WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi,Dkt. Leonard Chamuriho, ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kuhakikisha inasimamia ukusanyaji wa mapato yote ya Serikali na matumizi yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
Chamuriho ametoa maagizo hayo wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika leo mkoani Dar es Salaam na kuwataka kuwasilisha kwa wakati gawio la Shirika kwenye Mfuko wa Serikali.
Chamuriho ameiagiza bodi hiyo kuzingatia nyaraka na miongozo inayotolewa na Msajili wa Hazina na kuhakikisha uwepo na utekelezaji wa mikataba ya utendaji.
"Hakikisheni kuwa kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yenu kunakuwa na mkataba unaoeleweka kati ya Bodi na Msajili wa Hazina na mkataba kati ya Mkurugenzi Mkuu na Katibu Mkuu wa Uchukuzi." Amesema Chamuriho.
Aidha, ameitaka bodi hiyo kuhakikisha hakuna mgongano wa kimaslahi au kisheria na taasisi nyingine za Serikali katika utekelezaji wa majukumu ya Shirika.
Pia, ameiagiza bodi hiyo kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo changamoto za kiutendaji hususani zinazohusu majukumu ya kibiashara ili kuwahakikishia wateja wanapata huduma bora, zenye gharama nafuu.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi – Sekta ya Ujenzi, Gabriel Migire alisema kuwa sekta ya usafiri wa majini ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na hivyo wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanaitumia kwa kuboresha maslahi ya nchi.
Migire ameitaka bodi hiyo kuzingatia mipaka kati ya bodi na menejimenti na kuheshimiana ili kuendelea kukuza sekta ya usafiri wa majini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Kapt. Musa Mandia, amesema bodi imepokea maagizo hayo na kuwaahidi Waziri pamoja na Katibu Mkuu watayafanyia kazi.
Uteuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania ulianza rasmi tarehe 07 Julai 2021 ambayo inaongozwa na Mwenyekiti Kapt. Musa Mandia na wajumbe sita ambao ni Bi. Rukia Shamte, Bw. Said Nzori, Bw. Said Kiondo, Mha. Aron Kisaka, Kapt. King Kwirujila Chiragi na Bw. Casian Ngamilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...