Sehemu ya wananchi wa Kijiji cha Madabala katika Kata ya Visiga mkoani Pwani wakiwa kwenye kikao cha kutoa maombi yao kwa Rais Samia Suluhu Hassan awasadie kupata haki yao ya ardhi ambayo waadai imechukuliwa bila kufuata utaratibu.

Mwenyekiti wa wananchi hao Ally Kawanda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua mbalimbali ambazo wamezipitia katika kuhakikisha wanapata haki yao , lakini kwa hali ilipofikia wameamua kutoa kilio chao kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili awasaidie kupata haki yao.
Ally Kawanda ambaye ni Mwenyekiti wa wananchi hao akitumia vifungu vya Katiba kufafanua mgogoro uliopo kati yao na mtu aliyepewa ardhi yao bila utaratibu.

Mmoja ya wananchi wa eneo hilo akitoa ya moyoni mgogoro huo.


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

TUNAOMBA Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie kupata haki yetu! Ndivyo wanavyoeleza wananchi wa Kijiji cha Madabala katika Kata ya Visiga mkoani Pwani ambao wanamuomba Rais awasadie kupata haki yao ya ardhi hekari 561 ambazo kwa sasa zinaonekana kutaka kuchukuliwa kiujanja ujanja na mmoja ya watu aliyejitambulisha muwekezaji.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wawakilishi wa wananchi hao ambao wanadai kuporwa ardhi yao bila kufuata utaratibu wa kisheria hasa kwa kuzingatia kwa nyakati tofauti imeonekana kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia madaraka yao kuhakikisha wananchi wanaondolewa wakati ukweli wa maeneo hayo ni ya kwao na wapo kwa miaka mingi.

Wamesema kwa hali ilipofika sasa , wamebaki na matumaini makubwa na Rais Samia Suluhu Hassan tu ambaye anaweza kuwasaidia kupata haki yao , kwani wanaamini ni Rais ambaye anataka kuona haki inatendeka ingawa wamekiri kuwa Waziri wa Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi atakuwa kiunganishi kizuri wao kupata haki yao maana viongozi ambao wamekuwa wakishiriki kupora ardhi hiyo wako kwenye ngazi ya Wilaya na kitengo cha ardhi kanda ya Pwani.

Akizungumza Mwenyekiti wa wananchi hao amesema kuwa wananchi hao wakazi na wakulima wa Madabala Mtaa wa Mbwawa wilayani Kibaha mkoani Pwani wameamua kupaza sauti zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan hali ya kuwa wenye huzuni na maumivu makubwa.

"Rais wetu , tukiwa katika makazi yetu mwaka 2010 tulifunguliwa kesi na Abdallah Sagaf katika Baraza la ardhi na nyumba Kata ya Visiga wilayani Kibaha kwa madai tupo ndani ya shamba lake lenye ukubwa wa heka 561 alilonunua kwa Said Sinaela mwaka 1986 na kulihudumia kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 1989.

"Baraza lilipomtaka alete hati ya mauziano ama aliyemuuzia alishindwa kuleta vielelezo (ushahidi) na hatimaye akaanza kutumia baadhi ya askari Polisi kituo cha Mlandizi na kukamata wananchi wawili, shauri hili lilihamishwa baraza la ardhi Wilaya , hata hivyo halikuweza kufunguliwa.

"Mheshimiwa Rais mwaka 2011 tulifuguliwa kesi Mahakama Kuu kitengo cha ardhi na Hasshim Sagaf kuwekewa pingamizi la kisheria kutokana na nyaraka alizowasilisha mahakamani zilisababisha ashindwe kufika mahakamani zaidi ya miaka miwili,"amesema Kawanda na kuongeza ilipofika mwaka 2018 alijitokeza Abdallah Saggaf kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo na kudai wamevamia ardhi yake na kujitambulisha kuwa yeye ni mtoto wa Saggaf."Tulimfahamisha Mkuu wa Wilaya hatua zote ambazo tulizopitia na kumkabidhi hukumu ya Mahakama.

"Lakini Mkuu wa Wikaya kwa kushirikiaa na na baadhi ya viongozi wa Halmashauri walidhamiria kwa gharama kutupola ardhi yetu kwa kivuli cha Saggaf ambao sasa walimuita muwekezaji anayepima viwanja na kuuza."

Ameongeza kuwa katika kipindi chote tangu mwaka 2018 wananchi hao wanapitia kipndi kigumu , kwani baadhi ya vyombo vya ulinzi viliweka kambi kwenye makazi yao wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi , jambo ambalo liliwauma sana.

Amesisitiza kutokana na hali hiyo waliamua kuandika barua kwa Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ambapo walipata ushirikiano mkubwa sana lakini bahati mbaya mmoja ya makamishna wake wa ardhi Kanda ya Dar es Salaam aliamua kufanya mkutano nje ya eneo la mgogoro na wananchi ambao si walengwa.

"Akatoa uamuzi ya kukabidhi shamba kwa Saggaf wakati akijua fika ni ardhi yetu, nyumba na mazao yetu hili ndio jambo lililotuumiza mno.Tunakuomba Rais wetu, Mama yetu suala hili liwe kwenye mikono yako na sisi tunamaini yetu yamebakia kwako , tunaimani la Lukuvi lakini kwa tulikofika tunaomba ulipokee na utusaidie tupate haki yetu,"amesema Kawanda kwa niaba ya wananchi hao ambao ni zaidi ya kaya 400 walioko eneo hilo.

Adha amesema kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa kisheria kwani pamoja na shauri hilo kuwepo mahakamani lakini, wanashangaa wakiona unatolewa uamuzi na Kamishna wa ardhi Kanda ya Dar es Salaam la kukabidhi ardhi hiyo kwa mtu ambaye si haki yake , hivyo wanaona kuna ukiukwaji mkubwa wa kisheria ambao unafanyika kwa maksudi.

Mkazi mwingine wa eneo hilo Abdallah Kalunga amesema wamekuwa wanyonge katika ardhi yao, hivyo wanachokiomba ni wao wapatiwe haki yao na kupitia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia pamoja na wasaidizi wake Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanaamini haki itatendeka.

Amesisitiza Rais Samia ni msikivu na mtetezi wa wanyonge hivyo kupitia uongozi wake watapata haki yao na hicho ndicho wanachoamini.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...