Na Amiri Kilagalila,Njombe
Halmashauri
ya mji Njombe kwa kushirikiana na kampuni ya Lixil watengenezaji wa
vyoo aina ya “SATO” ,vya plastiki imetoa mafunzo kwa mafundi 60 wa kila
kijiji na mtaa,katika halmashauri hiyo ili kutimiza lengo la kuhakikisha
kuwa kila taasisi na kaya inakuwa na vyoo bora na salama.
Akizungumzia
lengo la mradi wa uboreshaji vyoo Meneja wa Kampuni ya Lixil Justine
Mbowe amesema kuwa wazo hilo lililotokana na jitihada za kuboresha
mazingira katika ngazi ya Kaya na Taasisi ambapo kwa mwaka 2018 Kampuni
hiyo ilitoa idadi ya vyoo elfu themanini kwa Serikali kupitia wizara ya
Afya kupitia kampeni mbalimbali za usafi ikiwemo kampeni ya nyumba ni
choo ili Wananchi wenye uhitaji na wa hali ya chini waweze kupata fursa
ya kuboresha vyoo vyao na kuwa na mazingira salama.
“Licha
ya kuwapatia elimu mafundi tumeona pia tutoe elimu hii katika Shule za
Msingi kwani tunaamini tabia huanza kujengwa toka mtoto anapokuwa mdogo.
Hii inamaana kuwa watoto watakapopata elimu hii ya matumizi ya vyoo
hivi kuanzia shuleni watakuwa ni mabalozi wazuri katika kaya zao. Kwa
upande wa wanafunzi wa Shule za Msingi tunaamini ni rahisi kwao
kuendeleza matumizi ya choo bora tangu wakiwa na umri mdogo.”Alisema
Mbowe
Kwa upande wake
Afisa Afya Halmashauri ya Mji Njombe Saimon Ngassa amesema kuwa
madhumuni ya ujenzi wa vyoo kwa kutumia masinki ya plastiki aina ya
“SATO” ni muendelezo wa Kampeni mbalimbali za uboreshaji wa Mazingira na
kwa sasa Halmashauri inaendelea na Kampeni ya uboreshaji wa vyoo katika
maeneo ya Taasisi na Kaya ambapo kwa sasa kampeni hiyo imelenga
kuboresha vyoo vya asili kwa kuviwekea masinki ya vyoo vya plastiki na
yanayoendana na mazingira halisi.
“Tumejifunza
kuwa vyoo hivi vinatumia maji kidogo na ufanisi wake ni mkubwa katika
kuzuia harufu na wadudu wanaoingia kwenye vyoo na kwenda kwenye makazi
jambo litakaloweza kupunguza maradhi kwa kiasi kikubwa lakini pia ni
vyoo vyenye gharama nafuu kwa Wananchi wenye kipato cha chini.”Alisema
Ngassa.
Aliendelea kusema
“Kampeni hiyo inatekelezwa kwa kuwajengea uwezo mafundi wa eneo husika
ambapo kila Kijiji kilitoa fundi mmoja kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ili
wawewatekelezaji katika kuboresha na kuwajengea vyoo bora Wananchi
ngazi ya kaya.”
Johnson
Joseph, Bisaya Musa Wanafunzi kutoka shule ya Msingi Kisilo kwa pamoja
wanasema kuwa changamoto iliyokuwepo katika vyoo vya mashimo ni uwepo wa
harufu kali na wadudu kutoka chooni kusambaa jambo ambalo limepatiwa
ufumbuzi kupitia vyoo vipya na wamesema kuwa vyoo hivyo vitasaidia
kwenye uthibiti wa magonjwa mbalimbali na atawashauri wazazi kuwa na
vyoo hivyo
Patrick
Mdetele Fundi kutoka Kijiji cha Utalingolo na Kutoka Rocks Mwalongo
kutoka Kijiji cha Idihani wamesema kuwa elimu hiyo inamanufaa makubwa
kwao hususani kwa Wananchi watakaowahudumia kwani gharama ni nafuu
ukilinganisha na masinki ya aina nyingine na uwepo wa mfuniko ni
mdhibiti tosha wa uchafuzi wa mazingira kwa njia ya hewa.
Mkoa
wa Njombe umepatiwa jumla ya vyoo 1630 ambapo mpaka sasa Shule za
Msingi 33 kutoka Halmashauri ya Mji Njombe zimeweza kujengewa vyoo vya
masinki ya “SATO” huku Wananchi wakihamasishwa kutumia teknolojia hiyo
na kwa wenye uhitaji waweze kuwasiliana na maafisa afya na watendaji wa
vijiji,mitaa na Kata husika ili kuweza kufungiwa vyoo hivyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...