Audax Bahweitima-Naibu Kamishna wa NCAA anayesimamia Huduma za Shirika Akizungumza na Wadau wa Utalii (Picha na Jane Edward Michuzi TV, Arusha)
Jane Edward Michuzi TV, Arusha
Baadhi ya wadau wa utalii wamelalamikia baadhi ya changamoto zinazowakabili katika eneo la hifadhi ya ngorongoro na kuomba kupatiwa utatuzi wa haraka.
Akizungumza wakati wa kikao kazi na wadau wa utalii kilichoandaliwa na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, kamishina msaidizi wa huduma za shirika ,Audax Rwezaura amesema kuwa changamoto kubwa inayokuwa ikiwabili ni uwepo wa ugonjwa wa corona hivyo watajikita katika kusimamia huduma zote za kiutendaji ambazo zinakwamisha na nyingine kuziwakilisha ngazi za juu ili ziweze kutatuliwa.
Amesema kuwa wanajua hali itakuwa sawa kutokana na ugonjwa huo na kwamba vikao kazi vya namna hiyo vitasaidia kuona changamoto na fursa ili kuzifanyia Kazi na kuondoa changamoto zinazo lalamikiwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa madereva utalii, Paul Hilonga amesema kitendo cha ugawaji wa zawadi kwa wananchi waishio ndani ya hifadhi ni kizuri lakini kuna muda wageni hawafanyi hivyo hali inayosababisha hasira kwa wananchi waishio ndani ya hifadhi na kusababisha kupiga mawe magari hali inayowapelekea hasara kwao.
Ametanabaisha kuwa ni vyema wakaachana na ugawaji wa zawadi barabarani bali wakatoe katika maeneo maalumu kama shule ili kuepusha mtu kukaa barabarani kusubiria zawadi.
Baadhi ya Wadau wa utalii Khalifa Msangi, anasema kuwa ugonjwa wa korona umeyumbisha sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa hali inayofanya kushindwa kumudu gharama za Maisha, na kwamba Mkutano huo unaweza kuleta tija kama mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro itafanyia kazi changamoto zilizopo.
Ameishauri mamlaka hiyo kufanya mawasiliano na viongozi wa juu wa serikali,hasa katika kujenga miundombinu ya barabara,Tehama pamoja na kuweka njia bora ya kufanya malipo hasa kwa kuangalia hali ya kiuchumi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...