Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akifanya mazungumzo na mgeni wake Balozi wa Uholanzi nchini Jeroen Verheul ofisini kwake Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akiangalia kitabu cha mbegu bora za aina mbalimbali za viazi mviringo vilivyoboreshwa ambacho kimeandaliwa na kuchapishwa na Ubalozi wa Uholanzi nchini ambacho alipewa na Balozi Jeroen Verheul ofisini kwake Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akipokea zawadi ya kitabu chenye taarifa mbali kuhusu taifa la Uholanzi kutoka kwa Mgeni wake Balozi Jeroen Verheul ofisini kwake Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.

Sehemu ya Wataalam kutoka Ubalozi wa Uholanzi wakiongozwa Abdallah Msambachi (Kulia) ambaye ni Mshauri wa masuala la kilimo wakifuatilia mazungumzo ya Waziri wa Kilimo na Balozi wa Uholanzi.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akiwa pamoja na Mgeni wake Balozi wa Uholanzi nchini Jeroen Verheul nje ya ofisi yake Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.

*************************************

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda leo (Jana) tarehe 9 Aprili 2021 amekutana na Balozi wa Uholanzi nchi Jeroen Verheul na kumwambia Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji katika Sekta ya Kilimo na kumuomba kushawishi uwekezaji kwenye Sekta ya Kilimo hususan kwenye uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta, usindikaji wa mafuta ya kula, uzalishji wa mazao ya mboga, matunda, viungo,maua pamoja na upatikanaji masoko ya mazao hayo.

“Nafikisha ombi kwako la kutusaidia kushawishi Wawekezaji zaidi nchini kwenye eneo la uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta, usindikaji wa mafuta ya kula na usindikaji wa mazao ya aina mbalimbali kwenye Sekta ya Kilimo pamoja na masoko ya mzao hayo.” Amesisitiza Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda amesema Wizara ya Kilimo imejipanga ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo inachangia ukuaji wa uchumi kwa kuongeza mara dufu fedha katika eneo la utafiti wa mazao ya mbegu za mafuta kama alizeti na pamba, uzalishaji wa mazo ya kimkakati pamoja na huduma za ugani na kuahidi kuwa mambo hayo yamewekwa kwenye utekelezaji wa bajeti inayokuja ya mwaka 2021/2022.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa fedha na msisitizo umewekwa kwenye kuzalisha mazao ya mbegu za mafuta ili kupunguza utegemezi kwenye eneo hilo ambalo nchi imekuwa ikitumia zaidi ya shilingi bilioni 400 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.

Waziri Mkenda amesema kwa kuanzia Vituo vya Utafiti vitajikita katika kutafiti mbegu bora za mazao ya mbegu za mafuta ili kuja na mbegu bora lakini pia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kupitia mashamba yake; ASA itazalisha mbegu bora kwa wingi ambazo zitauzwa kwa Wakulima kwa bei nafuu.

Eneo lingine ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani kote nchini na kwa kuanzia Wizara imepanga  kuwawezesha Maafisa Ugani wa mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu kupata vitendea kazi kama kama pikipiki na kuwezeshwa pembejeo bora za kuanzisha mashamba darasa kwa kila Afisa Ugani.

“Pamoja na juhudi zote hizo lengo letu ni kuhakikisha tunatatua tatizo la masoko kwa Wakulima wetu lakini pia kuongeza uwekezaji kwa ujumla na ndiyo maana tunaona juhudi hizi tuwashirikishe na Sekta Binafsi ambayo itasaidia katika mageuzi katika kuendesha kilimo cha kisasa”. Amekaririwa Profesa Mkenda.

Kwa upande wake Balozi wa Uholanzi nchini Jeroen Verheul ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye Sekta ya Kilimo hususan kwenye uzalishaji wa mbegu bora za zao la viazi mviringo kupitia Mradi wa SHAWISHA unaotarajiwa kuanza baada ya kusimama kwa muda.

“Tutaendela kusaidia kwenye biashara ya mazao ya kilimo na uwekezaji kwa ujumla kwa sasa na kwa baadae hususan kwenye eneo la uzalishaji wa mbegu bora za viazi mviringo”. Amesisitiza Balozi Jeroen Verheul.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...