Na Shukrani Kawogo, Njombe.
Imeelezwa kuwa kutokana na huduma ya elimu kuwa mbali na kupelekea watoto kushindwa kutembea kwa umbali wa km 9 kufuata elimu hiyo kwa wakazi wa kitongoji cha Mtemaluche kilichopo katika kata ya Lubonde wilaya ya Ludewa mkoani Njombe kumepelekea wakazi wengi wa kitongoji hicho kutojua kusoma na kuandika.
Kitongoji hicho ambacho kina wakazi zaidi ya 300 na wamekosa huduma ya elimu ya msingi na kuwalazimu watoto kutembea umbali huo kwenda Kiyombo ili kufuata elimu hiyo kitu ambacho kinawakatisha tamaa na kupelekea watoto hao kuwa watoro shuleni.
Wakizungumza hayo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga pamoja na diwani wa kata hiyo Edga Mtitu walipotembelea katika kitongoji hicho na kukuta wananchi hao wameanza kujenga chumba kimoja cha darasa ili watoto wao waweze kupata elimu kwa urahisi.
Nicholous Mtweve ni mmoja wa wananchi hao ameiomba serikali kupitia mbunge huyo kuwasaidia kukamilisha ujenzi wa shule hiyo kwani kwa nguvu zao wamejenga chumba kimoja cha darasa ambacho kinamaliziwa kukarabatiwa na wanatarajia mwakani wanafunzi wa chekechea waanze kusoma.
"Wakazi wa kitongoji hiki tunaipenda elimu ila tunaikosa kutokana na umbali, watoto wanatembea usiku tena njia zenyewe ni maporini hivi kwa hali hii hata kama kuna mtoto ana nia ya kusoma atasoma kweli? Serikali tunaomba ituone na sisi ili kitongoji cha Mtemaluche tuweze kupata elimu", Alisema Mtweve.
Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo amesema kuwa miradi inayoanzishwa na wananchi ni miradi endelevu na wanakuwa na uchungu nayo hivyo ataunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kuanzia ameahidi kutoa mifuko 50 ya saruji.
Sanjari na hilo mbunge huyo aliwaeleza wananchi wa kata hiyo ya Lubonde kuwa serikali imewaletea kiasi cha shilingi milioni 600 kwaajili ya ujenzi wa shule ya sekondari.
Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa elimu Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa kila jimbo kujenga shule hizo ambapo kwa jimbo hili la Ludewa shule hiyo itajengwa katika kata ya Lubonde.
"Wakazi wa Lubonde mmepata bahati ya kipekee sana ambapo katika kata zote 26 za jimbo hili kata yenu ndo imependekezwa kujenga shule hii hivyo mnapaswa kuunga mkono juhudi hizi zinazofanywa na serikali ili kuleta maendeleo katika maeneo yetu", alisema Kamonga.
Kwa upande wa diwani wa kata hiyo Edga Mtitu ameishukuru serikali na mbunge huyo kwa msaada huo kwakuwa uhitaji wa shule ya sekondari upo katika kata zote na kwa nguvu za wananchi ingewachukua muda mrefu kujenga sekondari.
Ameongeza kuwa kuna eneo lenye ekari 79 ambapo hekari 20 zitatumika kujenga shule hiyo na eneo litakalobaki litatumika kujenga zahanati na matumizi mengineyo.
Darasa lililojengwa kwa nguvu za wananchi wa kitongoji cha Mtemaluche ili kusogeza huduma hiyo jirani.
Baadhi ya viongozi wa CCM na serikali wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Lubonde. Kutoka kushoto ni diwani wa kata ya Lubonde Edga Mtitu, mbunge jimbo la Ludewa Joseph Kamonga, mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa CCM wilaya Stanley Kolimba na katibu wa CCM wilaya Bakari Mfaume.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Lubonde wakifuatilia mkutano wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph kamonga wakusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi.
Katibu ya CCM wilaya ya Ludewa akizungumza na wananchi wa kata ya Lubonde.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akiburudika na kikundi cha ngoma cha ngwaya alipofanya ziara katika kata ya Lubonde
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (aliyevaa miwani) akisalimiana na wananchi baada ya kuwasili katika kata ya Lubonde.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (wapili kulia) akiwa ameongozana na diwani wa kata ya Lubonde Edga Mtitu(watatu kulia) wakiwa wameongozana na baadhi ya viongozi wa CCM na serikali wakipita katika eneo lililotengwa kwa ujenzi wa shule ya sekondari.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...