Serikali imesisitiza kuendelea kuipa kipaumbele michezo mbalimbali inayofanya vizuri Kimataifa kwani imekuwa ni sehemu ya Kuitangaza nchi, kuibua vipaji pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul leo tarehe 21 Juni, 2021 alipoitembelea kambi ya timu ya Taifa ya mchezo wa Kabaddi katika shule ya Sekondari Nguva wilayani Kigamboni Jijini Dar es Salaam, ambapo pia amewapongeza wadhamini waliojitokeza kudhamini Kambi hiyo huku akiwasihii viongozi wa Kabaddi kushirikisha sekta nyingine kama vile Utalii kwa ajili ya kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo nchini katika mashindano hayo.

"Niombe pia mjaribu kuzishirikisha Sekta nyingine katika fursa hii muhimu, mfano ndugu zetu wa Utalii, wanaweza kutumia fursa iliyopo kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo nchini kwa mataifa ambayo yanakuja kushiriki mashindano haya," amesema Mhe. Pauline.

Aidha Mhe.Pauline amewataka wachezaji waliopo kambini kufanya mazoezi kwa bidii ili kulibakisha kombe la Afrika nyumbani kama mwenyeji wa mashindano ya mchezo wa kabaddi Afrika yanayotarajiwa kuanza tarehe 29 Juni hadi 5 Julai, 2021katika Ukumbi wa Ubungo Plaza Jijini Dar es salaam.

"Itakuwa vizuri kama tutajituma mazoezini ili tuweze kuchukua ubingwa kwa mchezo huu sisi kama wenyeji,  itakuwa ni aibu sana kama tutatolewa mapema kama wenyeji, hivyo tukapambane ili tuweze kuliwakilisha vyema Taifa letu," amesema Mhe. Pauline.

Mashindano ya Afrika ya mchezo wa Kabaddi kwa mwaka 2021yatakayofanyika hapa nchini yanatarajia kushirikisha nchi sita za Tanzania, Kenya, Mauritius,Misri, Cameroon na Zimbambwe ambapo wageni kutoka katika nchi zaidi ya 20 za Afrika wanatarijiwa kuwasili hapa nchini kwa ajili ya kuratibu na kushuhudia mashindano hayo.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...