MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma(PSSSF) pamoja na Benki ya Azania wameingia makubaliano yatakayowezesha wanachama wa mfuko huo na wananchi wengine kukopa kwenye benki hiyo kwa kupata riba nafuu.


Akizungumza leo Juni 21,2021 mkoani Dar es Salaam,Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Hosea Kashimba amesema taasisi hizo zina dhima ya kuhakikisha wanaendana na azma ya Serikali ya kutekeleza kwa vitendo malengo yaliyomo kwenye dira ya Taifa ya 2025.

Na vipaumbele vya Ilani ya CCM inayohimiza kupatikana kwa huduma bora za afya, elimu , maji,makazi na umeme mijini na vijijini ambapo lengo lake kuu ni kustawisha maisha ya kila mtanzania.

"Ikumbukwe PSSSF kupitia jukumu lake la kisheria la uwekezaji umeendelea kutekeleza miradi ya kuuza nyumba za gharama nafuu pamoja na viwanja vya makazi.Madhumuni ya miradi hii ni kuwezesha wafanyakazi ambao ni wanachama wa mfuko na watanzania kwa ujumla kupata makazi bora na salama.

"Kwa kununua nyumba na viwanja vilivyopima kwa kulipia kwa njia rafiki ikiwemo mikopo ya makazi , aidha mradi wa nyumba za gharama nafuu upo katika Mkoa wa Dar es Salaam , Morogoro, Shinyanga, Tabora ,Mtwara na Iringa.

"Pia mradi wa viwanja vya gharama nafuu upo mikoa ya Ruvuma ,Kagera, Tabora Iringa,Katavi Morogoro ,Dar es Salaam, Kigamboni kule Kimbiji ,Rukwa, Lindi na Mtwara."amesema.

Hivyo ametumia nafasi hiyo kuwashukuru benki ya Azania akiwemo Mkurugenzi Mtendaji na timu yake kwa kuwa wa kwanza kuonesha utayari wa kushirikiana nao kukubali kutoa mikopo hiyo yenye riba na masharti nafuu.

Ameongeza kwa kufanya hivyo wanatekeleza azma ya Serikali ya kuongeza idadi ya wafaidika wa mikopo kwa ajili ya makazi bila mzigo wa riba kwa kuendelea kushusha viwango vya riba hadi kufikia kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka ambacho ni kiwango nafuu.

"Miongoni mwa maeneo yaliyoonesha mafanikio katika dira ya uwekezaji ya mwaka 2025 na Ilani ya CCM ni kuendelea kushusha kwa riba iliyokuwepo ya kati ya asilimia 21 hadi asilimia 25 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 13 na 18 mwaka 2020.

PSSSF na Benki ya Azania tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha azma hii inatekelezwa kwa vitendo,kupitia makubaliano haya wananchi watafaidika kwa kukopesha nyumba na viwanja,hivyo kuimarisha na kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi walioko maeneo yote nchini ili wawe na makazi bora na kutimiza kauli mbiu ya Serikali nyumba bora kwa wananchi wote inawezekana.

"Makubaliano haya yatamuwezesha mkopaji kulipa mkopo wake taratibu huku akiendelea kutimiza majukumu mengine ya kimaisha.PSSSF na Benki ya Azania tumeenda hatua zaidi kwa kuhakikisha tunawalinda wakopaji dhidi ya majanga kama vile moto , mafuriko, kimbunga na majanga mengine ya kibima wakati wote wa mkopo ili kulinda thamani ya uwekezaji ambao umefanywa,"amefafanua.

Kashimba amesema benki ya Azania imeshaandaa utaratibu wa kibima ili kuwalinda wakopaji dhidi ya majanga hayo na kwamba mteja atakapokamilisha mkopo wake atakabidhiwa hati yake ya nyumba na benki ya Azania.

"Muda wa marejesho ya mkopo huu ni kipindi kisichozidi miaka 15 kwa mkopo wa nyumba na miaka miwili kwa mkopo wa kiwanja .Masharti mengine ya msingi kwa mkopaji ni kuweka asilimia 10 ya thamani ya mkopo au mali yenye thamani hiyo kwa dhamana ya mkopo.

"Kiwango cha juu kabisa ambacho mteja anaweza kukopeshwa ni asilimia 90 ya thamani yote ya nyumba au kiwanja.Aidha taratibu zote na maelekezo ya masharti na vigezo vingine vya mkopo utakavyopatikana vitatolewa kwa wakopaji pindi watakapofika kwenye ofisi za PSSSF na Benki ya Azania,"amesema.

Aidha jumla ya nyumba 192 na viwanja 886 vyenye hati vitakuwa sokoni na vitauzwa kwa njia ya mkopo wenye riba nafuu utakaotolewa kwa wanachama na wananchi wote kwa kutegemea vigezo na masharti mepesi yaliyowekwa.

