1. Hii ni kende malamu, kwa heri baba Kaunda,
Kwa kweli umehitimu, hongera baba Kaunda,
Umeacha ya muhimu, ya kukumbuka Kaunda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika

2. Ametuachia suti, huyu Kenneth Kaunda,
Tuvae Kaunda suti, tukukumbuke Kaunda,
Kiongozi madhubuti, tutakuenzi Kaunda,
Pole Wazambia wote, polebara Afrika.

3. Maisha yake tamati, tunalia amekwenda,
Katika ile Kamati, Ukombozi alipenda,
Ilikuwa ni mtiti, hatimaye walishinda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

4. Jua Rais wa Kwanza, wa Zambia ni Kaunda,
Yeye ndiye alianza, nchi hiyo kuiunda,
Kasi hakuipunguza, ukombozi alipenda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

5. Waliungana pamoja, Nyerere naye Kaunda,
Mawazo yao pamoja, wakoloni kuwaponda,
Wala si kwa neno moja, na silaha walipenda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

6. Kamati ya Ukombozi, kusini waliiunda,
Kweli walichapa kazi, kunyosha waliopinda,
Uhuru si uchokozi, Afrika walipenda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

7. Walifanya kwetu sote, uzalendo kuupenda,
Hadi tuwe huru sote, wazalendo wakashinda,
Na kwa jitihada zote, mwisho wake walishinda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

8. Nyerere, Seretse Khama, pamoja naye Kaunda,
Kidete walisimama, wakoloni kuwaponda,
Maputo ikasimama, na Angola wakashinda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

9. Samora na yule Neto, ukombozi wakapenda,
Namibia moto moto, baadae wakashinda,
Sauzi kukawa joto, na Mandela akashinda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

10. Mugabe sijamtaja, limfaidi Kaunda,
Alikuwa ni mteja, Smith akimponda,
Akawa naye mmoja, Kamati iliyoshinda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

11. Nujoma wa Namibia, limfaidi Kaunda,
Alivyowapigania, hadi mwisho wakashinda,
Na yeye alichangia, Sauzi hadi kushinda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

12. Wale hamumfahamu, huyu Kenneth Kaunda,
Hili bora mfahamu, najua mtalipenda,
Akili zake timamu, usawa aliupenda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

13. Toka sitini na nne, alitawala Kaunda,
Tisina moja si nne, upinzani ukashinda,
Rais hebu muone, akapisha aloshinda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

14. Afrika kiongozi, kama Kenneth Kaunda,
Kuachia uongozi, bila figisu kupenda,
Kuwapata ipo kazi, siyo hivyo kwa Kaunda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

15. Katika kizazi chake, alibakia Kaunda,
Lishaondoka wenzake, sasa naye amekwenda,
Takutana na wenzake, hatujui nakokwenda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

16. Hii Reli ya TAZARA ni Nyerere na Kaunda,
Bomba la Mafuta sura, ni Nyerere na Kaunda,
Waliiva barabara, Nyerere naye Kaunda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

17. Sasa waasisi wetu, Nyerere naye Kaunda,
Kwa sasa hawako kwetu, kwingine wameshaenda,
Tukumbuke wanakwetu, kwa vile tuliwapenda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

18. Siyo muda wa kulia, kwa kuondoka Kaunda,
Muda wa kushangilia, mazuri aliyotenda,
Na tena kushikilia, kuenzi aliyotenda,
Pole Wazambia wote, pole bara Afrika.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...