NAIBU Waziri wa Ujenzi na
Uchukuzi, Mwita Waitara, ametoa siku 14 kwa uongozi wa Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA), kumpa taarifa ya mradi wa upanuzi wa Bandari ya Tanga
unaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 500.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya
Naibu Waziri huyo kutoridhishwa na maelezo ya namna kiasi cha shilingi Bilioni
172 zilivyotumika katika ujenzi wa kuongeza kina katika bandari hiyo ili kuziwezesha
meli kubwa kutia nanga.
“Natoa siku 14 niwe nimepata
taarifa ya kina kuhusu mradi huu na namna ya mchakato wa kumpata mkandarasi
ulivyofanyika, nani alifanya upembuzi yakinifu, nani alishauri kutumiwa kwa
hizo fedha, nani walihusika katika usimamizi wa huo mradi na tathimini ya fedha
zilivyotumika ili kuiwezesha Serikali kuchukua hatua”, amesisitiza Naibu Waziri
Waitara.
Amesema nia ya Serikali ni
kuiona Bandari ya Tanga ikifanya kazi katika viwango vya juu na hivyo kuchangia
kukuza uchumi wa Taifa na yoyote atakayebainika kukwamisha dhamira hiyo ya
Serikali atachukuliwa hatua kali.
Amemtaka Mkurugenzi Mpya wa
TPA, kupanga safu yake ya uongozi mapema iwezekanavyo ili kuendana na kasi na
matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Amewataka watumishi wa Taasisi
zote zilizo chini ya Wizara yake kusoma mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2020 -
2025 ili kuweza kujua wanatakiwa wafanyeje na kwa namna gani katika kipindi
hicho.
“Fanyeni kazi kwa weledi, acheni
majivuno, hudumieni wananchi”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
TPA, Bw. Erick Hamis, amesisitiza kwamba taarifa zinazotakiwa zitawasilishwa
kwa wakati na miradi inayoendelea katika Bandari ya Tanga itakamilika katika
kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kuiwezesha Bandari hiyo kuhudumia tani
milioni mbili za shehena toka tani laki saba zinazohudumiwa kwa sasa.
“Tutahakikisha uwepo wa reli
na barabara za uhakika katika Mkoa wa Tanga kuelekea mikoa ya Kaskazini na
katikati ya nchi kunawezesha bandari hii kufanya kazi kwa ufanisi”, amesema Bw.
Hamis.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Waitara amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani (KM
50) kwa kiwango cha lami na kumtaka mkandarasi M/S China Henan International
kukamilisha barabara hiyo kwa wakati na Serikali haitakubali visingizio visivyo
na tija.
Naye, Meneja wa Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Tanga, Mhandisi Alfred Ndumbaro, amesema
Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hiyo
na zoezi la kulipa fidia litaanza Mei 03, mwaka huu.
Amemhakikishia Naibu Waziri
huyo kuwa atamsimamia kikamilifu mkandarasi ili kuhakikisha barabara hiyo
inajengwa kwa viwango na kukamilika kwa wakati na hivyo kufungua ukanda wa
Wilaya ya Pangani.
Naibu Waziri Waitara yupo
mkoani Tanga kuendelea na ziara yake ya siku nne ya kukagua miundombinu ya
Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi ambapo pamoja na mambo mengine amezungumza na watumishi ili kuwapa muelekeo
wa Serikali na kusikiliza hoja zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...