Na Benny Mwaipaja, Tunduma

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewahakikishia wakazi wa Mji wa Tunduma, Wilayani Momba mkoani Songwe kwamba Serikali itatoa fedha sh. bil. 17 kwa ajili ya mradi wa kusambaza maji katika mji huo kutoka chanzo cha maji cha Mto Bupigu, kilichoko Wilaya ya Ileje.

Dkt. Nchemba alisema hayo Mjini Tunduma wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo wakiwemo wafanyabiashara katika Mpaka huo wa Tanzania na Zambia.

“Mama yetu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumtua ndoo mama kichwani kwa kuipa kipaumbele sekta ya maji, nimepokea maelezo yenu sisi watendaji wake ni kutekeleza ahadi alizowaahidi” Alisema Dkt. Nchemba.

Alifafanua kuwa Wizara itahakikisha inatoa kiasi hicho cha fedha ili wananchi hao wapate maji na kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji mijini unafikia wastani wa asilimka 95 na vijijini asilimia 85.

*Kuhusu kupanda kwa bei ya mbolea*

Dkt. Nchemba aliwajibu wananchi hao waliolalamikia kupanda kwa bei ya mbolea kwamba Serikali inalifanyiakazi suala la kupanda kwa bei hiyo na kwamba wataalam wa Sekta ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango wanapitia na kuyafanyiakazi masuala mbalimbali ya kisera yatakayosaidia kupungua kwa bei hiyo.

“Kupanda kwa bei ya mbolea hakutokani na kodi na tozo zilizoongezwa kwenye bajeti hii bali inatokana na kupanda kwa bei huko inakozalishwa nje ya nchi” Alisisitiza Mhe. Nchemba

*Kuhusu wafanyabiashara wa Tanzania kuhamia Zambia*

Aliwataka wafanyabiashara hao kurejea na kufanyabiashara nchini na kuwahakikishia kuwa malalamiko yao kuhusu kodi yatafanyiwakazi.

Wito huo ulitokana na baadhi ya wafanyabiashara kueleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wenzao wamehamishia biashara zao upande wa Nakonde nchini Zambia wakidai kuwa kufanya biashara upande huo kuna nafuu ya kodi ikilinganishwa na upande wa Tanzania.

“Wewe ni Mtanzania usiikimbie nchi yako, tutarekebisha matatizo, lakini kama umepata fursa ya kuwekeza huko, wekeza! Laniki usiikimbie nchi yako kwa sababu ya matatizo. Tanzania inaheshima ya kuzikomboa nchi zote hizi hatuwezi kushindwa kutenda haki kwa wananchi wetu” Aliongeza Dkt. Nchemba

Akutana na TRA na Wafanya Biashara.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kuweka utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara mara kwa mara ili kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kutoa stakabadhi za kielektroniki zikiwa na bei halali.

Aliwaonya pia wafanyabiashara kuacha tabia ya kuuza huduma na bidhaa zao kwa kutumia bei za aina mbili; moja ikiwa ni kuwauzia wateja bidhaa bila kutoa risiti au kuandika kiasi kisichosahihi akibainisha kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kwamba wakikamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akitoa taarifa ya utendaji, Meneja wa TRA mkoa wa Songwe Bw. John Micah alisema kuwa Mamlaka yake imefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji kodi ambapo katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2020/2021 walikusanya sh. bil. 92.7 sawa na ufanisi wa asilimia 115 ikilinganishwa na lengo walilowekewa la kukusanya sh. bil. 80.3.

Kwa upande wa wafanyabiashara, waliiomba Serikali kuhuisha masuala ya kodi ili waweze kulipa kodi kwa mamlaka moja badala ya kila taasisi kudai kodi na tozo mbalimbali jambo walilosema linawaletea usumbufu.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba yuko ziarani mkoani Songwe kukagua shughuli za maendeleo zinazohusiana na Wizara yake ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wafanyabiashara.



Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwapungia mkono mamia ya wakazi wa Mji wa Tunduma, Wilayani Momba mkoani Songwe, akiwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Mamlaka ya Mapato Tanzania na kutembelea baadhi ya njia za panya zinazotumika kupitisha bidhaa za magendo katika Wilaya ya Momba mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisoma baadhi ya mabango yaliyobebwa na baadhi ya wakazi wa Mji wa Tunduma, Wilayani Momba mkoani Songwe, waliozuia msafara wake akiwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Mamlaka ya Mapato Tanzania na kutembelea baadhi ya njia za panya zinazotumika kupitisha bidhaa za magendo katika mpaka wa Tanzania na Zambia katika Wilaya ya Momba.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwapungia mkono mamia ya wakazi wa Mji wa Tunduma, Wilayani Momba mkoani Songwe, akiwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Mamlaka ya Mapato Tanzania na kutembelea baadhi ya njia za panya zinazotumika kupitisha bidhaa za magendo Katika Wilaya ya Momba mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Mkazi wa Mji wa Tunduma, Wilayani Momba mkoani Songwe Bi. Thabita Shadrack, akifurahia jambo wakati Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akihutubia wananchi waliojitokeza barabarani na kuzuia msafara wake ili azungumze nao akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani Momba mkoani humo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba(Mb) (wa pili kushoto) alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mpaka wa Tunduma, wilayani Momba mkoani Songwe, akiwa katika ziara ya kikazi katika mpaka wa Tanzania na Zambia.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Bw. Misaile Mussa, alipotembelea Mpaka wa Tanzania na Zambia katika eneo la Kapele akiwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Mamlaka ya Mapato Tanzania na baadhi ya njia za panya zinazotumika kupitisha bidhaa za magendo katika Wilaya ya Momba.
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Tunduma, Wilayani Momba mkoani Songwe wakimshangilia Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akihutubia wananchi waliojitokeza barabarani na kuzuia msafara wake ili azungumze nao akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani Momba mkoani humo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (Katikati) akikagua eneo la Mpaka wa Tanzania na Zambia katika eneo la Kapele wilayani Momba mkoani Songwe akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo. Kushoto ni Mbunge wa Momba Mhe. Condester Sichalwe na kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Bw. Misaile Mussa.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Songwe Bw. John Micah, akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TRA katika Mpaka wa Tanzania na Zambia katika mpaka wa Tunduma kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) alipotembelea Ofisi hizo kukagua shughuli zinazofanyika mpakani hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe Bw. Fack Lulandala na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Songwe Bw. John Micah, wakifuatilia mkutano kati ya TRA na na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) alipotembelea Ofisi hizo kukagua shughuli zinazofanyika katika Mpaka wa Tunduma (Tanzania na Zambia).(Picha na Wizara ya Fedha na Mipango, Tunduma).




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...