Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
Kaimu Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga amekanusha kujiuzulu katika nafasi hiyo baada ya kuwepo taarifa za yeye kuachana na Klabu hiyo kutokana na kushindwa kuelewana na Waajiri wake waliompa kazi hiyo siku chache zilizopita.
Kamwaga ametoa taarifa ya kanusho hilo leo Agosti 16, 2021 kupitia mitandao yake ya kijamii, huku akionyesha kushangazwa na taarifa hizo zilizoshtua Viongozi wa Klabu wakiwemo Wanachama na mashabiki wa Simba SC.
Amesema kuwa alipigiwa Simu na baadhi ya Waandishi wa Habari kwa lengo la kupata mizania ya taarifa hiyo (Balanced Story) kuhusu yeye kujiuzulu katika nafasi hiyo aliyopewa kukaimu kwa sasa, huku akisema tayari ilizua taharuki kwa Viongozi na baadhi ya Wanachama, Mashabiki wa Klabu hiyo.
“Uongo wa kupuuzwa. Nimeshangazwa na taarifa hizi zinazosambazwa na waandishi wenzangu - wengine wazoefu, kuhusu mimi kubwaga manyanga Simba.
Wengine wamenipigia simu ku 'balance' wakati tayari wameshasababisha taharuki isiyo na sababu kwa viongozi wangu, wanachama wenzangu na washabiki wa Simba kwa ujumla.
Nimepewa majukumu yangu mahususi Simba kwa muda wa miezi miwili na bado kazi hiyo sijaikamilisha. Nimedhamiria kukamilisha majukumu hayo mpaka ukomo wake.
Baada ya kuona usajili wa aina yake na mipango mikubwa mikubwa ya Simba ikiwa inatekelezwa, wabaya wetu wameibuka na uongo mwingine. Njia ya mwongo ni fupi.
Mimi bado nipo Simba. Tena bado nipo sana. Uongo huu dhidi yangu na Simba SC upuuzwe”, ameandika Kamwaga.
Ezekiel Kamwaga aliteuliwa na Simba SC katika nafasi hiyo ya Kaimu Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano baada ya Haji Manara kuondolewa katika nafasi hiyo kutokana na kutoelewana na baadhi ya Viongozi wa Klabu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...