Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema iko tayari kushirikiana na wadau wa maendeleo zikiwemo Taasisi za kifedha ili iweze kutoa maelekezo kwenye Ofisi za Wilaya na Mikoa kwa ajili ya kuwakutanisha na makundi yote ya Vijana, Wanawake, Walemavu waweze kunufaika.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira, Patrobas Katambi wakati akizindua msimu wa pili wa kampeni ya Benki ya CRDB inayoitwa 'Tupo Mtaani kwako'.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Naibu Waziri Katambi ametoa wito kwa Benki ya CRDB kushirikisha Serikali na hasa kupitia Wizara yake ili kuweza kuwakutanisha wananchi na Benki ili kunufaisha pande zote mbili.
Katambi amesema Serikali itaendelea kusukuma sera na sheria na wajibu ilionao ni kuhakikisha Mabenki yote nchini yanashusha riba katika mikopo huku akipoongeza CRDB kwa kufanya hivyo.
" Niwapongeze Sana CRDB mmekua mkishusha riba zenu za mikopo na mmefanya hivyo, huko ni kuwasaidia wananchi hawa na hasa wenye vipato vya chini kujitokeza kwa wingi kukopa na kufanya Biashara ambazo zitanyanyua vipato vyao.
Athari ya kutokutunza fedha wakati mwingine tuna kasumba ambazo tunazikumbatia wenyewe Mwenyenzi Mungu ametupa fursa nyingi na mabenki mengi lakini sisi hatutaki kuzitumia unapata 100,000 leo kwa dharura unataka kuitumia yote tunza kidogo weka basi hata 50,000 halafu nyingine teketeza hatuna utaratibu wa kutunza fedha,hivyo nitoe rai pia tuwe na utaratibu wa kutunza fedha," Amesema Katambi.
Akizungumzia kampeni hiyo, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kati,Chabu Mishwaro amesema kampeni ya Tupo Mtaani kwako mwaka jana ilikuwa na mafanikio kwani waliweza kutembelea mikoa 20 na kuwafikia watanzania zaidi ya 100,000.
Chabu amesema msimu wa pili wa kampeni ya 'Tupo Mtaani kwako' unalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za benki pamoja na kuwaunganisha watanzania walio wengi kutumia huduma za Benki ili kuchochea kasi ya maendeleo.
"Tumeenda katika Halmashauri tunatoa fedha kule kama umechukua mkopo nenda CDRD watakusaidia pia wanaweza kukopesha kwa kukuongezea ili ufanye biashara kubwa zaidi pia wamekuwa wakikopesha makundi mbalimbali ya wajasiriamali," Amesema Chabu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...