

WATAFITI wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), wamebaini fursa mbalimbali zilizoko kwenye majitaka ya vyooni na kinyesi cha bindamu.
Fursa hizo ni gesi ya majumbani, mbolea na maji ya kumwagilia mashambani ambayo yamesafishwa kutokana na majitaka kutoka vyooni na kinyesi.
Hayo yamebainishwa na watafiti hao kwenye kituo chao cha utafiti chuoni hapo walipokuwa wakielezea namna wanavyozalisha mbolea na gesi katika kituo cha cha utafiti cha Sanitation Biotechnologies Research Center chuoni hapo..
Mmoja wa watafiti hao, Edward Ruhinda ambaye ni Mtafiti wa Shahada ya Uzamivu, amesema moja ya vitu vinavyozalishwa ni gesi ambayo inaweza kutumika majumbani.
Ruhinda anafanya utafiti wa uchakataji wa tope choo kupata rasilimali gesi, mbolea ya mboji na maji taka kuwa safi ambayo hutumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Jonas Gervas anafanya utafiti wa kuangalia athari za utumiaji wa maji taka yaliyochakatwa kwenye udongo na kwenye mimea na mazao yaliyomwagiliwa.
Fredrick Ligate anafanya utafiti wa matumizi ya mifumo midogo ya ukusanyaji maji taka na uchakataji pamoja na taka ngumu zinazooza.
Ruhinda amesema wamekuwa wakichukua maji taka na kuyasafisha ambapo baada ya hapo yanaweza kutumika kumwagilia mashamba na mimea kuwa safi kwa matumizi ya binadamu
Amesema wamekuwa wakichukua tope ngumu ya kinyeshi kuichakata na kutengenezea mbolea ambayo inaweza kutumika katika kukuzia mazao mbalimbali na kutumiwa na binadamu.
Ameongeza kuwa, kwa kutumia taka ngumu zinazotokana na kinyesi cha bidadamu na kutengenezea biogesi ambayo inaweza kutumika katika matumizi ya nyumbani kama ilivyo kwa gesi asilia.
Amesema gharama ya kusafirisha majitaka na kinyesi vyooni ni kubwa kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kuhifadhia hivyo tafiti hizo zinafanyika kujaribu kuokoa hali hiyo.
Ametoa mfano kuwa hivi sasa kuna maeneo mawili tu ya kuhifadhia majitaka na kinyesi ya DAWASA maeneo ya Vingunguti na Kurasini pekee hivyo wanafanya tafiti kupata sehemu rahisi za kuhifadhia kuokoa gharama inayotumiwa kusafirisha.
Kuhusu namna wanavyochakata tope taka, Ruhinda alisema wanatengeneza mazingira kama ya tumboni kuwezesha mfumo wa umeng’enyaji wa kinyesi kuendelea kufanya kazi ili kupata gesi hiyo na mbolea.
Amesema kutokana na uhaba wa maji duniani mataifa mengi sasa yanatumia majitaka yaliyochakatwa kwa shughuli mbalimbali kama umwagiliaji kwenye kilimo na hayana sumu.
Amesema ili kubaini kama maji taka yanayotumika kumwagilia hayana madhara wameanzisha mashamba darasa ya kumwagilia kwa kutumia maji taka yaliyochakatwa na mashamba yanayomwagiliwa kwa kutumia maji safi ili kubaini tofauti kwenye mazao hayo.
"Kwenye mashamba haya, mazao yanayomwagiliwa kwa kutumia maji yaliyochakatwa yameonyesha kukua na kustawi kwa haraka sana kulinganisha na yale yanayomwagiliwa kwa kutumia na maji safi...,watu hawapaswi kuwa na wasiwasi na majitaka yanayochakatwa kwasababu yanatumika sehemu mbalimbali duniani na yakishachakatwa hayawi na sumu yoyote yanakuwa salama kwa matumizi,” amesema.
Kudos kwa watafiti wetu na Chuo kikuu kwa ujumla.
ReplyDelete