WAHUDUMU 15 wa
kujitolea ngazi ya Jamii ambao
wamekuwa wanafanyakazi ya kuwasaidia watoto wa kaya masikini 423 mkoani Ruvuma
wamepewa msaada wa baiskeli ili kuwasaidia kutoa huduma kwa jamii.
Msaada huo umetolewa na
Shirika la Social Action Trust Fund(SATF) kwa udhamini wa mfuko wa dharura wa
Rais wa Marekani wa kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI(PEPFAR), kupitia
mfuko wa Balozi wa Marekani nchini Tanzania.
Akitoa taarifa kwa
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema katika hafla fupi
iliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Songea ,Mwakilishi
wa Mkurugenzi wa SATF Dkt.Sylivia Ruambo amesema jumla ya shilingi milioni 3.7
zimetumika kununua na kusafirisha baskeli hizo hadi Songea.
Dkt.Ruambo amebainisha
kuwa SATF inatekeleza mradi wa tuwalinde watoto katika Halmashauri tatu za Mkoa
wa Ruvuma ambazo amezitaja kuwa ni Madaba,Songea na Nyasa na kwamba mradi huo
ni wa mwaka mmoja.
“Mradi umelenga
kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupata huduma za
elimu,afya,ulinzi na haki za mtoto pamoja na kuziwezesha kaya masikini kujenga uwezo kiuchumi’’,alisisitiza
Dkt.Ruambo.
Hata hivyo
amesema,pamoja na shughuli nyingine,mradi huo uliwajengea uwezo wahudumu 15 wa
kujitolea katika ngazi ya Kata ambao wamekuwa wanasaidia kuielimisha jamii
kuhusu haki za mtoto na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Amesema,mradi umeamua
kuwanunulia basikeli wahudumu hao ili kuwarahisishia usafiri na kuwafikia
walengwa majumbani kwao.
Akizungumza baada ya
kuwakabidhi basikeli hizo,Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema
ametoa rai kwa wahudumu hao kuzitunza basikeli hizo na kuendelea kuwatumikia
walengwa kama mradi ulivyoelekeza.
“Natambua kazi yenu kwa
sehemu kubwa ni ya kujitolea,hivyo nawaomba mtangulize mbele maslahi ya jamii ili kuweza kutimiza
adhima ya kuwahudumia’’,alisisitiza Mgema.
Mgema amelishukuru
Shirika la SATF na PEPFAR kupitia ubalozi wa Marekani kwa kazi kubwa ambayo
wanaifanya mkoani Ruvuma ambako wanatekeleza mradi wa Tuwalinde ambao
unahudumia watoto 423.
Naye Mwakilishi wa
Balozi wa Marekani Jeremy Divis amesisitiza kuwa wapo tayari kuendelea
kushirikiana na serikali ya Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali yenye tija
kwa jamii ukiwemo mradi wa tuwalinde ambao unatekelezwa pia mkoani Ruvuma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...