Na Said Mwishehe, Michuzi TV
DIWANI wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) katika Halmashauri ya Wilaya Ubungo mkoani Dar es Salaam Liberatha Samson amendaa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake wa halmashauri hiyo ili kuwawezesha na kuwajengea uwezo katika shughuli zao za ujasiriamali.
Katika mafunzo hayo yaliyofanyika ukumbi wa Nable Hall uliopo Kimara Mwisho , wanawake wajasiramali zaidi ya 450 wamenufaika kwa kupata mafunzo hayo ambapo watalaamu wa masuala ya ujasiriamali na saikolojia walitoa elimu hiyo.
Akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa mafunzo hayo Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Ubungo Liberatha Samson amesema ameandaa mafunzo hayo ili kuwasaidia wanawake wajasiriamali kutambua fursa zilizopo sambamba na kuwajengea uwezo na uwelewa kuhusu shughuli za ujasiriamali.
"Lengo la semina hii ni kuwaongezea ujuzi na uwezo wa kufanya vizuri katika shughuli za ujasiriamali.Semina hii inatoa fursa ya kuzungumza fursa ambazo zipo katika halmashauri yetu ya Ubungo.
"Kupitia mafunzo haya ya ujasiriamali wanawake wa Ubungo watakwenda kufanya vizuri kwenye shughuli zao za ujasiriamali na hivyo kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi kwa faida yao , halmashauri na Taifa la Tanzania kwa ujumla.
"Semina hii ya ujasiriamali nimeandaa mimi , kwa nafasi yangu ya Diwani Viti Maalum nimeamua kufanya kazi na akina mama na mafunzo haya ya ujasiriamali yatakuwa endelevu kwa kushirikiana na Liberatha Foundation itakayokwenda kufanya tathimini na kuangalia changamoto wanazokutana nazo wanawake, kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo pamoja na kusaidia katika biashara zao,"amesema.
Ameongeza aliona kuna upungufu wa uelewa, upungufu wa ujuzi katika hizo biashara ndogo ndogo."Na ukiangalia Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imekuwa ikitoa mikopo ya fedha asilimia 10 kwa ajli ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
"Na kuna mikopo ya kutoa vifaa, hivyo wanashidwa kukopesha katika mikopo hii ya vifaa maana hawajui wanakwenda kufanya nini.Tukaona ni vema nikaleta semina ili wapate ujuzi wa kutumia fursa zilizopo Halmashauri ya Ubungo ili waweze kunufaika na mikopo ambayo inatolewa ya asilimia 10.
"Kwanza kabisa kabisa mimi ni diwani ninayetokana na Chama Cha Mapinduzi na tunajua Chama chetu kina viongozi ambao wamesambaa kwenye mashina na ndio maana imekuwa rahisi kuwapata wanawake wengi kiasi hiki ambao wamevuka idadi tuliyokusudia.Leo wamefika wanawake 450 kuja kupata mafunzo haya , kwangu ni jambo la faraja na niahidi nitaendelea kutoa mafunzo kwa ajili ya wanawake wa Ubungo,"amesisitiza.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Halmashauri ya Ubungo Chief Silvester Yered amempongeza Diwani huyo wa Viti Maalum Ubungo kwa kuandaa semina hiyo ambayo inakwenda kunyanyua maisha ya wanawake wa Ubungo hasa wale ambao wanajishughulisha na ujasiriamali.
"Tunampongeza kwa uamuzi huu wa kusaidia wanawake, ni jambo jema sana ambalo Diwani Libetatha amelifanya ndani ya halmashauri ya Ubungo, amekuwa na mtazamo chanya dhidi ya wanawake na ametumia nafasi yake kama kiongozi kuwasaidia wanawake wajasiriamali.
"Chama tunasema tuko pamoja naye, mafunzo haya ya ujasiriamali yatasaidia hata pale watakapopata mikopo watajua namna ya kuitumia vizuri katika kufanya shughuli zao za ujasiriamali,"amesema.
Wakati huo huo Mmoja ya wanawake wajasiriamali Dalini Abdull amesema mafunzo hayo yamemuongezea uelewa kuhusu ujasiriamali na hata akitoka hapo anakwenda kufanya vizuri zaidi.
"Kupitia mafunzo hayo sasa nimefahamu namna sahihi ya kufanya katika shughuli zangu za ujasiriamali, nitatumia vema fedha za mikopo ambazo tunazipata aidha katika halmashauri au Serikali kuu."
Naye Katibu wa CCM Kata ya Saranga ametumia nafasi hiyo kumpongeza Liberatha kwa kuandaa mafunzo hayo."Sisi wanawake tunakila sababu ya kupatiwa mafunzo haya ili yatusaidie kwenye shughuli zetu, tunafahamu tulio wengi tunafanya biashara ndogondogo lakini kupitia mafunzo haya tunakwenda kuwa wafanyabiashara wakubwa."
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...