Charles James, Michuzi TV

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe amewataka  wakutubi wote nchini kufanya kazi kwa bidii na kuongeza ubunifu Ili kuweza kurejesha utamaduni uliokuepo wa watanzania kujisomea.

Prof Mdoe ametoa kauli hiyo leo Mkoani Iringa wakati akizindua Maktaba ya Mkoa huo ambayo ilikua ikifanyiwa ukarabati na maboresho.

Ukarabati wa Maktaba hiyo umegharimu kiasi cha Sh Milioni 150.3 ambapo umeenda sambamba na Maktaba za mikoa mingine saba ambayo jumla yake ilitengewa kiasi cha Sh Bilioni 1.1 na Serikali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Prof Mdoe amesema maboresho hayo yamefanywa ikiwa ni mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kukarabati Taasisi zilizo chini yake na Maktaba zikiwemo lengo likiwa ni kukuza kiwango cha elimu nchini.

" Serikali kupitia Wizara yetu tumefanya maboresho makubwa kwenye Vyuo vyetu vikuu, na taasisi zake ambapo eneo la Maktaba ni wanufaika wakubwa wa maboresho haya ambayo yamelenga kurudisha kiwango cha elimu nchini pamoja na kuelimisha wananchi wetu ili waweze kushiriki katika kujenga uchumi wa kwao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Tumeanza maboresho haya kwenye baadhi ya Mikoa lakini lengo letu ni kusogea zaidi kwenye Maktaba za Mikoa na Wilaya zote nchini, rai yangu kwa wakutubi ni kuongeza ubunifu ili kuvutia wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kujisomea," Amesema Prof Mdoe.

Amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zilizopo ikiwemo uhaba wa rasilimali watu pamoja na maktaba hiyo kuunganishwa na mkonga wa Taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Maktaba Taifa, Mboni Ruzegela ameishukuru Serikali kwa maboresho makubwa iliyofanya kwenye maktaba nchini ikiwemo ya Iringa ambapo amesema kwa sasa maktaba hizo zitakua na muonekano wenye hadhi na kuvutia.

Amesema kiasi cha Sh Milioni 150 ambacho Serikali iliipatia Maktaba ya Iringa kimetumika kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali ambayo yalikua na changamoto na ujenzi huo umefanyika kwa mfumo wa 'force account'.

" Matumizi ya fedha ambazo tumepatiwa zimetumika kufanya maboresho ya mfumo wa maji safi na taka, umeme, kuziba nyufa, ukarabati wa paa, madirisha na milango, samani za ndani, marekebisho ya sakafu, kupiga rangi, maji, ufundi na usafiri.

Tunaishukuru Serikali kwa maboresho haya kwani licha ya kutuondolea changamoto zilizokua zikitukabili hasa wa paa kuvuja, mifumo ya majisafi na taka lakini pia umeipa hadhi Maktaba yetu na kuifanya kuwa na muonekano mzuri wa kuvutia kulinganisha na awali," Amesema Mboni.

Ameiomba Serikali kutatua changamoto yao ya ukosefu

 wa jengo la TEHAMA, kuunganishwa kwa mkonga wa Taifa pamoja na kuwaongezea rasilimali watu kwani idadi ya wanachama waliopo ni wengi kulinganisha na watumishi waliopo.

Nao wanachama wa Maktaba ya Iringa, Juma Kimenya na Shida Mgaya wameipongeza Serikali kwa kufanya maboresho hayo ambayo yameifanya maktaba ya Iringa kuwa na hadhi na yenye kuvutia huku wakitoa wito kwa wananchi kujenga utaratibu wa kujisomea.

" Niishukuru sana Serikali awali tulikua tunakuja hapa kupata huduma ya kujisomea lakini changamoto zilikua ni nyingi hasa uvujaji wa paa nyakati za mvua, mfumo wa maji lakini tumejionea maboresho makubwa yamefanywa na hakika inaridhisha kufika hapa," Amesema Kimenya.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe akikata utepe kuashiria kuzindua Maktaba ya Mkoa wa Iringa ambayo imefanyiwa maboresho na ukarabati uliogharimu Sh Milioni 150.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe akizungumza na wandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Maktaba ya Mkoa wa Iringa.
Mkurugenzi Mkuu wa Maktaba nchini, Mboni Ruzegela akizungumza na wandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Maktaba ya Mkoa wa Iringa ambayo imefanyiwa maboresho.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe akikagua Maktaba ya Mkoa wa Iringa kujionea ukarabati uliofanywa na Serikali kwenye maktaba hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...