Kaimu Postamasta Mkuu Bw.Macrice D. Mbodo akizungumza katika hafla ya kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya Mikopo kwa mwaka 2021/2022, iliyofanyika Julai 2, 2021 katika Ofisi za HESLB, Tazara Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akipokea nakala ya mwongozo wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/2022 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdful-Rzaq Badru mara baada ya kutangaza mwongozo huo leo Ijumaa Julai 2, 2021 katika Ofisi za Heslb, Tazara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe anayefuata ni Kaimu Postamasta Mkuu Macrice D. Mbodo.
Kaimu Postamasta Mkuu Macrice D. Mbodo akielezea jambo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako katika ofisi za HESLB kabla ya kuanza kwa hafla ya kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya Mikopo kwa mwaka 2021/2022, Tazara jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe akizungumza jambo katika ofisi za HESLB kabla ya kuanza kwa hafla ya kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya Mikopo kwa mwaka 2021/2022, Tazara jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, Kaimu Postamasta Mkuu Macrice D. Mbodo (kushoto) na Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru (kulia).
 


KAIMU Postamasta Mkuu Bw. Macrice D. Mbodo aeleza namna ambavyo Shirika la Posta Tanzania limejipanga kuhakikisha fomu zote za maombi ya mkopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu kwenda Bodi ya Mikopo (HESLB) zinafika kwa wakati katika ofisi za bodi hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/2022, jijini Dar es Salaam, ambapo Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice D. Mbodo amesema Shirika limejiandaa kuhakikisha maombi ya wanafunzi wa elimu ya juu yanaratibiwa vizuri na limetenga maeneo maalumu yakiwa na vifaa vyote kama Kompyuta sambamba na wafanyakazi waliokuwa tayari kuwasaidia wanafunzi katika kujaza fomu hizo.

Aidha, Mbodo alieleza kuwa Posta imejiandaa kuhakikisha maombi ya wanafunzi yote yanafika kwa wakati kwani Shirika limeboresha huduma zake za usafirishaji kwa kuboresha miundo mbinu ya usafiri na kwa kuwa kuna magari yanayotoka katika kila mkoa nchini kuja Jijini Dar Es Salaam na kwenda mkoani kila siku, hivyo yatawezesha fomu hizo kufika kwa wakati katika ofisi za Bodi ya Mikopo, jijini Dar es Salaam.

“Fomu zitakazokuwa zinawasilishwa, zinaletwa Bodi ya Mikopo kila siku mara tatu, asubuhi , mchana na jioni ili kuhakikisha hakuna uchelewesho wowote ule unatokea”. Alisema Mbodo

Macrice Mbodo, aliongeza kuwa, Shirika la Posta kushirikiana na HESLB wameunda kamati maalum ambayo itatumika kuelimisha na kutatua changamoto zitakazokuwa zinajitokeza katika mchakato mzima wa uombaji wa mikopo kwa wanafunzi ili ziweze kufanyiwa kazi kwa wakati.

“Shirika limeunda kamati maalum itakayoshirikiana na Bodi ya mikopo kuelimisha wananchi na kutatua changamoto zitakazokuwa zimewasilishwa kupitia ofisi zetu na dawati letu la wateja yaani “Customer care” na zitakazowasilishwa kwa Bodi ya Mikopo, na kamati hii itahakikisha wanafunzi wote wanapata huduma kikamilifu.”  Alisema Mbodo. 

Sambamba na hili Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo, alizungumzia huduma mpya inayotolewa na Shirika la Posta ijulikanayo kama Posta Kiganjani ambayo inamuwezesha mteja kufungua sanduku lake kupitia namba yake ya simu. 

Huduma hii itawawezesha wanafunzi watakaaomba mikopo kutumia namba zao za simu kama masanduku yao ya Posta, na kwa kuwa huduma hii inasajiliwa kwa njia ya mtandao inamwezesha mwanafunzi kufuatilia fomu yake ya maombi toka inapofikishwa katika Ofisi za Posta na mpaka kufika katika Ofisi za Bodi ya Mikopo.

Mbodo alieleza kuwa, huduma hii ya Posta Kiganjani inapatikana kwa kupakua “application” inayopatikana “Play Store” kwa kuandika “SmartPosta”, na baada ya hapo mwanafunzi ataweza kuandika taarifa zake kupitia fomu inayopatikana katika “Application” hiyo. Na hapo mwanafunzi ataweza kupata taarifa za fomu yake tangu inapoanza safari mpaka inapofika kwenye ofisi za HESLB.

“Shirika Posta limeanzisha huduma ambayo namba yako ya simu ndio sanduku lako, kwa hiyo muombaji usihangaike kufikiri anuani yako ukisajili namba yako ya simu kama anuani, utapata ujumbe unapotuma maombi yako na yanapopokelewa”. Alisema Mbodo.

Hata hivyo, Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice D. Mbodo, ametoa wito kwa waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kuwa, waombaji wafike mapema kukamilisha maombi yao na kuacha kusubiri mpaka siku za mwisho za ukomo wa maombi ya mikopo, kwani hii itasaidia kuepusha usumbufu wowote unaojitokeza wakati huo. Pia amewaomba waombaji wote wa mikopo ya elimu ya juu wafike katika ofisi za Shirika la Posta zilizo karibu yao ili waweze kuhudumiwa kwani Shirika limejipanga kikamilifu kuwahudumia.

“Tunawaomba waombaji wafike ofisi za Posta kuhudumiwa, tumejipanga kikamilifu, wasihangaike tumejipanga kuhakikisha waombaji hawa wanapata huduma bora na hawatapata tabu yoyote katika maombi yao”. Alisema Mbodo.

Hafla hiyo ya uzinduzi pia ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe na wawakilishi kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambao pia huwahudumia waombaji mikopo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...