Na Shukrani Kawogo, Njombe
IKIWA zimetimia siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwepo madarakani katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) wilayani Ludewa mkoani Njombe Bakari Mfaume amesema Rais huyo amejipambanua vyema na kuonyesha kuwa wanawake wanaweza.
Hayo ameyasema katika mkutano wa kazi wa baraza la umoja wa wanawake UWT wilayani humo na kuongeza kuwa wanawake wote nchini wanapaswa kumuunga mkono kwakuwa ameonyesha dhamira ya dhati ya kuwakomboa wanawake na watanzania wote kwa ujumla.
Amesema kwa juhudi hizo anazozifanya zinapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa nafasi zote za uongozi zilizo chini yake kwani endapo itafanywa kinyume na hapo watamfedhehesha Rais ambaye amejinasibisha kuwa wanawake wanaweza.
"Nchi yetu tangu ilipopata uhuru imekuwa na marais watano na wote wanaume na sasa tumempata Rais wa sita ambaye ni mwanamke, Rais huyu toka alipoingia madarakani amejipambanua kuwa ni mtu wa watu kwa kukutana na viongozi wa dini zote, wazee, kundi la wanawake ambalo linawakilisha sehemu kubwa ya watanzania katika maendeleo ya chama na nchi kwa ujumla", alisema Mfaume.
Sanjali na hilo pia aliwasilisha mchango wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga pamoja na mbunge wa viti maalum mkoa wa Njombe Balozi Dk. Pindi Chana ambao kwa pamoja wametoa kiasi cha shilingi milioni mbili na laki sita ambazo zimelenga kugawiwa katika kata zote 26 za Wilaya hiyo ili kukuza miradi mbalimbali iliyoanzishwa na UWT ngazi za kata.
Mfaume aliwaasa wanawake hao kuhakikisha linaimarisha miradi iliyopo ili iweze kuwasaidia kujitegemea katika masuala mbalimbali yanayowahusu badala ya kupeleka maombi ya uwezeshwaji kifedha kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ili wafanikishe shughuli zao.
Leah Mbilinyi ni mwenyekiti wa UWT wilayani humo aliwashukuru wabunge hao sambamba na kuwataka wanachama wake kuwa makini katika uendezwaji wa miradi iliyopo katika ngazi ya kata ili iweze kuwasaidia katika mahitaji mbalimbali ya kichama.
Aliongeza kuwa inapofanyika mikutano ngazi ya wilaya wanachama wamekuwa wakitarajia kulipwa nauli pamoja na posho kutoka kwa wahisani mbalimbali hivyo aliwataka viongozi wote wa ngazi ya kata kuikuza miradi hiyo ili iweze kuwawezesha kujitegemea wenyewe pasipo kutegemea wahisani.
"Hii miradi tunapoisimamia vyema itasaidia kuimega hata katika ngazi ya matawi hivyo wanawake wenzangu tuamkeni na tuimarishe miradi yetu kwani kwa kufanya hivyo itatuwezesha kusimama kwa miguu yetu wenyewe", alisema Bi. Mbilinyi.
Aidha kwa upande wa wanachama hao wa UWT wamekubaliana kusimamia vyema miradi hiyo sambamba na kuomba kupatiwa mikopo ya halmashauri ili iwasaidie kutanua wigo wa miradi hiyo ambayo ni ya kilimo, ufugaji, ufundi pamoja na mashine ya kusagia nafaka.
Katika kufanikisha suala hilo la mikopo mmoja wa wanachama hao ambaye pia ni diwani wa viti maalum tarafa ya mwambao Rainalda Tweve ameiomba ofisi ya maendeleo ya jamii kutoa elimu ya kutosha juu ya mikopo hiyo kwa watendaji kata na wananchi kwani kumekuwa na usumbufu mkubwa juu ya kuandika barua hizo za maombi ya mkopo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...