UBALOZI  wa Denmark nchini Tanzania umeipatia Foundation for Civil Society (FCS) fedha za nyongeza kiasi cha fedha za nchi hiyo  Krone milioni 4.3 ambazo ni sawa na Sh. bilioni 1.6 kwa lengo la kuchangia maendeleo endelevu nchini.

Fedha hizo za nyongeza zinaleta jumla ya Sh.bilioni 4.4 za ufadhili wa Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania kwa asasi ya kiraia kwa muhula wa mwaka 2021.Aidha Ubalozi huo  kupitia Shirika la Maendeleo la kimataifa DANIDA, umesaini makubaliano ya kuongeza msaada wa Denmark kwa FCS Mei 5, 2021.

Mkataba huo umesainiwa na Balozi wa Denmark nchini Tanzania Mette Nørgaard Dissing- Spandet na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga.

Akizungumzia baada ya kusainiwa kwa fedha hizo, Balozi huyo ameeleza sababu za ubalozi wa Denmark kushirikiana na asasi za kiraia hasa  FCS  huku akifafanua wanafanya kazi kwa kushirikiana na asasi za kiraia, kwa sababu wanaamini asasi za kiraia ni kiini katika kuhakikisha mamilioni ya watu wanakua, wanawezeshwa kimaendeleo.

Pia mamilioni ya wasichana na wanawake, na watu wenye ulemavu wanakuwa na uwezo wa kupaza sauti zao katika jamii na kusikika, kuwa na uwezo wa kushiriki katika maisha ya kisiasa, kiuchumi na namna ya kuitambua jamii inayowazunguka na umuhimu wa Utamaduni wake.
 
"Hivyo tumependezwa na tunajivunia kwamba, leo tumetia saini ya mkataba mpya wa nyongeza ya jumla ya kiasi cha fedha za kidenmark (Danish Krone) milioni 4.3(Sh.bilioni 1.6).Kiasi hiki tunatarajia kitumike vyema katika kuzifikia asasi za kiraia takribani 130 za kitanzania.

"Kwa misingi chanya ya kuhamasisha Utawala kidemokrasia, kuimarisha usawa wa kijinsia na kuboresha maisha ya Watanzania wengi,” amesema Balozi Mette Nørgaard Dissing- Spandet.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga amesema kuwa Denmark imekuwa ikisaidia jitihada za FCS kuboresha Maisha ya Mamilioni ya Watanzania hasa jamii katika ngazi za vijijini na makundi ya pembezoni.

Akizungumzia kuhusu ufadhili wa ziada uliopokelewa, kiwanga alibainisha kuwa FCS inatarajia kuongeza mafanikio zaidi kwa wananchi kupitia kazi zake.

"Sasa tuko kwenye kipindi cha mpito kutoka kukamilika kwa mpangomkakati wa 2016 - 2020 miaka hiyo tuliweza kufikia zaidi ya wanachi milioni 5 nchi nzima katika juhudi za kuwawezesha wananchi kushawishi utawala wa kidemokrasia na unaojumuisha watu wote.

"Kwa mfano, miradi yetu ya uwajibikaji jamii imewawezesha wananchi kufuatilia miradi ya umma ipatayo 945 yenye thamani ya takribani Tsh bilioni 312. Programu zetu za uwezeshaji kiuchumi zimechangia katika Manispaa kadhaa nchini kutoa Sh. Milioni 406 kama mikopo kusaidia shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu na vijana. kupitia programu hii pia tumechangia katika vijana kupata Sh. bilioni 6.34 kama mikopo ya halmashauri.
 
"Pia tumewezesha wananchi kuripoti visa 8,887 vya ukatili wa kijinsia (GBV) na hivyo kusaidia kupatikana  kwa haki za maelfu ya wanawake na wasichana nchini. Miradi yetu ya haki za ardhi pia imewezesha zaidi ya wanawake 3,400 kote nchini kupata hati zao za kimila za umiliki wa zaidi ya ekali 4,575 za ardhi zenye makisio ya thamani takriban Sh. bilioni 17,"amesema.

Ameongeza fedha hizo za nyongeza zitasaidia  kuhakikisha tunadumisha jitihada zilizoleta mafanikio kwa jamii, kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuongeza tija ya kazi zao wanapojitahidi kutoa mchango mkubwa wa kujenga Tanzania tunayoitaka.

Tangu mwaka 2017 hadi mwaka huu wa 2021 Ubalozi wa Denmark kupitia shirika lake la maendeleo DANIDA limegharimu kiasi cha Sh.bilioni 15.5 kwa asasi ya kiraia ya FCS.


Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Nørgaard Dissing- Spandet (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga (kulia) wakikabidhiana hati za mkataba wa fedha ya ruzuku ya nyongeza Sh. Bilioni 1.6 kutoka Denmark kwaajili ya kuisaidia FCS kuweza kutekeleza miradi ya Asasi za Kiraia Chini.


Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga (kulia) akiweka saini wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa Sh Bilioni 1.6 kutoka Ubalozi wa Denmark kwaajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ya Asasi za kiraia nchini Tanzania.


Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Nørgaard Dissing- Spandet (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga (kulia) wakionesha mkataba waliosaini mara baada ya kumalizika kwa zoezi hilo katika Ofisi za FCS Jijini Dar es Salaam.



Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Nørgaard Dissing- Spandeta kizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani) wakati wa hafla hiyo. (kushoto) ni Balozi wa Denmark nchini Tanzania Mette Nørgaard Dissing- Spand


Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Nørgaard Dissing- Spandet (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga (wa nne kulia), Menejimenti ya FCS na Afisa wa DANIDA mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kutia saini mkataba wa fedha za Kitanzania Sh Bilioni 1.6 kutoka ubalozi wa Denmark katika Ofisi za FCS Jijini Dar es Salaam..

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...