Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MKUU wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba SC, Haji Manara amesema endapo Waamuzi wa mchezo wao dhidi ya Yanga SC watachezesha mchezo huo kwa kufuata Sheria na Kanuni za Soka, ameeleza Kikosi chao kitaondoka na ushindi wa mabao zaidi ya matatu kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara utakaopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa Julai 3, 2021.
Manara amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari, mkoani Dar es Salaam kuelekea kwenye kipute hicho siku ya Jumamosi Uwanja wa Mkapa, amesema ana amini Kikosi chao kuwa bora zaidi ya Kikosi cha Yanga SC msimu huu wa Mashindano.
“Sisi tuna Wachezaji wengi wenye ubora wa hali juu angalia tuna Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Bocco, Chama, Onyango, Wawa, Miquissone na wengine, Waamuzi wakichezesha kwa Sheria na Kanuni za Soka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa hatoki mtu siku hiyo”, ameeleza Manara
Pia amesema hadi sasa anaamini Kikosi cha Simba kitatangaza Ubingwa wake wa nne mfululizo kutokana na kubakisha alama nne pekee ili kutwaa taji hilo la Ligi Kuu ya Tanzania, “Sisi kuanzia Uongozi wa Klabu, Wanachama hadi Mashabiki tunahitaji furaha tu, hatutaki kitu kingine zaidi ya furaha wakati wote, tunaamini Ubingwa wa nne upo mikononi mwetu”, amesema.
Kuhusu Nyota wa Klabu hiyo, Luis Jose Miquissone, Manara amesema Mchezaji huyo bado ana mkataba na Wekundu hao na si sawa kumuhusisha na usajili katika Klabu nyingine kutokana na mkataba wake na Simba SC.
“Miquissone bado ana mkataba na sisi hizo tetesi za kumhusisha na timu nyingine si sahihi kabisa, kama kuna timu inamtaka Mchezaji huyo ije mezani tukae na walete Dola Milioni 10 tuone kama wanaweza kumsajili”, amesema
Aidha, amewapongeza Yanga SC kuingia rasmi kwenye mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa Klabu yao, amesema anaamini kwa Yanga kuingia kwenye mabadiliko hayo Soka la Tanzania litakuwa na kufika mbali ikiwemo katika masuala ya uendeshaji wa Klabu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...