Charles James, Michuzi TV
BARAZA la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) linatarajia kufanya uchaguzi wake wa kitaifa Julai 8, mwaka huu jijini Dodoma.
Aidha, kabla ya Julai 10, mwaka huu uchaguzi wa Baraza hilo kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa utakuwa umekamilika na viongozi wapya kukabidhiwa rasmi ofisi.
Hatua hiyo inafuatia agizo la Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima kutoa siku 30, kwa Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO) kufanya uchaguzi wake.
Akizungumza na Wandishi wa Habari jijini Dodoma leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchagauzi wa NaCoNGO, Wakili Flaviana Charles amesema utekelezaji huo wa uchaguzi unatokana na maelekezo ambayo yalitolewa na Waziri Dk Gwajima.
Amesema kuwa Juni 7, Mwaka huu Waziri Dk Gwajima alifanya uteuzi wa kamati ya mpito kwa ajili ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa Baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Kamati hiyo inaundwa na wajumbe 10, kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali ya kitaifa na kimataifa na ilipewa siku 30, kufanikisha zoezi hilo," Amesema Wakili Flaviana.
Amesema kuwa jukumu la kamati hiyo ni kuratibu na kusimamia uchaguzi wa Baraza hilo.
Amesema kuwa baraza litakaloundwa litakuwa na wajumbe 30, kati yao 26, kutoka katika mikoa yote ya Tanzania bara na wajumbe wanne watachaguliwa kutoka katika makundi maalum.
Wakili Flaviana amesema makundi hayo ni pamoja na mashirika ya kimataifa, watu wenye ulemavu pamoja na watoto na vijana.
“Kwa msingi huo taarifa hii inalenga kutoa tathimini ya mwenendo wa uchagauzi wa Baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali hususani ngazi ya wilaya uliofanyika Juni 26, mwaka huu," Amesema Flaviana.
Akizungumzia chaguzi za ngazi ya chini amesema kwa ujumla uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu katika wilaya zaidi ya 130, za Tanzania bara ambapo kumekuwepo na mwitikio mkubwa na hamasa ya hali ya juu kwa wagombea na wapiga kura.
“Tathimini ya ujumla katika wilaya zaidi ya 130, zilionyesha zoezi hilo kati ya watia nia watano waliochukua fomu za kuomba uongozi wa baraza jumla ya watia nia wanne walirudisha fomu hizo kwa msingi huo zoezi la kuchukua na kurudisha fomu lilifanikiwa kwa takribania asilimia 80," Amesema Wakili Flaviana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO), Wakili Flaviana Charles akizungumza na wandishi wa habari JIJINI Dodoma leo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...