NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
WAAJIRI kutoka sekta ya Umma na Binafsi mkoani Morogoro wameelezwa kuwa moja ya majukumu yao ni kukuza mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama vifo vitokanavyo na kazi kwa kuzingatia sheria ya usalama na afya mahali pa kazi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidida kwa Wafanyakazi (WCF) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waajiri 165 wa mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini kutoka WCF Dkt. Abdulsalaam Omar alisema wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waajiri wa mkoa huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Juni 22, 2021.
“Mfuko huu umeundwa kwa dhumuni la kukidhi matakwa ya mikataba ya kimataifa kuhusu fidia kwa wafanyakazi ambapo kukuza mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama vifo ni moja ya matakwa hayo.” Alifafanua Dkt. Omar
Aliwaambia washiriki kuwa Mfuko umekuwa na faida kubwa kwa wafanyakazi, waajiri na taifa kwa ujumla kwani wafanyakazi wana uhakika wa kinga ya kipato kutokana na majanga yasababishwayo na ajali, magonjwa au vifo vitokanavyo na kazi.
“Hali kadhalika waajiri nao wanapata muda zaidi wa kushughulikia masuala ya uzalishaji na uendelevu wa biashara zao kwani mfuko ndio unaobeba jukumu la kugharamia pindi mfanyakazi anapoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi” alifafanua na kuongeza kuwa ‘Wafanyakazi nao wanapata utulivu kazini kutokana na kupungua kwa migogoro hasa pale ajali zinapotokea sehemu za kazi na hii inasaidia sana kuongeza tija na uzalishaji na kuchangia kuongeza pato la taifa.
Akiwasilisha mada kuhusu Usalama na Afya sehemu za kazi, Meneja Tathmini za Vihatarishi Sehemu za Kazi, Bi. Naanjela Msangi alisema ili kuzingatia sheria ya usalama na afya mahali pa kazi waajiri hawana budi kuweka mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa kuwapatia wafanyakazi vifaa vya kujikinga (Protective gears) na wahakikishe wanavitumia ipasavyo.
Ili kuonyesha madhara ya kufanya kazi bila ya kuvaa vifaa vya kujilinda, Bi. Naanjela aliongoza washiriki kufanya onyesho la kuonyesha madhara kwa wafanyakazi kutokana na ajali kazini.
Wakizunguzma kwa nyakati tofauti baada ya kupata mafunzo hayo, washiriki walisema yamekuwa ni yenye manufaa makubwa kwao na bila shaka watatumia elimu waliyoipata ili kuhakikisha wanatekeleza vema jukumu la kuweka mazingira salama kwa wafanyakazi mahali pa kazi.
"Tusiridhike na tusibweteke na Mfuko kwa kusema midhali WCF ipo basi masuala ya usalama na afya mahali pa kazi iwe sio kipaumbele chetu la, tusifanye hivyo, Fidia iwe ni kitu cha mwisho ije pale tu inapohitajika. ‘hakuna namna mtu akiumia au amepata ugonjwa basi aweze kupata fidia." Alisema Iddi Fuko, Meneja wa Usalama Mahali pa Kazi, Unitrans Tanzania Limited, Morogoro.
Alisema mafunzo hayo yasibaki kwa washiriki tu bali yaende hadi kwa maofisa na wafanyakazi wa ngazi za chini ili elimu hiyo iweze kuwasaidia wengi.
"Mafunzo haya yamenipa motisha mkubwa kwa kutambua usalama kazini, lakini pia tumefundishwa umuhimu wa kulinda viungo vyetu na hivyo yatupasa kuweka mazingira mazuri mahali pa kazi ili kupunguza ajali na magonjwa kazini." Alisema Dotto Ramadhani, kutoka Haki Hoteli Morogoro

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...