Na Mwandishi Wetu,Michuzi Tv Moshi

Wito umetolewa kwa Asasi za kiraia hususani zile zinazopigania haki za binadamu nchini kuhakikisha kuwa wanazingatia haki za watoto wakati wanapotekeleza majukumu yao ili kulinda usalama na usiri kwa watoto. 

Hayo yamezungumza hivi karibuni mjini Moshi na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Tusonge, Aginatha Rutazaa wakati wa kuandaa washiriki katika maandalizi na utekelezaji wa majukwaa  ya jamii kwa Asasi 17 kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Akielezea maana ya Jukwaa la Jamii amesema ni mkusanyiko wa kundi (jamii) wenye lengo la kujadili jambo lililopo ndani yao kwa lengo la kupata suluhu au muafaka ambapo lengo ni kujadili masuala mazima yanayohusu ukatili wa kingono ndani ya jamii.

Amewataka washiriki wa mafunzo hayo ya siku mbili kuwa ni vema wakati wa kuandaa majukwaa hayo kuelezea sheria na taratibu zilizopo katika kusaidia wahanga wa ukatili, kuelezea taratibu zilizopo katika kufanya kazi na watoto na kuzingatia usalama na usiri wao ikiwa ni pamoja na kuielimisha jamii ili iweze kuzungumzia masuala ya ukatili wa kingono kwa uhuru na haki.

"Ni vema tuhakikishe tunatengeneza usiri katika mahojiano baina ya waathirika wa masuala ya ukatili wa kingono wakiwemo watoto kila tunapotekeleza majukumu yetu, tuzingatie miongozo na taratibu zilizopo ili tuleta tija kwa kile tunachokifanya" alisema Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kukuza Usawa kwa Kutumia Elimu ya Haki za Binadamu kutoka katika Shirika hilo, Consolata Kinabo aliwaambia washiriki hao kuwa lengo la Jukwaa la Jamii ni kutoa nafasi ya majadiliano jumuishi, salama na shirikishi kwa wanawake, wanaume, wasichana, vijana na watu muhimu kutafakari masuala ya ukatili wa kingono na kubainisha mikakati ya msingi ya kutatua.

"Umuhimu wa kutumia mbinu hii shirikishi ni ili kupata matokeo chanya ikiwemo kuongeza kujiamini, kujiheshimu kwa wanawake, wasichana na wavulana ili wajione wenye tija ndani ya jamii, lakini pia serikali kuongeza ulinzi kwao" Alisema Consolata.

Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo wanatarajia kujenga uelewa wa Haki za Binadamu na msingi wa maadili, kujenga uelewa wa Usawa wa kijinsia, kujenga uelewa wa ukatili wa kingono pamoja na utambuzi wa fursa na vizuizi kwa wanajamii katika kutatua ukatili wa kingono.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Community Economic Development and Social Transformation (CEDESOTA) Jackson Muro amesema kupitia mafunzo yanayotolewa na Tusonge kwa Asasi hizo, wanatarajia kuwa na jamii inayozingatia haki za binadamu isiyokuwa na vitendo vya ukatili wa kingono na yenye kuheshimu Usawa na kijinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Tusonge lenye Makao makuu yake mjini Moshi, Aginatha Rutazaa akitoa mafunzo kwa washiriki kutoka Asasi 17 kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Washiriki wakiwa katika vikundi vya majadiliano


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...