Na Amiri Kilagalila,Njombe
Wakulima
wa chai nchini wametakiwa kuboresha teknolojia ya uchumaji chai kutoka
kuchuma kwa mikono hadi kwa mashine na kupata chai iliyobora ili
kuendana na mahitaji ya soko la Dunia.
Hayo
yalisemwa na meneja mkuu wa kiwanda cha chai Kibena Mohamed Kasila
baada ya kutembelewa na wadau wa chai kutoka mikoa mitano ya hapa nchini
walioshiriki mafunzo kwa vitendo katika kiwanda hicho kilichopo mkoani
Njombe yaliyoandaliwa na mradi wa Mark Up unaofadhiliwa na umoja wa
ulaya.
Amesema duniani
kwasasa sekta ya chai imekumbwa na changamoto ya kuanguka kwa bei kwenye
soko la dunia hivyo njia pekee ya kuinasua sekta hiyo ya chai ni
kuhakikisha wanazalisha chai yenye ubora kwa kufuata kanuni bora za
kilimo, kanuni bora za uchakataji ili iweze kufika sokoni ikiwa na ubora
wa hali ya juu.
Amesema
kupitia mafunzo waliyoyapata mameneja wa mashamba, wakaguzi wa mashamba
ya chai na waliopo katika uchakataji utasaidia kupata chai yenye viwango
itakayouzwa kwa bei nzuri sokoni na kushindana na makampuni mengine
kutoka sehemu mbalimbali duniani yanayozalisha chai.
Ameiomba
Markup kusaidia mchakato wa kupata masoko nje ya nchi wakati serikali
ikiwa kwenye mchakato wa kuanzisha mnada wa chai hapa nchini.
"Katika
huo.mnada ili tufanye vizuri ubora wa chai inayozalishwa hapa nchini ni
kitu cha msingi tusipokuwa na chai bora mnada huo tutakaofungua
hautofanya vizuri" amesema Kasila.
Mratibu
wa mradi wa Markup Tanzania unaojishughulisha kusaidia wazalishaji na
wajasiriamali kuongeza thamani ya mazao yao na kupata masoko Safari
Fungo alisema kwa muda wa siku mbili wamekuwa na mafunzo ya nadharia
kwa wajasiriamali na wazalishaji ili kuwajengea uwezo na siku mbili
nyingine watakuwa kwenye mafunzo ya vitendo kwa kufika kwenye mashamba
ya chai na kuangalia vitu vya kuzingatia katika kuzalisha chai iliyo
bora.
"Uzuri wake ni
kwamba wanapata nafasi ya kuweza kushirikiana na kupeana uzoefu na
wazalishaji wengine kwasababu tuna wazalishaji wengi kutoka viwanda
mbalimbali hapa nchini " alisema Safari.
Alisema
siku ya mwisho ya mafunzo hayo wataingia katika sehemu ya masoko hii
ni baada ya kujifunza namna ya kuongeza thamani ya zao hilo la chai.
"Wamepata
kile ambacho soko linahitaji sasa ni namna gani ya kupata masoko mazuri
duniani pamoja na ukanda huu wa jumuiya ya Afrika mashariki hiyo hasa
ndiyo dhamira yetu" alisema Safari.
Aliushukuru
umoja wa nchi za ulaya kwa kuwa sehemu ya kutoa ufadhili katika mradi
wa Markup pamoja na Kibena tea ambao wamekubali kiwanda chao kuwa sehemu
ya kuweza kuendesha mafunzo hayo kwa njia ya vitendo.
Baadhi
ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo meneja uzalishaji Stanslaus Benela
na meneja mashamba kutoka kiwanda cha chai Kibena walisema mafunzo
hayo yatawajengea ujuzi kwa kuongeza ubora kwa kile wanachokizalisha
shambani nakupunguza gharama za uendeshaji ili wawekezaji wapate faida
zaidi.
"Kupitia Markup
na program hii waliyoifanya sisi tumeifurahia sana kwani imetuongezea
ujuzi zaidi na kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji" alisema
Stanslaus.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...