* Shilingi bilioni 570 kuwanufaisha wanafunzi 160,000 mikopo ya elimu ya juu
* Watoa huduma za uombaji mikopo kwa njia za intaneti (Internet Cafe,) washauriwa kufanya kazi hiyo kwa uzalendo
SERIKALI kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepanga kutumia bajeti ya kiasi cha TZS 570 Bilioni katika mwaka 2021/2022 na kuwanufaisha zaidi ya wanafunzi 160,000.
Akizungumza leo (Ijumaa,
Julai 2, 2021) jijini Dar es salaam katika hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa
uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/2022, Waziri wa Elimu Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema kiwango cha fedha kilichotengwa kwa
2021/2022 kimevunja rekodi katika miaka 16 ya uhai wa HESLB.
Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako,
kati ya wanafunzi hao 160,000, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanatarajiwa kuwa
62,000 wakati wanaoendelea na masomo watakua 98,000.
“Niwaibie siri tu. Hadi mwezi
uliopita, bajeti ya mikopo kwa mwaka 2021/2022 ilikua TZS 500 bilioni. Lakini katika siku zake 100 za uongozi kama Rais
wetu, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan ameongeza TZS. 70 bilioni na kufikia hizi
TZS. 570 bilioni kwa mwaka 2021/2022 sawa sawa na ongezeko la TZS. 106 bilioni
(22.8%)” alisema Prof. Ndalichako.
Aliongeza kuwa ongezeko hilo linathibitisha nia ya
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan ni kuendelea
kuwawezesha vijana wengi kupata fedha na kusoma ili watumikie nchi yao na kuwataka
waombaji wahitaji watulie, na kusoma maelekezo na kuomba kwa usahihi ili
watimize ndoto zao.
Katika mwaka wa masomo wa
2020/2021, Serikali imetenga na kutoa TZS 464 bilioni zinazowanufaisha jumla ya
wanafunzi 149,398. Kati yao, wanafunzi 55,287 ni wa mwaka wa kwanza na wengine
94,111 ni wale wanaoendelea na masomo.
Aidha katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako aliitaka HESLB kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa waombaji ili waweze kuelewa sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa usahihi na kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwasaidia vijana wengi wanaoomba mikopo.
Pia Prof. Ndalichako amewataka watoa huduma za uombaji mikopo kwa wanafunzi (Internet Cafe,) kutoa huduma hiyo kwa uzalendo kwa kuhakikisha wanajaza taarifa hizo kwa ufasaha na si kwa kutanguliza mbele maslahi binafsi.
Akizungumza katika hafla hiyo
iliyofanyika katika ofisi za HESLB, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq
Badru amesema wamepokea maelekezo na kuanzia Julai 12 mwaka huu, maafisa wa
HESLB wataanza kuendesha programu za elimu ya uombaji mikopo kwa usahihi chini
ya kampeni ya #WeweNdoFuture.
“Tunakamilisha utaratibu na
uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili tuwafikie vijana wote waliopo
katika kambi 19 za JKT kuanzia Julai 12 … tutaendesha pia programu hizi kupitia
televisheni, redio, mitandao ya kijamii na mikutano na wadau,” amesema Badru.
Kuhusu utaratibu na muda wa
kuomba, Badru amesema Mwongozo wa
Uombaji mkopo unaoeleza sifa na utaratibu wa kuomba mkopo unapatikana katika www.heslb.go.tz kuanzia leo (Ijumaa, Julai 2,
2021).
“Mwongozo upo katika tovuti
kuanzia leo, Julai 2 na tunawashauri waombaji wausome kabla ya kuomba. Aidha,
mfumo wa kupokea maombi kuwa wazi kwa siku 53 kuanzia, Julai 9 hadi Agosti 31,
2021,” amesema Badru.
Mkutano huo wa uzinduzi pia
uliohudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Prof. James Mdoe na wawakilishi kutoka Shirika la Posta Tanzania (TPC) na
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambao pia huwahudumia waombaji
mikopo.
HESLB ilianzishwa kwa mujibu
wa Sheria, ikiwa na majukumu makuu ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na kukusanya
mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali kwa wanafunzi wa elimu ya juu tangu
mwaka 1994/1995.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...