MASHINDANO maalumu ya mpira wa Netiboli yanayolenga kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan yamezinduliwa leo jijini Dar es Salaam kwa timu nne kati ya 25 kutimua vumbi katika viwanja vya shule ya Msingi viziwi Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kuzindua mashindano hayo diwani ya kata ya Buguruni Busolo Pazi amesema, mashindano hayo yamelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan vilevile yamelenga kukuza na kuinua vipaji kwa mchezo huo wa Netiboli katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Pazi amesema, kupitia mashindano hayo wachezaji watadumisha ushirikiano pamoja kushirikishana fursa mbalimbali kwa kuwa michezo ni ajira.
Akizungumza kwa niaba ya taasisi ya Furahika Education College David Msuya amesema timu 25 za Netiboli kutoka Mkoa wa Dar es Salaam zenye kuhamasisha uzalendo zimeshiriki mashindano hayo yatakayofanyika kwa siku 5.
Amesema kuwa taasisi hiyo imeendelea kuiunga mkono serikali kupitia sera ya elimu na michezo mashuleni na kupitia mashindano hayo washindi watapata nafasi ya kujishindia fedha taslimu na vikombe vya ushindi.
Kwa upande wake katibu wa Chama cha Netiboli Dar es Salaam (CHANEDA,) Joseph Stanslaus amesema mashindano hayo yamehusisha timu za kada mbalimbali ikiwemo afya, jeshi na magereza ambako ni chimbuko la mchezo huo.
Pia amewataka wadau kujitokeza kudhamini mchezo huo wa Netiboli kwa kuwekeza katika vifaa vya michezo na viwanja vya michezo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...