Na Mwamvua Mwinyi,Mafia


MKUU wa wilaya ya Mafia ,mhandisi Martin Ntemo ,ameuagiza wakala wa ufundi na umeme  (TEMESA ) pamoja na mamlaka ya Bandari (TPA ) kuhakikisha wanashughulikia kero zinazolalamikiwa katika kivuko na Bandari ,ikiwa ni pamoja na kupitia upya nauli zinazotozwa kuwa kubwa kuliko uhalisia.

Aidha ,nauli itakayopangwa ipitishwe na mamlaka zenye dhamana ya kupanga viwango vya nauli katika vyombo vya usafiri.

Akitoa maelekezo hayo katika mkutano wa wadau uliohudhuriwa na mbunge wa Mafia Omar Kipanga ambapo wadau waliwasilisha kero zao kwa ujumbe wa TEMESA ili kufuatilia maelekezo ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi aliyoyatoa Julai 2021,alipotembelea eneo la Nyamisati ambako kivuko hicho huanzia safari zake kuelekea Mafia.

Mkuu wa wilaya hiyo Ntemo baada ya kupokea michango mbalimbali ya wadau ,alieleza kero hizo zimekuwa zikilalamikiwa kipindi kirefu hivyo kusababisha kudidimia kwa uchumi na maendeleo ya wilaya.

Ameiagiza TEMESA pia wakati ikipeleka timu ya ufuatiliaji maelekezo ya Naibu Waziri wa Ujenzi wahakikishe kero zilizotolewa na wadau zinafanyiwa kazi .

Hata hivyo ,aliwataka kufungua ofisi za kusimamia shughuli za kivuko na kukatia tiketi kwa upande wa Mafia na Nyamisati na mashine za kukatia tiketi ziongezwe.

Nae Kipanga ameeleza ,tayari amewasilisha barua na kumkabidhi mtendaji mkuu, ikielezea maeneo yenye kero.

Wakati huo huo ,Ntemo amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Ujenzi wa chuo cha VETA ambacho ujenzi wake uko katika hatua ya kukamilika.

"Chuo hiki ni sehemu ya mradi wa serikali wa Ujenzi wa vyuo 25 vya aina hii vinavyojengwa katika wilaya mbalimbali kwa gharama ya sh .bilioni 1.6 kwa kila chuo"

Ntemo pia alipitia ofisi za TANESCO kujionea mitambo inayozalisha umeme ambayo ndio chanzo cha nishati ya umeme wilayani humo ,ambapo Mafia inapata umeme unaozalishwa kwa mtambo wa dizeli .

Katika eneo hilo zipo jenereta tano zenye uwezo wa kuzalisha kilowatts 624 kila moja zote pamoja zikiwa na uwezo wa kuzalisha kilowatts 3,120 ikilinganishwa na mahitaji ya wilaya hiyo kilowatts 1,520 .







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...