Na Karama Kenyunko Michuzi TV.
ALIYEKUWA Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva amesema kamati tendaji ya Simba iliamuru fedha za kumuuza Okwi zitumike katika ujenzi wa Kiwanja cha Bunju huku USD 17,000 alipwe aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili Zachariah Hans Pope alizokuwa akiidai klabu hiyo.
Aveva ameyasema hayo leo Juni 29,2021 wakati akitoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba dhidi ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili yeye na wenzake wawili.
Akiongozwa na wakili wa utetezi, Kung'he Wabeya, Aveva amedai kati ya mwaka 2014 hadi 2017 alikuwa rais kwa klabu ya Simba ambapo katika kipindi hicho Klabu ya Simba ilipata USD 319,212 zilizotokana na mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi kwenda klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
Amedai, baada ya kupokelewa kwa fedha hizo, yeye kama Rais aliitisha kikao cha kamati tendaji ili kuchanganua matumizi ya fedha hizo ndipo kamati Tendaji ikaamua fedha hizo zitumike katika ujenzi wa Kiwanja cha mpira cha Club hiyo kilichopo Bunju, na USD 17,000 alipwe aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili Zachariah Hans Pope alizokuwa akiidai klabu hiyo.
Amedai kamati Tendaji ilipendekeza fedha hizo ziwekwe katika akaunti maalum zoezi ambalo lilishindikana hivyo kamati ikamuomba aweke fedha hizo kwenye akaunti yake binafsi.
"Nilikubaliana na ombi hilo lakini nilitoa sharti kwamba lazima kuandaliwe mkataba wa makubaliano juu ya fedha hizo na maamuzi yake, jambo ambalo lilikubaliwa na mkataba uliandaliwa na kusainiwa na watu watatu ambao ni mimi rais wa klabu, makamu wa rais Geofley Nyange (Kaburu) na Katibu Mkuu ambaye pia alikuwa Mhasibu wa klabu Amos Gaumeni" amedai Aveva.
Baada ya kuandaliwa kwa mkataba huo zoezi la kuhamisha fedha hizo kwenda kwenye akaunti yake ya CRDB lilianza. Amedai kuwa pia, alihusika kwenda benki kusaini fomu ya kuhamisha fedha hizo huku Gaumeni akikamilisha taratibu za kibenki kuhamisha fedha hizo.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Julai 12 mwaka huu.
Mbali na Aveva washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Geoffrey Nyange 'Kaburu' na Hans Poppe ambapo wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, kutoa nyaraka za uongo, na kutoa maelezo ya uongo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...