halmashauri yetu. Uaminifu ni jambo la msingi sana. Alisema Mayemba

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi. Illuminatha Mwenda amesema kuwa Halmashauri imeweza kutoa mikopo mingi kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani jambo ambalo linapelekea ongezeko la utoaji mikopo kila wakati na hivyo amewataka Wananchi kuhakikisha kuwa wanakuwa wachangiaji wazuri wa mapato na kuwa wasimamizi kwa kuhakikisha kuwa hakuna upotevu wa mapato kwani mafanikio hayo ni kutokana na makusanyo ya mapato ya ndani kuwa mazuri.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti baadhi ya  wawakilishi wa vikundi hivyo wameipongeza Halmashauri kwa jitihada hizo na wameahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufanya marejesho na kupata fursa ya kuweza kukopeshwa tena.

Kwa upande wake Donas Innocent Kayombo  mwakilishi kutoka kikundi cha Vijana Melinze  amesema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo vijana kwenye uundaji wa vikundi ni ukosefu wa shughuli ya pamoja jambo linalopelekea vijana wengi kushindwa kujiunga kutokana na kuwa kila kijana anakuwa na shughuli yake ya kujiongezea kipato na hivyo kuiomba Serikali kuweza kuboresha miongozi hiyo ili kasi ya ukopaji kwa vijana iwe kubwa.

“Tulikuwa tunasikia mitaani kuhusu mikopo. Tukaamua kuunda kikundi. Tuliomba milioni kumi na tumepata kadri tulivyoomba na tunakwenda kuinuka kiuchumi.”Alisema Kayombo

Naye Rehema Nyezi mwakilishi kutoka kikundi cha wanawake  amesema kuwa wanaishukuru Halmashauri kwani wameweza kupatiwa mkopo kadri walivyoomba na amesema kuwa lengo lao ni kwenda kuanzisha kilimo cha parachichi na kuendeleza mradi wa ufugaji kuku na wameahidi kwenda kufanyia kazi fedha hizo ili waweze kuzirejesha kwa wakati.

kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 Halmashauri imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya  shilingi  milioni mia tisa arobaini  laki nane na themanini  kwa vikundi 96 ambapo  72 vya wanawake 22 vijana na 2 walemavu ikiwa ni mapato ya ndani ya Halmashauri na fedha za marejesho. Rai imeendelea kutolewa kwa watu wenye ulemavu  kuchangamkia fursa ya ambapo kwa sasa kumekuwa na mabadiliko ya idadi ya wanaojiunga ambapo   hata mlemavu mmoja anaweza kuomba na kupatiwa mkopo.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...