NA YEREMIAS NGERANGERA…NAMTUMBO.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Julius Keneth Ningu ameahidi kumaliza mgogoro wa shamba uliodumu zaidi ya miaka minne toka kuanza kwa mgogoro huo mwaka 2017katika kijiji cha Mchomoro kati ya kijiji na mwekezaji.
Akiongea na wananchi wa kijiji cha mchomoro nje ya ofisi ya kijiji hicho mkuu wa wilaya ya Namtumbo aliwaahidi wananchi wa kijiji cha mchomoro kumaliza mgogoro uliojitokeza katika kijiji hicho kwa kuwa amejionea chanzo cha tatizo la kuzuka kwa mgogoro huo kwa kutembea kwa miguu katika shamba linalopigiwa kelele na kupitia vielelezo vilivyopo katika ofisi ya kijiji pamoja na kupata maelezo sahihi kutoka serikali ya kijiji iliyomaliza muda wake na serikali iliyopo madarakani.
Ningu pamoja na mambo mengine aliwaambia wananchi wa kijiji cha mchomoro kuendelea kuwa watulivu wakati serikali inalishughulikia swala hilo na kuhakikisha hakuna upande utakaoonewa katika kutoa ufumbuzi wa mgogoro huo.
Saidi Mkalela mwenyekiti wa kijiji cha mchomoro alimwambia mkuu wa wilaya huyo kuwa anayelalamikiwa ni aliyekuwa kuwa mkuu wa wilaya ya Namtumbo Luckness Adrian Amlima kwa kuingilia mashamba ya wananchi na kuyafyeka kwa kutaka kuyafanya sehemu ya mashamba yake tofauti na mashamba aliyopewa kisheria na kijiji.
“Taarifa nilizozikuta katika mihutasari ya kijiji na zipo katika mafaili ya kijiji kuwa Lucknes Adrian Amlima aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Namtumbo aliomba ekari 50 na wananchi kupitia mkutano wa hadhara wa kijiji uliridhia apewe ekari 40 ndicho ninachojua mimi” alisema mwenyekiti wa kijiji mbele ya mkuu wa wilaya huyo,
Ally Hassani na Mwanahamisi Gomo walitumwa na kijiji kumpimia aliyekuwa mkuu wa wilaya huyo maeneo ya wazi ekari hizo 40 na walimwonesha maeneo yote waliyoyapima na kuacha kupima katika maeneo ya mashamba ya watu lakini wajumbe hao nao walishangazwa na mwekezaji huyo kufanya tofauti na makubaliano ya kijiji .
Hassani Likwata ,Saidi Linyaka na Issa Likungwa wa kijiji hicho walisema wakati wanafuatilia haki yao walisha kamatwa na kufunguliwa kesi ya kuchoma vibanda vya mwekezaji huyo,kuvamia shamba la mwekezaji pamoja na kuiba vifaa vya mwekezaji huyo.
Wananchi wa kijiji cha Mchomoro walidai mgogoro kati ya mwekezaji huyo na wananchi ulianza toka mwaka 2017 ambapo wananchi wa kijiji cha mchomoro walikuwa wanamlalamikia mwekezaji huyo kukiuka makubaliano bila mafanikio ambapo kwa sasa mkuu wa wilaya Julius Ningu amewahaidi kumaliza mgogoro huo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...