******************************

Na Albano Midelo

KUMEKUWA na muingiliano mkubwa kati ya binadamu na wanyamapori hasa wanyama aina ya tembo wamekuwa wanaingia katika makazi ya watu na kuleta madhara ikiwemo kusababisha vifo.

Pori la Akiba la Selous ambalo hivi sasa linafahamika kama Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,ni moja ya maeneo ambayo yanatajwa kuongezeka kwa idadi kubwa ya tembo ambao wamekuwa wanaripotiwa kuleta madhara kwa watu.

Wilaya za Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma ni miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wanaathirika na tembo kwa sababu maeneo katika wilaya hizo, yamepitiwa na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere pamoja na ushoroba wa wanyamapori wa Selous-Niassa.

Ni ukweli usiopingika kuwa  idadi ya watu hapa nchini imeongezeka ambapo ongezeko hilo linakwenda sanjari na ongezeko la shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji,uchimbaji wa madini na shughuli nyinginezo ambazo zinaathiri uhifadhi endelevu.

Mkuu wa Chuo Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii (CBCTC) kilichopo Likuyu wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma Mhifadhi Jane Nyau anasema hivi sasa kumekuwa na muingiliano mkubwa kati ya binadamu na wanyamapori hususan tembo kuingia kwenye makazi ya binadamu.

Hata hivyo anasema kiuhifadhi kuna dhana ambayo inasema kwamba wanyamapori wameongezeka,ambapo anasema ongezeko lake sio kubwa kama inavyodhaniwa na wengi na kwamba kiuhalisia,idadi ya watu imeongezeka zaidi na kusababisha ongezeko la shughuli za kibinadamu.

Mhifadhi huyo akizungumza kwenye mahafali ya kozi maalum ya uhifadhi  namba 17 ya mwaka 2021 ya askari wanyamapori wa vijiji  106,anasisitiza kuwa ongezeko kubwa la watu linasababisha kuharibu makazi ya wanyamapori,ushoroba wa wanyamapori, kuharibu maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori na vyanzo vya maji.

“Ongezeko la binadamu ni changamoto kubwa kwa sasa katika uhifadhi,katika kukabiliana na changamoto hii,serikali imeandaa mpango mkakati wa namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ili kuwa na uhifadhi endelevu’’,anasisitiza Mhifadhi Nyau.

Anabainisha zaidi kuwa mpango mkakati huo tayari ulishazinduliwa na umeanza kutekelezwa na chuo cha CBCTC Likuyu Namtumbo ambacho ni chuo cha serikali kilichopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kwamba chuo hicho kinawajibika kutekeleza mpango mkakati huo ili kuhakikisha kwamba uhifadhi unaendelea,wananchi wanakuwa salama na wanaishi na wanyama kama rafiki kwenye mazingira yao.

Anaitaja mkakati mbinu mojawapo ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kuwa ni kutoa mafunzo maalum kwa askari wanyamapori na wanajamii ili kuwajengea uwezo wananchi wanaoishi  kando kando ya hifadhi ikiwemo hifadhi.

Anasisitiza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wananchi kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho na kuwa na mahusiano rafiki na wanyamapori.

Katika kutekeleza mpango mkakati huo,Mkuu wa Chuo cha CBCTC anasema chuo kinaendesha mafunzo maalum kwa askari wanyamapori wa vijiji  (VGS),kuwafundisha mbinu maalum za kukabiliana na wanyamapori waharibifu na wakali.

Akizungumzia mafunzo maalum ya uhifadhi ambayo yamefanyika kuanzia Mei 12,2021 na kukamilika Juni 12 mwaka huu,Mkuu wa Chuo anasema jumla ya wanafunzi 110 kati yao wanaume 103 na wanawake saba walishiriki mafunzo hayo ambapo walioweza kumudu kumaliza mafunzo na kutunukiwa vyeti ni wahitimu 106.

Anawataja wanafunzi waliopata mafunzo hayo,kuwa wanafunzi kumi wanatoka katika hifadhi ya msitu katika kijiji cha Engoserosambu wilayani Ngorongoro mkoani Manyara na washiriki 100 wanatoka hifadhi  za Jumuiya za Mbarang’andu, Kimbanda na Kisungule wilayani Namtumbo na Jumuiya za Chingolo na Nalika wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Sophia Kizigo ambaye amewakilishwa na Alikwini Ndimbo  anatoa rai kwa wahitimu kutambua kuwa kazi ya uhifadhi ni ya kizalendo,kiuadilifu na uaminifu kwa maslahi ya Taifa.

Kizigo anasisitiza kuwa askari wanyamapori wakiwa wazalendo watazilinda tunu za taifa,kuondoa ujangili dhidi ya wanyamapori na kuacha maslahi binafsi.

“Ninyi askari wa wanyamapori mliohitimu,mafunzo maalum ya uhifadhi,mnakwenda kuwa walinzi wa maliasili zetu,huko kuna wanyama,miti,misitu,madini,mheshimu kiapo chenu,acheni tamaa na maslahi binafsi bali wekeni mbele maslahi ya Taifa’’,anasisitiza Mkuu wa Wilaya.

Anatoa rai kwa askari hao katika maeneo yao kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo yao ili wanyamapori wasionekane kuwa adui kwa binadamu kwa kuwa wamejifunza mbinu bora za kuishi na wanyamapori.

Akisoma risala ya wahitimu wa kozi hiyo,mmoja wa wahitimu Masoud Nyoni anabainisha kuwa wamefanikiwa kupata elimu sahihi ya uhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili vijijini kwa maendeleo endelevu.

“Elimu hii imegusa Nyanja mbalimbali za uhifadhi wa maliasili kupitia masomo ya sheria za uhifadhi,utambuzi wa wanyamapori,matumizi ya silaha katika uhifadhi, uhifadhi wa misitu,matumizi ya GPS na ramani na maadili katika uhifadhi’’,anasema Nyoni.

Mafunzo mengine waliojifunza anayataja kuwa ni huduma ya kwanza,ukakamavu,haki za binadamu,mbinu za doria, intelijensia, upelelezi,upekuzi na ukamataji,ujanja wa porini,udhibiti wa eneo la tukio, utunzaji wa vielezo, taratibu za kimahakamani na utoaji ushahidi.

Hakuna ubishi jukumu la uhifadhi wa maliasili ni la jamii nzima,kwa sababu sekta ya maliasili na utalii ina mchango mkubwa katika pato la Taifa kupitia utalii wa wanyamapori,utalii wa picha na utalii wa uwindaji hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika sekta ya utalii nchini.

Imeandikwa na Albano Midelo

Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

Juni 16,2021

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...