Na Zainab Nyamka, Michuzi TV
SHIRIKA la BRAC Tanzania limeendelea kutanua wigo wake kibiashara baada ya kuzindua tawi la lake Katika Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu.
BRAC limezindua tawi hilo kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha nchini Tanzania. Tawi hilo limezinduliwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Albert Lutaiwa akiwataka wananchi kujiunga na shirika la BRAC ili kuweza kupata huduma za mikopo.
Akizungumza katika hafla ndogo ya uzinduzi iliyofanyika katika tawi hilo lililopo katika mji wa Meatu, Albert Rutaiwa amesema, “Nawashukuru sana kwa kuweza kusogeza huduma katika wilaya yetu ya Meatu na hivyo kuahidi kuwapa ushirikiano kutoka kwetu utakaohitajika.'"
Amesema, "Ninaomba sana kuweza kuwapa taarifa muhimu wakina mama hawa wanaokuja kupata huduma za mikopo ili waweze kukopa wakiwa na taarifa kamili. Tunachotakiwa kufanya ni kuzingatia sheria ili kuweza kupata faida kutoka kwenye huduma zinazotolewa.”
Rutaiwa amesema, wakina mama wanaokuja kukopa waje kwa malengo ili kuweza kurejesha kwa wakati na pia kupata faida kutoka kwenye huduma ya mikopo ambayo leo imezinduliwa.
Amesema, Mkoani Simiyu BRAC ilianza operesheni mwaka 2016 katika wilaya za Maswa na Bariadi na hivyo kuongezeka kwa tawi la Meatu kunakuwa na jumla ya matawi matatu mkoani humo ambayo yanahudumia wakinamama zaidi ya elfu tatu kwa mikopo midogo midogo isiyo na dhamana kupitia njia ya vikundi.
Meneja wa Mkoa wa BRAC Elizabeth Okama, amesema kuwa lengo kuu la shirika hilo ni kunyanyua wanawake kiuchumi kupitia mikopo midogo midogo yenye masharti nafuu.
Okama amesema "BRAC inajivunia kuwa shirika lenye mtazamo wa kumnyanyua mwanamke kijamii na kiuchumi. Bidhaa yetu kuu ni mikopo isiyo na dhamana kwa sababu tunatambua changamoto za kinamama katika kupata huduma za kifedha hasa mikopo.''
Amesema, nia ya BRAC pia ni kuhakikisha tunafikisha huduma za kifedha katika maeneo ambayo huduma hizi hazipatikani kirahisi hasa katika miji midogo na vijijini.
Shirika la BRAC llimejikita kutoa huduma jumuishi za kifedha kwa njia ambayo ni rahisi, kupitia bidhaa zilizoundwa kukidhi mahitaji ya wateja wake.
BRAC inajivunia kuwa na matawi 155 ambayo yapo katika wilaya 83 kati ya mikoa nchini. BRAC na mshirika mkubwa kwa wanawake kwani asilimia 97 ya wateja wake nchini ni wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo, wakulima na wafugaji.
Pamoja na mkopo usio na dhamana kupitia vikundi vya kinamama, BRAC pia hutoa huduma za mikopo binafsi kwa wajasiriamali wa kati ulio wa dhamana kwa wateja wanawake na wanaume.
Dhamira ya BRAC ni kutoa huduma mbalimbali za kifedha kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu kiuchumi, hasa wanawake wanaoishi vijijini na maeneo ambayo upatikanaji wa huduma za kifedha ni mgumu. Lengo kuu ni kuweza kuwapatia fursa za kujiajiri, kujenga nidhamu ya matumizi ya kifedha, na kuendeleza ndoto zao za ujasiriamali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...