Na. Shukrani Kawogo, Njombe.

Changamoto ya maji safi na salama imekuwa ni tatizo kubwa kwa maeneo mengi ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe na kupelekea wananchi kutumia maji ya mito ikiwemo na kutembea kwa umbali mrefu katika kuyafuata maji hayo.

Kutokana na changamoto hiyo mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amepambana katika kuhimiza serikali ili iweze kuleta miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ikiwemo kata ya Mlangali ambapo juhudi hizo zimezaa matunda kwani tayari baadhi ya maeneo yamefanikiwa kupata fedha za kuanzishwa kwa miradi hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa wananchi katika kijiji cha Lufumbu kata ya Mlangali pamoja na kijiji cha Ligumbilo wilayani humo Mbunge huyo amesema kuwa tayari serikali kupitia wizara ya maji imesha wasilisha kiasi cha shilingi milioni 50 kwaajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika kata ya Mlangali huku kijiji cha Liughai kilichopo kata ya Masasi kikitengewa milioni 381 na kijiji cha Kiyogo milioni 268 pamoja na maeneo mengineyo.

Ameongeza kuwa kilio cha maji kwa wakazi hao wa Mlangali anakifahamu ikambidi kuwasilisha tatizo hilo  katika  wizara ya maji akaambiwa kuwa kwa sasa suala haliwezi kuingia kwenye bajeti kwakuwa  tayari liko nje ya bajeti hiyo.

“Mpaka sasa tayari hatua za awali zimeshaanza kuchukuliwa katika kuanza mradi na tayari mabomba yamekwisha kununuliwa hivyo naomba nitoe rai kwa waandisi wetu kuzitumia vyema fedha kwa mahitaji husika”, Alisema Kamonga.

Aidha kwa upande wa wananchi wa kijiji cha Lufumbu pamoja na Ligumbilo wamemshukuru mbunge huyo kwa jitihada anazozifanya  kwani kero hiyo ya maji ni ya muda mrefu kwao.

Lidya Haule ni mkazi wa kijiji cha Lufumbu amesema kuwa tabu wanayoipata ni kubwa sana kwani wanatumia maji ya mto ambao una umbali wa zaidi ya kilometa mbili.

Aliongeza kuwa licha ya umbali huo pia maji hayo si salama kwa matumizi ya mwanadamu kwani mto huo hupita na taka taka nyingi ikiwemo matumizi ya wanyama kama ng'ombe na wengineo.

Naye diwani wa kata ya Mlangali Hamis Kayombo amewataka wananchi kumuunga mkono mbunge huyo kwani ana muda mfupi tangu aingie madarakani lakini maendeleo aliyoyafanya hayaendani na kipindi alichoshika madaraka.

Ameongeza kuwa Kamonga amekuwa ni mpambanaji katika kuleta maendeleo hayo amekuwa akiyatoa bila ubaguzi wowote bali kwa wananchi wa maeneo yote ya jimboni kwake.

Stanley Kolimba ni mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi wilayani Ludewa amesema licha ya elimu aliyonayo mbunge huyo lakini pia ana kalama ya uongozi kwani amekuwa akitumia muda mwingi kutafuta maendeleo ya wananchi ikiwemo kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.

"Mimi niliwahi kuwa mbunge mwaka 2000 hadi 2005 lakini kuna baadhi ya maeneo ya wananchi wangu sikuwahi kufika kuwatembelea na tatizo hilo si kwangu tu bali hata kwa baadhi ya wabunge waliopita lakini mbunge huyu Kamonga hakuna eneo analoliacha hivyo ni jambo la kumpongeza", Alisema Kolimba.

Wananchi wa kijiji cha Lufumbu wakimshangilia mbunge wao Joseph Kamonga baada ya kuwasili katika eneo la mkutano.
Mbunge wa jimbo la Ludewa (wapili kushoto) akiwa sambamba na diwani wa kata ya Mlangali(kushoto) wakipokelewa kwa  maandamano na wananchi wa kijiji cha Lufumbu baada ya kuwasili kwaajili ya kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akihutubia wananchi katika kijiji cha Lufumbu.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ( katikati) akiwa ameshika kuku aleyepewa zawadi na wananchi wa kijiji cha Lufumbu. Kulia kwake ni diwani wa kata ya Mlangali Hamis Kayombo na kushoto ni mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Lugumbilo alipowasili kusikiliza changamoto za wananchi hao.
 Wakazi wa kijiji cha Lugumbilo wakimpokea mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kwa kumtandikia khanga chini ili akanyage baada ya kuwasili katika kijiji hicho kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi hao.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...