Amesema utaratibu wa kuviona, na kutoa mikopo utaratibiwa kupitia ushirikiano kati ya PSSSF na benki ya Azania pamoja na benki nyingine zitajitokeza baadae kwa kuzingatia idadi ya nyumba na viwanja.

"Mikoa ambayo nyumba za miradi zipo ni Dar es Salaam eneo la Chanika Buyuni, ambalo lina nyumba 106.Morogoro eneo la Lukobe nyumba moja, Tabora eneo la Usule kuna nyumba 25 ,Mtwara eneo la Mang'amba nyumba sita ,Shinyanga eneo la Ibadakuli nyumba 46, na Iringa eneo la Mawelewele kuna nyumba nane.

"Aidha nyumba ziko za aina nne zenye ukubwa tofauti kuanzia nyumba za vyumba viwili hadi vyumba vinne , bei ya nyumba ni kati ya Sh.milioni 36 hadi Sh.milioni 61 kulinagana na aina na ukubwa wa nyumba husika.

"Bei hizi zimejumuisha kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT .Makubaliano haya na benki ya Azania ni pamoja na uuzaji wa viwanja kwa njia ya mkopo ambapo vinapatikana mikoa ya Ruvuma viwanja 128.

"Kagera viwanja 192,Tabora kiwanja kimoja ,Iringa viwanja vinne, Katavi viwanja 50, Morogoro kiwanja kimoja ,Singida viwanja 211, Dar es Salaam eneo la Kigamboni kule Kimbiji viwanja 87,Rukwa viwanja 54,Lindi viwanja 70 na Mtwara viwanja 70"amesema.

Amesisitiza viwanja hivyo vina hati na vina ukubwa kati ya mita za mraba 450 hadi mita za mraba 1500 na vinapatikana kwa kati ya Sh.2500 hadi Sh.15000 za mita za mraba.Hata hivyo mfuko huo bado una uhuru wa kuuza kwa muuzaji mwingine.

Pia PSSSF itaendelea kuandaa mipango kama hiyo ya kuwapatia wanachama wake fursa ya kumiliki makazi yao pindi wakiwa bado kwenye ajira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Azania, Bw. Charles Itembe...amesema benki yao inaona faraja kuwa sehemu ya mradi huo mkubwa na kwamba benki hiyo ilikuwa ya kwanza na kinara wa ukopeshaji wa nyumba kwa riba nafuu.

"Kwa hiyo ni jambo ambalo tunauozoefu nalo kwa miaka mingi sana,tulikuwa ni benki ya kwanza kabisa kutoa mikopo ya nyumba toka miaka 2005 na mwaka 2016 wakati benki nyingine zikiwa bado hazijaanza kufanya kazi hiyo.

"Ukiangalia benki hii kwa kiasi kikubwa huduma ya mikopo ya nyumba imechukua asilimia kubwa, hivyo kwetu hili si jambo la kwenda kuiga bali tumeshalifanya na wengi wamefaidika hasa wafanyakazi wa sekta ya umma ukiondoa wa sekta binafsi.

"Na jambo hili kimsingi limetujengea heshima kubwa mtaani, ukisikia watu wengi wana nyumba za kuishi watakwambia ni kwasababu ya benki ya Azania, hivyo watanzania wanaokwenda kuomba mikopo ya nyumba au viwanja, basi benki hiyo iko tayari kuwahudumia, na mikopo hiyo inatolewa kwa riba ya asilimia 10.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bw. Hosea Kashimba (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Azania, Bw. Charles Itembe wakibadilishana nyaraka za makubaliano yatakayowawezesha wananchama wa PSSSF na wananchi wengine kukopa fedha kwenye Benki ya AZANIA kununua nyumba za gharama nafuu na viwanja zilizojengwa na Mfuko sehemu mbalimbali nchini.Wanaoshuhudia pichani kulai ni Mkurugenzi wa Mipango PSSSF Fortunatus Magambo na kushoto ni Meneja Mwandamizi wa Wateja Binafsi Jackson Lolai 


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bw. Hosea Kashimba (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Azania, Bw. Charles Itembe wakiwaonesha Waanishi wa Habari (hawapo pichani) nyaraka za makubaliano yatakayowawezesha wananchama wa PSSSF na wananchi wengine kukopa fedha kwenye Benki ya AZANIA kununua nyumba za gharama nafuu na viwanja zilizojengwa na Mfuko sehemu mbalimbali nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bw. Hosea Kashimba (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Azania, Bw. Charles Itembe wakisaini makubaliano yatakayowawezesha wananchama wa PSSSF na wananchi wengine kukopa fedha kwenye Benki ya AZANIA kununua nyumba za gharama nafuu na viwanja zilizojengwa na Mfuko sehemu mbalimbali nchini.


Picha ya pamoja

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...