Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika mahakama ya hakimu Mkazi Arusha.
Sabaya na wenzake wakitoka mahakamani mara baada ya shauri lao kuahirishwa.
Magari yaliyotumika kuwabeba Sabaya na wenzake kuwapeleka mahabusu katika gereza la Kisongo.
Baadhi ya wananchi wakiwa nje ya Mahakama ya hakimu mkazi Arusha.
Lengai Sabaya (wa nne kushoto,) akiwa na washtakiwa wenzake wakisubiri shauri lao kutajwa.

Na Grace Macha - Arusha

ALIYEKUWA Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, (34), amefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka sita tofauti, yakiwemo manne ya uhujumu uchumi na mawili ya unyang'anyi wa kutumia silaha kwenye kesi mbili tofauti.

Sabaya na wenzake wamefikishwa mahakamani leo pamoja na washitakiwa wenzake watano chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo wamerejeshwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo kwani mashitaka yanayowakabili hayana dhamana.

Umati mkubwa wa watu umejitokeza mahakamani hapo mara baada ya kusambaa kwa taarifa za Sabaya kufikishwa mahakamani hapo ambapo wananchi hao walikaa nje ya mahakama hiyo kuanzia majira ya asubuhi ambapo walizidi kuongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda.

Wananchi hao walionekana kushangilia wakati magari yaliyokuwa yamewabeba Sabaya na washitakiwa wenzake yakitoka kwa kasi mahakamani hapo kwa ajili ya kuwapeleka mahabusu kwenye gereza la Kisongo.

Washitakiwa wengine ni pamoja na msaidizi binafsi wa DC Sabaya, Sylivester Nyengu, (26) maarufu kama Kicheche, Enock Mnekeni, (41), Watson Mwahomange, (27) maarufu kama Maliamungu, John Aweyo maarufu kama Mike one na Daniel Mbura, (38).

Upande wa Jamhuri kwenye mashauri hayo,  uliongozwa na  Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Tumaini Kweka, Mawakili wa serikali wakuu waandamizi, Abdallah Chavula na Tarsila Gervas.

Katika shauri la uhujumu uchumi namba 27/2021 Ole Sabaya anakabiliwa na mashitaka manne huku wenzake wanne wakikabiliwa na mashitaka mawili.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mashitaka, Kweka aliieleza mahakama hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, Martha Mahumbuga kuwa, katika shitaka la kwanza  Ole Sabaya anadaiwa kuongoza genge la uhalifu kiyume cha sheria akishirikiana na washitakiwa wengine ambao si watumishi wa umma 

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo Januari 20, mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha Sabaya akiwa ni ofisa wa umma, mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro alikiuka majukumu yake ya kiofisi kwa pamoja akishirikiana na Mnikeni, Mwahomange, Aweyo na Nyengu.

"Kwa kujua na kwa malengo ambayo si halali, kwa kutumia mamlaka yake kama afisa wa umma huyu mshitakiwa wa kwanza walijipatia manufaa ambayo ni kinyume cha sheria," Kweka ameieleza mahakama hiyo.

Shitaka la pili na tatu yanamkabili Sabaya peke yake ambapo anadaiwa kushiriki matukio ya rushwa ambapo mnamo Januari 20, mwaka huu katika maeneo ya jiji la  Arusha alishiriki vitendo vya rushwa kwa kumshawishi Francis Mrosso ampatie fedha kiasi cha shilingi milioni 90 kwa kumuahidi kwamba atamsaidia kuweza kuepuka vitendo vya jinai vilivyokuwa vinamkabili ambavyo vilikuwa ni vya ukwepaji wa kodi.

Kweka aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa katika shitaka la tatu Sabaya anadaiwa kuwa mnamo Januari 20, mwaka huu kwenye maeneo ya Mrombo jijini Arusha alipokea rushwa ya kiasi cha shilingi milioni 90 kutoka kwa Mrosso kwa maelezo kuwa angemsaidia kukwepa vitendo vya kijinai alivyodaiwa kukabiliwa navyo vya ukwepaji kodi.

 Katika shitaka la nne  linalowakabili washitakiwa wote watano ni la utakatishaji wa fedha haramu ambapo Ole Sabaya akishirikiana na Mnikeni, Mwahomange, Aweyo na Nyengu wanadaiwa mnamo, Januari 20, mwaka huu huko maeneo ya Kwamorombo, Jijini Arusha walijipatia kiasi cha shilingi milioni 90 wakati wakijua kuwa kujipatia fedha hizo ambazo ni mazalia ya uhalifu ilikuwa ni mwendelezo wa kosa la vitendo vya rushwa.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina nguvu kisheria kusikiliza shauri hilo ambapo upande wa jamhuri uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo kwani upalelezi bado haujakamilika.

KESI YA UNYANG'ANYI WA KUTUMIA SILAHA

 Katika kesi ya jinai namba 66 la unyang'anyi wa kutumia silaha linalomkabili Sabaya pamoja na washitakiwa wengine wawili akiwemo Sylvester Nyengu na Daniel Mbura.

Wakili mkuu mwandamizi wa serikali, Tarsila amewasomea washitakiwa hao mashitaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama ya hakimu mkazi Arusha, Salome Mshasha.

Katika shitaka la kwanza washitakiwa wote wanashitakiwa kwa unyang'anyi kwa kutumia silaha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa Februari 9, mwaka huu katika mtaa wa Bondeni jijini Arusha wote kwa pamoja waliiba kiasi cha shilingi 390,000 mali ya Bakari Rahibu Msangi.

"Na baada ya wizi huo walimfunga na pingu, wakampiga makofi, wakampiga mateke, wakampiga ngumi na wakatumia silaha ambayo ilikuwa ni bunduki kumtisha ili wabaki na fedha ambazo walizichukua kutoka kwake,".

Tarsila aliwasomea shitaka la pili la unyang'anyi wa kutumia silaha ambapo ilidaiwa washitakiwa hao wote mnamo Februari 9, mwaka huu kwenye mtaa wa Bondeni jijini Arusha wote kwa umoja wao waliiba simu moja aina ya Tecno na fedha 35,000 mali ya Ramadhani Ayoub Rashid 

"Baada ya wizi huo walimpiga kwa makofi, ngumi, mateke na wakatumia silaha kumtisha ili waweze kubaki na mali ambazo walimuibia," wakili huyo mkuu mwandamizi wa serikali aliieleza mahakama.

Washitakiwa wote watatu walikana mashitaka ambapo kesi hiyo haina dhamana hivyo walipelekwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo.

Mashauri yote mawili yatarudi mahakamani hapo Juni 18, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...