WAKAZI wa Mkoa wa Katavi wameipongeza Benki ya NBC kwa kuzindua NBC Wakala Plus katika Manispaa ya Mpanda kwani kwa uwepo wa wakala mkuu huyo utafungua fursa zaidi za kiuchumi, kuziendeleza pamoja na kuinua uchumi wa wafanyabiashara katika Mkoa huo.
Akizungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara waliohudhuria katika hafla hiyo ya uzinduzi wa tawi hilo la NBC Wakala Plus, Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Katavi Komredi Juma Zuberi Homera ameupongeza uongozi wa Benki ya NBC kwa kuja kuwekeza katika Mkoa huu ambapo watu zaidi ya elfu moja wameshafungua akaunti katika tawi hilo.
Komredi Homera aliupongeza uongozi wa Benki ya NBC kwa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wa Katavi. Mafunzo hayo yalifanyika kwa muda wa siku mbili katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda. Komredi Homera pia aliusihi uongozi wa Benki ya NBC kutoa mikopo kwa wajasiriamli wa Katavi ili matunda ya mafunzo hayo yaonekane kwa haraka.
Aidha Homera ameishukuru Benki ya NBC kwa kutoa msaada wa mifuko 300 ya saruji, Bati 60 sambasamba na ndoo 5 za rangi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Mpanda.
Homera pia ameipongeza Benki ya NBC kwa kufika Mkoani Katavi na kuwakaribisha kwani fursa zipo nyingi katika mkoa huo zikiwemo za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na mazao ya kimkakati. Pia Mkuu wa Mkoa wa Katavi aliuhakikishia uongozi wa Benki ya NBC kwamba Katavi ni mkoa unaokua kwa kasi sana kutokana na shughuli za uzalishaji na za kimaendeleo hivyo huduma ya NBC Wakala Plus waliyoifungua imekuja kwa wakati muafaka.
“Kuzunduliwa kwa NBC Wakala Plus hapa Katavi maana yake ni kwamba huduma za kibenki zitapatikana kwa urahisi zaidi hivyo wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara wa Katavi changamkieni fursa hii na kuja kufungua akaunti na kufanya miamala mengine kama kulipa kodi za serikali.” alisisitiza Homera.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Theobald Sabi alisema kuwa wameamua kufungua NBC Wakala Plus katika Manispaa ya Mpanda kwani manispaa hiyo inakuwa kwa haraka kiuchumi kutokana na miradi mingi ya kimakakati iliyoanzishwa na serikali awamu ya tano na inayoendelea katika awamu ya sita.
"Na sisi NBC tumeona ni muhimu kuwa hapa ili tushirikiane na wananchi wa Katavi pamoja na wafanyabiashara katika kuhakikisha kwamba tunaziendeleza fursa hizi za kiuchumi ukizingatia nchi yetu ipo katika mkakati wa kukuza viwanda na kuongeza thamani katika mazao. Hivyo hiyo ni katika kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na huduma na elimu za kifedha,"alisema
"NBC Wakala Plus pia inatupa sisi fursa kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kufungua akaunti zinazolenga makundi tofauti zikiwemo NBC Shambani, Kuwa Nasi Akaunti inayolenga wajasirimali wadogo, Johari akaunti kwa ajili ya wanawake, Akaunti ya Chanua kwa watoto na akaunti kwa wanafunzi na wafanyakazi lakini pia kupata huduma za Bima mbali mbali.”
Sabi aliongeza kuwa Benki ya NBC pia ina fursa za mikopo kwa wafanyabiashara, waajiriwa na wakulima ili waweze kuongeza thamani katika mazao yao, kununua pembejeo kama matreka na kadhalika ili kuongeza uzalishaji.
Aidha kwa upande wake mfanyabiashara maarufu Mkoani Katavi, Raymond Kamtoni alisema kufunguliwa kwa NBC Wakala Plus imekuwa faraja na ni fursa kubwa kwa Wanakatavi kwani benki hiyo imetoa na itaendelea kutoa mafunzo ya usimamizi wa biashara na fedha hivyo kuwasisitiza wafanyabiashara wenzake kufungua akaunti na kushirikiana na Benki ya NBC katika huduma zake zote.
Mchekeshaji maarufu, Emmanuel Mgaya ambaye alikuwa mshereheshaji katika hafla ya uzinduzi wa NBC Wakala Plus Mkoani Katavi akiendesha shughuli hiyo baina ya baadhi ya wageni waalikwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...