MRAJISI na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dk Benson Ndiege ameitaka Menejimenti ya Tume ya Maendeleo kuzingatia mifumo ya udhibiti iliyowekwa ikiwa ni pamoja kuzingatia sheria, taratibu na miongozo katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.
Dk Ndiege ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa wajumbe wa menejimenti ya Tume na kamati ya ukaguzi.
Amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuimarisha na kuendeleza vyama vya ushirika ili kuleta tija kwa wanachama na kuijenga Tanzania yenye uchumi wa kati kupitia vyama hivyo.
Amesema ni Imani yake kwamba kama vyama vya ushirika vikiendeshwa na kusimamiwa vizuri vinayo fursa kubwa ya kushiriki na kujenga uchumi wa Nchi na watu wake kwa ujumla.
" Ni jukumu la menejimenti kuhakikisha kuwa kazi zinatekelezwa kwa kuzingatia malengo ya Tume, mipango na mikakati ya utekelezaji wa majukumu inazingatiwa na inatekelezwa ipasavyo na pia kunakua na matumizi mazuri ya rasilimali fedha na watu," Amesema Dk Ndiege.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TCDC, Evance Assenga amesema wanachofanya katika kamati hiyo ni kupitia taarifa za mkaguzi wa ndani na nje pamoja na kushauri katika eneo la utawala bora.
Amesema wamekutana kwa mujibu wa sheria ambayo inawataka kukutana mara nne kwa mwaka na kwamba wataendelea kufanya kazi kwa maslahi mapana ya umma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...