Na.Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali
inaendelea na utekeleza wa miradi mingi ya kuimarisha miundombinu
katika sekta mbalimbali ikiwemo mradi ya umeme (JNHPP-Julius Nyerere
Hydropower project) kwa gharama ya TZS Trilioni 6.5, Ujenzi wa Reli ya
Kisasa SGR kwa gharama ya shilingi trilioni 7 na miradi mingine ambayo
itaweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya biashara na uwekezaji.
Mnamo
Desemba 8, 2019, Rais wa Awamu ya Tano Hayati, Dkt. John Magufuli
alizindua ujenzi wa mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa meli kubwa ya
abiria na mizigo, ukarabati wa meli na ujenzi wa chelezo katika lango
la biashara na kiuchumi kanda za ziwa ambao utekelezaji wake unaendelea
vizuri ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya shilingi
bilioni 153.
Meli ya “MV Mwanza Hapa Kazi” itakayogharimu
shilingi bilioni 89, ni mradi wa ujenzi ambao unatekelezwa na kampuni
ya ujenzi ya GAS ENTEC wakishirikiana na KANG NAM kutoka Korea Kusini
pamoja na SUMA JKT kutoka Tanzania. Meli hii itakuwa mbadala wa meli ya
MV Bukoba ambayo miaka 25 iliyopita ilizama na kupoteza maisha ya
Watanzania wengi. Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015 Rais wa Awamu
ya Tano, Hayati, Dkt John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa kanda ya
ziwa kuwa atajenga meli kubwa kuwaenzi waliokufa kwenye ajali hiyo
lakini pia kuimarisha usafirishaji upande huo wa Tanzania kwani kuna
fursa nyingi za biashara, anaeleza Meneja Mradi Mhandisi, Vitus
Mapunda.
Katika moja ya Hotuba zake akiwa ziarani Jijini Mwanza
2019, Hayati Magufuli alisema “Ni miaka 23, Baada ya kuzama meli ya MV
Bukoba mwaka 1996, miaka mingi imepita, lakini pia kuharibika kwa meli
ya mizigo kumekuwa na tatizo kubwa katika sekta ya usafarishaji kwa
wananchi wanaioshi kuzunguka ziwa Victoria na hivyo kuathiri shughuli za
uchumi na uzalishaji kanda ya ziwa”.
Serikali ya Awamu ya Sita
Chini ya Jemedari, Samia Suluhu Hassan, inaendelea na utekelezaji wa
mradi huo mkubwa ambao uliambatana na miradi mingine kama vile ukarabati
wa meli ya Mv Victoria uliogharimu shilingi bilioni 22.7, Mv Butiama
bilioni 4.9, ambapo ujenzi wake ulitekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya
KTMI kutoka Korea Kusini huku ujenzi wa chelezo uliogharimu shilingi
Bilioni 36.4, ukitekelezwa na Stx Engine ikishirikina na SAE Kyong
kutoka Korea Kusini. Kati ya miradi hiyo, ujenzi wa chelezo na ukarabati
wa meli mbili umekamilika na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi
Tu ukiwa umefikia asilimia zaidi ya 50, na miradi yote hii itagharimu
shilingi bilioni 153.7, baada ya kukamilika na miradi yote hii
inatekelezwa kwa pesa za Watanzania.
MV Mwanza Hapa Kazi tu,
itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo tani 400, magari makubwa
3 na magari madogo 20, huku ikiwa na urefu wa mita 92, ambapo MV.
Victoria ikibeba abiria 1,200, mizigo tani 200 na MV. Butiama ikibeba
abiria 200 na mizigo tani 100. Meli zote tatu zitakuwa na uwezo wa
kubeba abiria 2,600 na tani 700 za mizigo, kwa wakati mmoja na hivyo
kupunguza adha ya usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo katika
ukanda huo.
“Ni wazi kuwa utekelezaji wa miradi hii
utakaogharimu shilingi bilioni 153 utasaidia sana kutatua tatizo la
usafirishaji kwa wananchi wanaoishi ziwa Victoria, siyo tu hapa nchini
bali hata kwa jirani zetu Kenya na Uganda kwa hiyo ni miradi ambayo ina
manufaa kwa uchumi wetu”, Hayati, Dkt. John Magufuli.
Aidha,
Serikali ya Awamu ya Sita inaeleza kuwa ujenzi wa mradi huo mkubwa MV
Mwanza Hapa Kazi Tu, utafungua ukanda huo kibiashara na kusaidia kukuza
pato la taifa, kama ilivyokuwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano Serikali ya
sasa imejitabanaisha kuendelea kufanya mabadiliko makubwa kwa kuleta
miradi wezeshi kwa wananchi bila kutegemea misaada yenye masharti
lukuki.
Sekta hii ya usafirishaji kwa njia ya maji imekuwa muhimu
sana na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) pamoja na Shirika la Huduma za Meli Tanzania (MSCL) wamekuwa na
usimamizi madhubuti ili kukuza sekta hiyo kwani ni nyenzo kubwa katika
uchumi.
Kampuni ya Huduma za meli iliyoanzishwa na Hayati Baba
wa taifa Mwl. Julius Nyerere kwa sasa inafanya kazi kubwa baada ya
Hayati, Dkt. Magufuli kuingia madarakani na kuiongezea nguvu kifedha na
kiutendaji. Kijiti hicho kwa sasa kipo kwa Rais Samia Suluhu Hassan,
kwani hapo mwanzo ilikuwa na meli 14 ikiwemo meli ya utalii lakini
ilikuja kuanguka kutokana uongozi mbovu, vitendo vya wizi na ubadhilifu
wa mali za umma na kufanya meli zote 14 kufa na kubaki na moja tu.
TPA
imekuwa ikiendelea na upanuzi na ujenzi wa Bandari mbalimbali nchini
zikiwemo bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza pamoja na
bandari zake ndogondogo za Kemondo, Bukoba, Kwemukwikwi na Nyamirembe
kwa upande wa kanda ya ziwa, na Bandari ya Kigoma.
Mhandisi
Mapunda anaeleza kuwa Ujenzi wa Meli mpya “Mv Mwanza Hapa Kazi Tu”
umefikia asilimia 53 tofauti na sasa ujenzi unaendelea vyema ili
kuwawezesha wafanyabiashara wa ukanda huo kuwa na nafuu ya usafiri na
usafirishaji mizigo baada ya mradi huo kukamilika.
Utekelezaji
wa miradi hiyo umeweza kutoa fursa nyingi kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza
ikiwemo ajira kwani mpaka sasa kuna ajira zaidi ya 1,000 na bado
zinaongezeka kwa kadri siku zinavyosonga mbele katika utekelezaji wa
miradi hiyo mikubwa kwa kanda ya ziwa.
Ujenzi wa Meli hii Kubwa
ni utekelezaji wa ahadi na kufanya maono ya Baba wa Taifa Mwl.Julius
Nyerere aliyetaka kuwepo na meli kubwa kwa ukanda huo wa kiuchumi wa
Tanzania, na alijenga MV Bukoba iliyokuja kuzama mwaka 1996 na kuleta
ugumu wa sekta ya usafirishaji kutumia Ziwa Victoria na sasa Serikali
inayaishi maono ya Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere, baada ya
kujenga MV Mwanza Hapa Kazi Tu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...