Na Muhidin Amri,Tunduru
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge, amewataka wazazi na walezi
katika wilaya ya Tunduru na mkoa wa Ruvuma kuchangamkia fursa ya
mafunzo ya ufundi yanayotolewa na chuo cha Nazareti kilichopo kata ya
Mbesa wilayani Tunduru badala ya kutumia muda mwingi kuwafundisha vijana
mila potofu zinazorudisha nyuma maendeleo.
Balozi Ibuge, amesema hayo baada ya kutembelea chuo hicho
kinachomilikiwa na Kanisa la Biblia Tanzania na kufurahishwa namna
kinavyotoa mafunzo kwa vijana na kwa weledi mkubwa pamoja na kuwa na
vifaa vya kisasa vinavyotumika kufundisha.
Hata hivyo, amesikitishwa na idadi ndogo ya wanafunzi waliopo licha ya
uongozi wa chuo kutoa nafasi kubwa na upendeleo kwa kuweka gharama
ndogo hasa vijana wanaotoka ndani ya wilaya ya Tunduru.
Chuo cha Nazareti Mbesa wilaya ya Tunduru kinafundisha masomo mbalimbali
ikiwemo Useremala na ufundi wa magari kwa lengo la kuwapatia ujuzi
vijana ili waweze kujitegemea mara baada ya kumaliza masomo yao.
Amesema,jambo la kusikitisha kuona kuna mwamko mdogo wa vijana hususani
wa wilaya ya Tunduru kwenda kupata ujuzi katika chuo hicho.
Aidha, amewasisitiza viongozi wa kata ya Mbesa na wilaya ya Tunduru
akiwemo Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini Daimu Mpakate kufanya jitahada
za makusudi kuhamasisha vijana wengi ili kujiunga na chuo hicho kwa
manufaa yao na jamii.
“nina fikiri kwa dhati kabisa mfanye jambo na vitu vitakavyosaidia
chuo iki kuwa na vijana wengi zaidi, unajua kuna ule msemo unaosema
kwenye miti mingi hakuna wajenzi na miti ipo kwa hiyo lazima
tuhamasishane ili tupate wajenzi wengi”
“Serikali haiwezi kuajiri vijana wote,kwani ina uwezo wa kuajiri
asilimia 3.1 tu sasa hawa wengine watakwenda wapi,kwa hiyo ni lazima
wajiajiri wenyewe”amesema Balozi Ibuge.
Amesema,uhamasishaji kwa ajili ya kupata vijana ni mdogo kwani chuo kina
uwezo wa kuchukua wanafunzi 96 na bado kuna wengine ziada 50
wanaoweza kujiunga bila kuhitaji kulala,lakini bado mwitikio wa
wanafunzi hasa wenyeji wa wilaya ya Tunduru kujiunga na chuo hicho ni
mdogo.
“apa kuna chuo kinachoweza kutoa huduma kwa jamii kwa kiwango kikubwa
lakini bado kinatoa kwa kiwango cha chini sio kwa sababu hakitaki bali
watu ndiyo hawataki”amesema.
Balozi Ibuge, ametaka uhamasishaji huo lazima uende kwenye kuondoa
mawazo mgando ya kijamii tuliyonayo hasa kuhusu mtoto wa kike kwa kuwapa
stadi za maisha yao na kuondokana na mila potofu.
Amesema, ana taarifa kwamba watoto kati ya miaka saba na minane katika
wilaya ya Tunduru wanafundishwa namna ya kuishi na wanaume, wengine
kuozeshwa wakiwa bado na umri mdogo jambo ambalo ni makosa makubwa.
Amesema, jamii na viongozi wa wilaya hiyo wana wajibu wa kuwapeleka
vijana shule na kuwapa stadi za maisha ili wapate elimu na baadaye kuwa
viongozi watakao iongoza Nchi yetu badala ya kuwafundisha mila potofu.
Balozi Ibuge ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama
mkoa amesisitiza kuwa, uhamasishaji na nguvu kubwa ujikite kuzungumzia
tabia na mila zisizofaa zinazopoteza muda wa maendeleo.
Amesema, chuo cha ufundi na Hospitali kinahitaji vijana wazawa na
wazalendo watakaofanya kazi kwenye taasisi hizo kuliko wanaokuja kutoka
nje ambapo ameitaka jamii ya wana Tunduru kuunganisha nguvu kwa kupata
vijana wengi watakaojiunga na chuo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Ezakiel Mapunda amesema, chuo kina
uwezo wa kuchukua vijana 96 kwa wa fani za ufundi magari na useremala,
hata hivyo waliopo kwa sasa hawafiki nusu ya uwezo wa chuo.
Amesema, chuo kilianzishwa kwa misingi ya kufundisha vijana wanaoishi
kuzunguka maeneo hayo na wilaya ya Tunduru ili wapate ujuzi
utakaowasaidia kujiajiri ,hata hivyo changamoto kubwa ni mwamko mdogo wa
wazazi kupeleka watoto kujiunga na chuo hicho.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mbesa Helga Amburste amesema,licha ya taasisi
hiyo kutoa huduma mbalimbali za kijamii na zinazochangia maendeleo,
lakini tatizo ni kutopewa hati miliki ya eneo lao.
Amemuomba Mkuu wa mkoa, kusaidia ili waweze kupata hati miliki ya ardhi yao ambayo wameiomba kwa muda mrefu.
,Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge kulia,akimsikiliza mkuu wa
chuo cha ufundi Nazareti Mbesa Ezekiel Mapunda kushoto namna chuo hicho
kinavyofanya kazi ya kutoa mafunzo ya ufundi wa magari na useremala
kwa vijana,katikati Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro.
Picha na Muhidin Amri,
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...