KATIKA kuunga mkono kampeni ya uchangiaji wa matibabu kwa watoto wenye matatizo ya vibiongo, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), limetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto hao pamoja na wengine waliolazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Pia STAMICO imetoa kiasi cha Sh milioni tatu kuchangia matibabu ya watoto zaidi ya 40 wanaosubiri matibabu ya tatizo la vibiongo.
Akikabidhi msaada huo leo Juni 25, 2021 jijini Dar kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Stamico, Deusidedit Magala alisema wameamua kuungana na majirani wenzao yaani Moi kuhitimisha wiki ya utumishi wa umma kwa kutoa msaada huo.
“Kwa kile tunachokipata tumeamua sehemu yake tujitolee kwa ajili ya kuwasaidia watoto hasa wanaotarajiwa kufanyiwa operesheni za kibiongo kwa hiyo tumekuja na vitu vya kuwagawia wagonjwa lakini pia katika hiyo kampeni tumechangia jumla ya Sh milioni tatu.
“Hii ni sehemu ya kuadhimisha utumishi wa umma ambapo wafanyakazi tunaungana kwa pamoja kuwaona wenzetu waliopo hapa Muhimbili,” alisema.
Aidha, akipokea msaada huo, Kaimu Mkurugenzi huduma za uuguzi taasisi ya mifupa Moi, Fidelis Lucas Minja aliishukuru Stamico kwa msaada waliowapatia ikiwamo kuunga mkono mbio za Marathoni ambazo zinalenga kukusanya zaidi ya Sh milioni 800 kwa ajili ya matibabu ya watoto hao wenye matatizo ya vibiongo.
“Wenzetu wanapohitimisha siku ya utumishi wa umma wameona ni vizuri kuchangia mbio za marathoni na kuwasaidia watoto wenye vibiongo na kuwaona wenye matatizo mbalimbali.
“Ni tendo la huruma kusaidia, hata sisi kama wauguzi na watumishi tunaweza kufanya lakini tunawaalika wengine kutoka taasisi mbalimbali na mashirika waje kuwasaidia watoto wenye shida kwani mahitaji ni mengi na serikali peke yake haiwezi. Hivyo kupitia taasisi hizi tunaweza kutimiza malengo ya nchi yetu“, alisema.
Alisema zaidi ya watoto 40 wenye shida ya vibiongo wanatarajiwa kutumia gharama zaidi ya Sh milioni 800 za matibabu ambapo motto mmoja pekee huhitaji zaidi ya Sh milioni 21.
“Watoto waliopo ni wengi, tunawaomba watu kutoka taasisi mbalimbali wachangie hasa kupitia marathoni hii itakayofanyika Jumapili Juni 27, mwaka huu.
“Kuna mbio ndefu za kati na awali yaani kilomita tano, 10 na 21. Vigezo hakuna isipokuwa unatakiwa kuchangia Sh 35,000 kiingilio ila ukichangia Sh 500,000 unatambulika kama mmoja wa wafadhili wa mpango huu“, alisema.
Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Madini -Stamico wakiwa ndani ya wodi ya watoto wenye matatizo mbalimbali katika Taasisi ya Mifupa Moi. Wafanyakazi hao walitembelea taasisi hiyo na kuwaona watoto wagonjwa waliolazwa katika wodi za taasisi hiyo na kuwagawia mahitaji mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...